Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Adamu Kailanga (30), mfanyabiashara na Mkazi wa Mtaa wa Mkudi wilayani Ilemela mkoani Mwanza, anadaiwa kumuua mpenzi wake aitwaye Benadeta Silvester, (21), kwa kumkaba koo kisha naye kujiua kwa kujinyonga na mtandio.
Hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi kuhusiana na vifo vya watu hao wawili vilivyotokea mtaa wa Mkudi, wilayani Ilemela katika nyumba namba 50 inayomilikiwa na Juma Iddi Masolwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 5,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema Februari 4,2025 majira ya saa 8 mchana , Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo wakieleza kuonekana kwa miili ya watu wawili katika chumba cha kupanga katika nyumba hiyo.
Ambapo askari walifika eneo la tukio kwa wakati na kukuta mwili mmoja wakike ukiwa chini sakafuni na wakiume ukiwa unaning’inia juu ya paa la nyumba.
Mutafungwa amesema kuwa watu hao waliokutwa wamefariki dunia ni Adamu Kailanga na Benadeta Silvester,huku akidai kuwa zipo taarifa kuwa binti huyo ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari Korogwe iliyopo Mkoa wa Tanga na ufuatiliaji wa taarifa hizo unaedelea.
Pia amesema,baada ya kuwahoji majirani ilionekana kuwa kulikuwa na ugomvi miongoni mwa watu hao ambao ni wapenzi,kwani inadaiwa mwanaume alikuwa akimtuhumu mpenzi wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
Kwa mujibu wa Mutafungwa amedai kuwa majirani walimsihi mwanaume huyo atulie kwa kuwa migogoro ya kimapenzi ni mambo ya kawaida kwa watu wengi, ndipo mwanaume huyo alirudi ndani na hakutoka tena hadi majirani walipofungua mlango na kuwakuta wapenzi hao wakiwa wamefariki kisha kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
“Uchunguzi umefanyika na kubaini kuwa Benadeta Silvester, alifariki baada ya kukabwa
koo na Adamu Kailanga kifo chake kilisababishwa na kujinyonga kwa kutumia mtandio,chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi,”amesema Mutafungwa.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia wenza wao, pale kunapotokea migogoro ya kifamilia.Badala yake watumie njia sahihi ya kutatua migogoro hiyo ikiwemo kuwashirikisha wazazi wa pande zote mbili, viongozi wa dini na taasisi zinazoshughulika na utatuzi wa migogoro ya kijamii.
Aidha,amewasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.