Aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba nchini na Katibu Mkuu Msaidia Marco Masanja amefariki nchini China akiwa kifungoni.

Marehemu ambaye alikuwa kiongozi katika miaka kadhaa huko nyuma, alifariki dunia tarehe 10 Februari mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia wa mwanamichezo huyo zinasema, Masanja alifariki dunia kutokana na maradhi ambayo hayakutajwa.

Kiongozi huyo wa zamani wa Simba, alikamatwa nchini China, akituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya. Alihukumiwa mwaka 2013, kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.

Taarifa zinasema, alitarajiwa kumaliza kifungo chake, mwaka 2025.

“Ni kweli kwamba ndugu yetu, kaka yetu, baba yetu na mwanafamilia wetu, Marco Masanja, amefariki dunia akiwa anatumikia kifungo chake nchini China,” ameeleza Salum Malilima, mmoja wa wanafamilia wa marehemu.

Anaongeza, “hatufahamu mazishi yake yatafanyika lini. Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa marehemu atazikwa huko huko China kwa sababu ya ukubwa wa gharama za kuusafirisha mwili wa kuja Tanzania.

Alikamatwa katika mji wa Guangzhou, akituhumiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kula njama, kusambaza na kusafirisha madawa ya kulevya. Serikali ya China, imeweka sheria kali kwa watu wanaopatikana na makosa ya aina hiyo.

Please follow and like us:
Pin Share