Raymond Mkulo (29) anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Novemba 18, mwaka jana katika ufukwe wa Coco, Dar es Salaam, naye amerejeshwa kwa mtindo unaoshabihiana na ule uliotumika kumrejesha mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo).

Mkulo alipotea kwa siku 47 tangu alipotekwa akiwa kwenye gari lake aina ya Noah lenye namba T 961 DCJ. Gari hilo ndilo linalodaiwa kukodiwa na watu wawili waliotaka awapeleke katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro.

Mkulo ameonekana Januari 4, mwaka huu saa 2:45 usiku katika eneo la Kongo Bar lililopo katika ufukwe wa Coco mahali ambako ndiko anadaiwa kutekwa.

Mzazi wa Raymond, Moses Mkulo, amelieleza JAMHURI kwamba siku hiyo alipigiwa simu na mtoto wake huyo akamchukue eneo la Kongo Bar baada ya kurejeshwa na watu waliokuwa wakimshikilia mateka. Baba huyo alikuwa nje ya Dar es Salaam.

“Watekaji walimpa simu yao ya kiganjani ambayo siwezi kuitaja kwa sasa hadi polisi watakapomaliza uchunguzi wao ili awasiliane nami kwamba yuko Kongo Bar tukamfuate.

“Alipochukuliwa wakaenda moja kwa moja Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa ajili ya kutoa taarifa ya kupatikana, lakini wakashindwa kuendelea na mahojiano naye kwa kina kwa sababu alikuwa anaonyesha kama amechanganyikiwa.

“Pia alikuwa na maumivu makali kwenye miguu, hivyo wakaomba arejeshwe tena Jumatatu (jana) kwa ajili ya kuendelea na mahojiano … anaonekana kujaa hofu anapotakiwa kuelezea mkasa huo,” amesema Mkulo.

Amelishukuru Gazeti la JAMHURI kwa kuandika kwa undani kuhusu tukio la kutekwa kwa mtoto wake huyo, akiamini habari hiyo imesaidia kurejeshwa kwa mtoto wake.

“…Mmeandika kwa usahihi na bila woga wowote kuhusu tukio hili na matokeo yameonekana sasa kwani amerejeshwa,” amesema.

Amesema wamebaini baadhi ya vifaa vya gari likiwemo gurudumu la akiba vimeibwa.

Tukio lilivyokuwa

Mama mzazi wa Raymond, Editruda Muhozya, mkazi wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam anasema Novemba 18, mwaka huu, saa 11:30 mtoto wake huyo alikuwa Hospitali ya Sinza na mchumba wake aitwaye Rut aliyekuwa mgonjwa.

Anasema saa 11:34 jioni waliwasiliana naye kuhusu majukumu ya kifamilia aliyoagizwa na baba yake siku hiyo.

Baadaye kidogo walipomtafuta saa 1:30 jioni hawakumpata kupitia namba zake zote tatu za simu, hali iliyowapa wasiwasi.

Raymond anaishi Sinza Kijiweni, Dar es Salaam akiwa na mchumba wake na mtoto wao wa miezi miwili.

Raymond amenukuliwa akisema baada ya baba yake kuzungumza naye alipigiwa simu na mtu aliyemtaka awapeleke Mikumi, hivyo baada ya matibabu, akiwa na mchumba wake walikwenda Coco Beach ambako walikutana na watu wawili.

Kati ya watu hao alikuwepo mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 50 na mwanamke mwenye umri wa miaka 25.

Mchumba wake anasema watu hao hawakuwa na begi, lakini walikuwa na bahasha mbili.

Watu hao waliingia ndani ya gari na Raymond akaagana na mchumba wake muda ukiwa ni saa 12:15 jioni. Rut akaenda kwao Masaki.

Anasema waliendelea kumtafuta kwa siku tatu kupitia kwa ndugu zao sehemu mbalimbali na kufuatilia katika Hifadhi ya Mikumi bila mafanikio. Wakatoa taarifa Kituo cha Polisi Urafiki Novemba 21 na kufunguliwa jalada lenye namba URF/RB/8116/2018.

Walishauriwa wapite hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuchunguza katika wodi za wagonjwa na vyumba vya kuhifadhia maiti ili kubaini kama watamwona Raymond.

“Baadaye tulienda katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako walimhoji mchumba wake (Rut), kufuatilia kwa rafiki zake na kampuni za simu.

“Tunachosema hakuna mwanadamu yeyote hapa duniani mwenye uwezo kumshinda Mungu wetu au akafanya uovu wowote na kudhani kwamba anaweza kujificha asionekane, hivyo bado tunaamini yote yatakuwa wazi,” alisema mama alipozungumza na JAMHURI.

Siku moja kabla ya Raymond kutoweka alituma picha kwa mama yake mzazi akiwa amepiga na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ambaye wamekuwa marafiki wa muda mrefu. JAMHURI lilimtafuta Lugola bila mafanikio.

Mkulo ni mhitimu wa kozi ya ugavi katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) mkoani Dodoma. Alijiendeleza kwa kuchukua kozi ya udereva katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kufuzu mafunzo ya udereva wa viongozi.

Miongoni mwa viongozi aliowaendesha ni aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli. Raymond ni ndugu yake Lembeli.

Lembeli alieleza kushtushwa na taarifa za kutekwa kwa Raymond.

Anasema alikuwa anamtumia kama kijana wa nyumbani na kwamba mwaka 2005 aliwahi kuwa dereva wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Amekuwa dereva wa mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mgonelwa. Vilevile amekwishawahi kuwapeleka wageni maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mikumi. Wazazi wake wanasema si mgomvi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jumanne Murilo amesema Raymond alipatikana ufukwe wa Coco baada ya watekaji kumrejesha.