"Tukiulizwa na wenye kiburi na fidhuli ya wingi wa mali; mna nini, nyinyi Watanzania? Tunaweza kujibu, si kwa fidhuli, lakini kwa fahari kabisa: tuna umoja na amani; vitu ambavyo havinunuliki kwa kiasi chochote cha fedha.
"Tuna haki ya kujivunia umoja huu na amani hii, maana ndivyo vilivyotuwezesha kupambana na matatizo makubwa ya vita ya uchumi, na hata ya kisiasa. Tuna haki ya kujivunia kwa sababu umoja huu na amani hii havikuzuka vyenyewe tu; mbona havizuki kila mahali?
Wahenga wamesema, “Ukiona vinaelea vimeundwa.”  Umoja wetu na amani yetu ni mafanikio ya wananchi wa Tanzania chini ya uongozi wa chama chetu. Na sasa hivi umoja huu na amani hii, ndiyo nguvu kubwa ya watu na Taifa letu, wakati tunapambana na matatizo ya uchumi, na kejeli na fidhuli za maadui zetu.”
Nimenukuu maelezo hayo yaliyomo katika sehemu ya kwanza ya hotuba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitoa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu wa chama hicho, Oktoba 22, 1987 mjini Dodoma.
Sababu ya kunukuu ni kuwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba amani tuliyonayo ni muhimu sana kuliko mali tulizonazo na starehe tuzifanyazo. Pili, ni kurudia kutoa hadhari kwa wanasiasa wetu wenye akili za kukejeli, za kuleta chokochoko na za kugombanisha wananchi. Waache.
Leo ninapokumbusha maelezo hayo ni takribani miaka thelathini na mtoa nasaha hiyo hatunaye duniani. Mwenyezi Mungu amrehemu mja wake. Amin. Sehemu hiyo imejaa hekima na haina chembe chembe ya kuchujisha amana ya umoja na amani.
Hotuba ya Mwenyekiti Mwalimu Nyerere imetambaa katika maeneo matano. Amani na utulivu katika Tanzania; pili Tanzania haijawa bado jamii yenye haki. Msimamo huu unaweza kutiliwa shaka. Chama kina kazi tatu na mwisho ni maoni ya mtoa hotuba.
Tangu tuwe na vyama vingi vya siasa nchini, tumeshuhudia migongano ndani ya vyama hivyo ya kugombea madaraka, ruzuku, usaliti na wakati mwingine viongozi kukimbiana kukutana ana kwa ana ili wasikabili ukweli wa mambo na kutoa vizibiti vitakavyosaidia kutanzua matatizo.
Si hivyo tu, hata chama na chama kwa maana ya ama baadhi ya wanachama au viongozi kuwekeana hiyana, choyo au wivu wasipate na kufanikiwa. Wanasahau umoja na amani na taratibu za demokrasia zikiwamo za kuzingatia taaluma na uwezo wa fikra na kazi.
Haifai wala si haki kila mmoja kumuona mwenzake ni msaliti. Dawa ya usaliti ni kukaa pamoja katika meza ya duara: jicho kwa jicho; ukweli juu ya ukweli na ushahidi juu ya ushahidi. Hapo ustaarabu na heshima vitapata nuru; demokrasia na Katiba zitapata haki yao.
Bila ya kufanya hivyo, ni kuwapa ‘kiki’ wapambe uchwara kutamba na kutenganisha wanachama na Watanzania kuvunja umoja na amani. Muda unaopotezwa katika malumbano ya kisiasa, kukimbiana, kuogopana na kuhisi kudhalilika unapita kama moshi na kamwe hautarudi wala kupatikana tena.
Hotuba ya Mwenyekiti inatoa mwanga kwa wana-CM na Watanzania kufanya mabadiliko katika mifumo ya siasa na uchumi kulingana na wakati uliopo bila ya kuathiri umoja, amani na utoaji wa haki zaidi kwa Watanzania wote.
Migogoro ndani ya vyama vyetu isiwe na nafasi wala isipewe chambi kwa sababu si mtaji wa ujenzi wa chama chochote chenye nia ya kuongoza Serikali, yenye majukumu ya kuleta maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii ya Watanzania.
“Na sasa hivi umoja huu na amani hii, ndiyo nguvu kubwa ya watu na Taifa letu, wakati tunapambana na matatizo ya uchumi, na kejeli na fidhuli za maadui zetu.” Kauli hii ni ya maana na muhimu sana Watanzania tunaosafiri katika awamu ya tano inayohitaji kuimarisha uchumi kwa njia ya viwanda na kuchapa kazi.
Shughuli haziwezi kufaulu iwapo amani na utulivu haupo kutokana na umoja na mshikamano unayumba. Haki inagongwa nyundo na kuzuiwa kwa mapambo ya demokrasia na utawala wa sheria uliojaa kejeli na fidhuli. Turudi na kuzingatia amani na utulivu katika Tanzania.