Dalili za kufikia mafanikio ya kuboresha afya ya kina mama na watoto katika Mkoa mpya wa Simiyu, zimezidi kuonekana baada ya Shirika la Tafiti na Dawa Afrika (AMREF) kuwakutanisha wadau huduma za afya.

Hatua hiyo ya AMREF imekuja ikiwa ni miezi 11 imepita baada ya kuzindua rasmi mradi mkubwa unaojulikana kama Uzazi Uzima, unaolenga kuongeza kasi ya jitihada za kuboresha afya za makundi hayo ya jamii mkoani humo.

Wadau mbalimbali wa huduma za afya walioshiriki kikao hicho mjini Bariadi, Mei 2-3, mwaka huu, wametoka katika halmashauri za wilaya za Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu zinazounda Mkoa wa Simiyu.

 

Kikao hicho kimewashirikisha viongozi waandamizi wa Idara ya Afya katika halmashauri hizo na mashirika ya AMREF, IntraHealth, BMAF, World Vision, Engender Health, Marie Stopes na PSI, yanayoshughulikia huduma za afya katika jamii.

 

Katika hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mwamvua Jilumbi, amepongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kuiunga mkono Serikali kwa jitihada za kuboresha huduma za afya mkoani Simiyu.

 

 

“Serikali inathamini misaada ya mafunzo kwa watoa huduma, uhamasishaji na elimu ya afya kwa jamii, ukarabati wa vituo vya huduma za afya, vifaa tiba, dawa, vyombo vya usafiri, vifaa vya mawasiliano na huduma majumbani, inayotolewa na wadau mbalimbali. Misaada hii itasaidia kuboresha afya kwa wananchi wetu,” amesema Jilumbi.

 

Jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ambayo yamebeba vipaumbele muhimu vya kushughulikia, ambavyo ni afya ya mama, uzazi na mtoto, malaria, Ukimwi, kifua kikuu, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watoto wachanga na usafi wa mazingira.

 

Takwimu za kitaalamu zinaonesha kuwa wanawake 43 walipoteza maisha katika wilaya za Bariadi, Maswa na Meatu kwa mwaka jana pekee.

 

Sababu kuu za vifo hivyo zinatajwa kuwa ni kutoka damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, uzazi pingamizi, upungufu wa damu na kuharibika kwa mimba, huduma duni, fikra potofu, mipango dhaifu na vipaumbele butu kuhusu huduma bora za afya, magonjwa ya kuambukiza na idadi ndogo ya wataalamu wa afya ya mama na mtoto.

 

“Lakini pia kila mwaka tunapoteza wazazi kutokana na magonjwa ya Ukimwi na malaria. Wastani wa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Simiyu ni asilimia 7.3.

 

“Vilevile kulitokea vifo vya watoto 47 wenye umri wa chini ya wiki nne na vifo 422 vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano mwaka 2012,” ameongeza Jilumbi.

 

Wadau wanaelekeza msukumo mkubwa katika kupunguza maambukizi ya VVU, kuongeza watumishi wenye taaluma na vituo vya huduma za afya, bajeti ya huduma za afya na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

 

Pia kuna changamoto ya kudhibiti mifumo pingamizi ya kijamii, ukiwamo mfumo dume unaosababisha kina mama na vijana wakiwamo wasichana kuchelewa au kutopata huduma za afya, zikiwamo za uzazi wa mpango, hivyo kukumbwa na matatizo ya kiafya yasiyo ya lazima.

 

“Changamoto zote hizi zinachangia vifo vya wajawazito na watoto, hivyo zinahitajika nguvu na mikakati ya pamoja kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo hivyo,” amesisitiza Katibu Tawala huyo.

 

Kimsingi, kikao hicho cha wadau wa huduma za afya kimewawezesha kujua ukubwa wa changamoto zilizopo na jinsi ya kushirikiana kuzikabili.

 

“Dhamira ya mkoa wetu [Simiyu] ni kuondoa umaskini kupitia kwa wananchi wenye afya nzuri na wenye uwezo wa kuzalisha mali. Wananchi washirikishwe kikamilifu katika kutambua na kukabili matatizo katika jamii zao.

 

“Tutumie kikamilifu takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na utafiti wa kisayansi vituongoze katika kubaini maeneo ya kuelekeza nguvu kubwa ili kuleta mabadiliko ya huduma za afya mkoani hapa,” amesema Jilumbi.

 

Katika majadiliano yao, baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamependekeza uundwaji wa vikundi vya kijamii vya wanawake na wanaume, kwa ajili ya kuwasaidia kinamama wanaohitaji kujifungua.

 

Wengine wamesisitiza ujenzi wa vyumba vyenye mazingira rafiki kwa kinamama wanaokwenda kujifungua, vyenye vifaa vya kutosha na vinavyowatunzia siri. Vilevile bado kuna hitaji la kukazania utoaji elimu ya afya kwa jamii mkoani Simiyu, ikiwamo ya matumizi ya vituo vya huduma za afya.

 

Wakunga wa jadi na viongozi wa vijiji wasio waadilifu wametajwa kuchangia kudhoofisha mikakati ya kuhimiza matumizi ya vituo vya huduma za afya mkoani Simiyu. Mwongozo wa sekta ya afya nchini unakataza wakunga wa jadi kuzalisha wajawazito wanaohitaji kujifungua kwa sababu za usalama wa mzazi na mtoto.

 

Ukosefu wa wataalamu na vifaa vinavyokidhi mahitaji, unatajwa kuwa miongoni mwa sababu za wajawazito wengi kukwepa kwenda kujifungulia katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

 

Dk. Costa Mniko ni Meneja Programu wa AMREF mkoani Simiyu, aliyetangaza kung’atuka rasmi wadhifa huo kuanzia Mei 6, mwaka huu. Amelishukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Canada (CIDA) linalofadhili shughuli za AMREF.

 

Ofisa wa Idara ya Afya katika Wilaya ya Itilima, Kelisa Wambura, amesema Serikali imejipanga kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwamo AMREF na wananchi kwa jumla, kutekeleza mipango ya kuboresha huduma za afya wilayani humo.

 

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Lucy Mashauri, ametangaza kuwa milango ya wilaya hiyo iko wazi kwa kampuni, mashirika na wahisani watakaoguswa kuisaidia Serikali kuboresha huduma za afya kwa jamii.

 

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, John Aloyce, amesema Serikali inaona faraja kwa wadau mbalimbali wanaojitokeza kuisaidia katika jitihada za kukabili matatizo ya kiafya wilayani humo.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Busega, Dk. Redempta Natalis, ameshauri vikao vya aina hiyo viwe endelevu kwani vitaongeza ufanisi wa shughuli za uboreshaji wa huduma za afya katika jamii.

 

Ofisa Programu wa IntraHealth, Dk. Moshi Nsanye, amesema shirika hilo linaendelea kuimarisha mipango ya mafunzo kwa watumishi katika hospitali za Meatu, Maswa na Bariadi, na kugharamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa njia ya mkoba mkoani Simiyu.

 

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Matoke Muyenjwa, amewaasa wadau hao kutumia mada zilizojadiliwa katika kikao hicho ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.

 

“Halmashauri zetu zinapaswa kuimarisha mipango ya kuboresha huduma za afya kwa kuzingatia takwimu sahihi za watu na vitu wanavyoshughulikia. Tuelekeze juhudi kubwa katika kuweka mikakati ya kupunguza kama si kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU, vifo vya wazazi na watoto.

 

“Sisi kama mkoa, tutasimamia ipasavyo shughuli hizi. Halmashauri zishirikishe sekta zote kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma za afya ya jamii,” amesema Dk. Muyenjwa.

 

Utekelezaji wa mradi wa Uzazi Uzima katika Mkoa wa Simiyu unatarajiwa kuwa na mafanikio katika ujenzi wa dhana ya matumizi ya huduma bora za afya, kupunguza vifo vya wajawazito, wazazi, watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano.

 

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo Juni, mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, aliwahimiza wananchi kuuchangamkia waweze kunufaika nao ipasavyo. Shirika la AMREF linatajwa kuwa la kwanza kupeleka mradi wa aina hiyo mkoani Simiyu chini ya ufadhili wa CIDA.

 

“Mradi wa Uzazi Uzima ni kielelezo cha dhamira njema ya kuleta mabadiliko ya kupunguza vifo vya kina mama, watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano. Sote tuunge mkono mradi huu kwani fursa hii ni muhimu katika kutuwezesha kutimiza malengo ya kuboresha huduma za afya kwa kinamama na watoto mkoani hapa,” amesema Mabiti.

 

Mkurugenzi wa AMREF Tanzania, Dk. Festus Ilako, ameahidi kuwa ofisi yake itashirikiana na CIDA, bila kuiweka kando Serikali kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa uzito unaostahili mkoani Simiyu.

 

“Mradi huu utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu na nusu…Ulianza Novemba 2011 na unatarajiwa kukamilishwa Juni 2015,” amesema Dk. Ilako.

 

Mkazi wa mjini Bariadi, Salome James, ameeleza kupokea kwake kwa faraja mradi huo, akiufananisha na mkombozi wa afya ya mama na mtoto mkoani Simiyu.

 

Mradi wa Uzazi Uzima unatarajiwa kuwa suluhisho thabiti la matatizo ya watumishi wachache wa sekta ya afya wakiwamo wakunga wenye taaluma, matumizi duni ya huduma bora za afya zikiwamo za uzazi wa mpango.

 

“Katika kuongeza uwezo wa Serikali za Mitaa kuimarisha huduma bora za afya ya mama na mtoto, AMREF itawezesha mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa afya kusaidia kuboresha mifumo ya rufaa na tiba kwa ujumla,” ameongeza Dk. Ilako.

 

Makundi yanayolengwa kunufaika moja kwa moja na mradi wa Uzazi Uzima ni wajawazito 108,353, watoto wachanga 21,010, wenye umri chini ya miaka mitano 114,575, wafanyakazi wa afya 500, kamati za afya ya jamii 4,600, viongozi wa jamii 1,218, wanawake na vijana 400,000.