Na Allan Kitwe, JamhuriMedia,Tabora

JESHI la Polisi Mkoani Tabora linamshikilia mtu mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua Juliana Mbogo (40) mkazi wa Mtaa wa Maselele kata ya Cheyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACSP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo majira ya saa 6 usiku wa kuamkia Agosti 13, mwaka huu, ambapo mtuhumiwa alifika nyumbani hapo majira ya saa 5 usiku na kumwamuru mtoto wa mama huyo akalale sebuleni.

Aliongeza kuwa ilipofika saa sita usiku mtuhumiwa alimyonga mama huyo kwa kutumia kamba ya filimbi na kisha akachukua mwili wa marehemu na kuutupa uvunguni mwa kitanda.

Kamanda Abwao alisema kuwa baada ya kupewa taarifa ya tukio hilo walianza uchunguzi ambapo walifanikiwa kumkamata mtu mmoja na wanaendelea na mahojiano na endapo atathibitika kuhusika na tukio hilo atafikishwa mahakamani.

Aliwataka wananchi kuacha kujichulia sheria mikono na kuacha kuuana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi au jambo lolote lile kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi, na ikithibitika sheria itachukua mkondo wake.

Aidha alibainisha kuwa kuendelea kuwepo kwa matukio ya mauaji kunachangiwa na jamii kukosa hofu kwa Mwenyezi Mungu, hivyo akashauri jamii kupendana na kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu ili kujiepusha na vitendo hivyo vinavyopelekea mauaji ya watu wasio na hatia.

Please follow and like us:
Pin Share