Mtu mmoja aliyepigwa risasi na polisi akiwa maeneo ya Ikulu Ndogo inayotumiwa na Makamu wa Rais jijini Mwanza atafikishwa mahakamani baada ya matibabu.

Raia huyo amelazwa Hospitali ya Rufaa mkoani hapa ya Sekou Toure akiendelea kuuguza jeraha la risasi mwilini mwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, amelithibitishia Gazeti la JAMHURI akisema tukio hilo limetokea Machi 11, 2019 mchana na kusisitiza kuwa ifahamike polisi hufanya ulinzi kwa kutumia silaha za moto, si manati, kwa hiyo amri zao ni lazima ziheshimiwe.

Ikulu hiyo ndogo ipo katikati ya msitu mnene, kwenye Mlima wa Machemba, karibu na zilipo Ofisi za Jiji la Mwanza.

Awali yalikuwa makazi ya mkuu wa mkoa huo kabla hajahamia eneo la Kiseke, Manispaa ya Ilemela.

Kulingana na Kamanda Muliro, mtu huyo ambaye hajatajwa majina na makazi yake rasmi, siku ya tukio alijaribu kuingia ikulu kufanya uhalifu.

Amesema awali mtu huyo alikaidi amri ya askari alipotakiwa kujisalimisha, ambapo alianza kutimua mbio na wenzake wawili kukwepa kukamatwa.

Muliro amekaririwa akisema kuwa askari wanaolinda eneo hilo waliwabaini ‘wahalifu’ hao na kuwaamuru wasimame lakini walikaidi amri halali.

“Kwanza ni kweli hilo tukio lipo. Aliingia na wenzake wawili waliofanikiwa kukimbia. Waliangalia polisi wapo huko wakapita kule.

“Amepigwa risasi moja. Namuombea apone haraka tumpeleke mahakamani,” RPC Muliro ameliambia JAMHURI katika mahojiano yake.

Amesema wenzake wawili walifanikiwa kutokomea kwenye msitu unaozunguka ikulu hiyo ndogo huku majeruhi huyo akikimbizwa hospitalini kupata tiba.

Akijibu swali aliloulizwa iwapo watu hao waliingia kwa kuvunja uzio wa seng’enge unaozunguka ikulu hiyo, amesema si lazima wavunje, kwani wahalifu wanaingia hata kwenye uzio wa ukuta.

Alipoulizwa iwapo mtu huyo aliingia katika ikulu hiyo na silaha, alisema: “Hao hawaachani na mapanga. Wanatembea na mapanga ya kuvunjia milango na makufuli.”

Gazeti hili limeona ikulu hiyo iliyo kando na Hospitali ya Sekou Toure imezungushiwa uzio wa seng’enge.

“Sisi tukisema tunalinda, tunalinda kweli kweli. Wewe ukiandika Ikulu Mwanza yaibiwa, kuna maswali saba ya kujiuliza.

“Yaibiwa polisi wakilinda, wakiwa na SMG mbili…(kicheko) imeibiwaje? Sisi hatutaki hayo mambo.

“Unaamrishwa simama hutaki, nani kakuambia sisi tunalinda na manati?” amehoji Kamanda Muliro huku akitoa onyo dhidi ya magenge ya wahalifu mkoani hapa kuacha hulka hiyo.

Wakati polisi ikisema hayo, habari zaidi zinabainisha kuwa mtu huyo anadaiwa ni mtumiaji wa dawa za kulenya.

Kwamba siku ya tukio majeruhi huyo na wenzake (hawajatajwa idadi) walikuwa kando ya mlima wa ikulu wakitumia dawa hizo zilizopigwa marufuku nchini.

Inadaiwa baadaye alikwenda kujisaidia haja kubwa kando ya msitu huo akiwaacha kando wenzake.

Duru za habari zinadai askari watatu wenye silaha waliokuwa wakiingia katika zamu ya ulinzi ikulu walimuona akijisaidia wakamkamata.

“Baada ya kukamatwa alipelekwa kule juu zilipo ofisi za ikulu, kisha akaanza kupigwa. Akiulizwa kwa nini alikuwa anajisaidia haja kubwa pale. Baadaye aliachiwa akapewa amri ya kukimbia ili kuondoka. Wakati anakimbia akawashwa risasi.

“Nimeambiwa watu wa vyombo vya usalama wamefuatilia hadi hospitalini, akawaeleza ilivyokuwa. Akaenda hadi kuwaonyesha kile kinyesi, wakakipiga na picha. Askari polisi watatu waliohusika wamekamatwa. Wamo ndani,” kilidokeza chanzo chetu cha habari kikimnukuu ofisa mmoja wa idara nyeti jijini Mwanza.

Hata hivyo, Kamanda Murilo alipoulizwa juu ya madai hayo alicheka kisha kukanusha akidai ni taarifa za kufikiria tu.

“Mimi ndiye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, nasema hakuna askari aliyekamatwa. Hivi mtu anayetumia dawa za kulevya anaweza kupata nguvu za kupanda mlima huo? Katiba ya nchi imetoa uhuru wa mtu kusema,” amesema RPC Muliro.

Gazeti hili halijafanikiwa kumuona majeruhi huyo hospitalini hapo kulingana na mazingira ya ulinzi yaliyopo.

Habari zinasema siku za nyuma watu wanaodaiwa kuwa wezi waliwahi kuingia katika ofisi hizo za ikulu ndogo inayolindwa na polisi, kisha kuiba vitu mbalimbali.

Kamanda Muliro ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) amethibitisha kuwahi kutokea uharamia huo katika ofisi hizo nyeti.

RPC Muliro ameliambia gazeti hili kuwa: “Kipindi cha huko nyuma kabisa wezi waliwahi kuingia na kuiba TV na vitu vingine.”

Wachambuzi wa mambo wametilia shaka usalama uliopo katika maeneo nyeti ya taasisi za umma, wakihoji iweje magenge ya kihalifu kujipenyeza na kuiba vitu, Ikulu ya Rais?

“Ulinzi na umakini uongezwe zaidi, maeneo nyeti kama ikulu na kwenye majengo mengine ya taasisi binafsi.

“Vifaa vya kiulinzi viongezwe maeneo yote muhimu. Hatutaki kushuhudia matukio ya kihalifu, yanayotokea nchi za wenzetu yakiingia Tanzania. Nchi yetu inasifika kwa ulinzi na usalama. Tusiipoteza hii bahati,” anasema Edson Njau.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza wameshauri vyombo vya usalama nchini kuongeza kasi ya udhibiti wa makundi ya kihalifu.

“Wanaweza kuweka kamera. Usalama wa raia ni muhimu sana. Maeneo ya miji mikubwa ulinzi uimarishwe.

“Kwenye majengo ya vitega uchumi napo paangaziwe na viona mbali,” anasema Joshua Mahalu, mkazi wa Mwanza.

Miezi kadhaa iliyopita watu saba wanaohisiwa kuwa ni majambazi waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi kwenye mlima mojawapo eneo la Kishiri jijini hapa.

Mauaji mengine yalifanyika Wilaya ya Ukerewe, Mwanza kabla ya mashambulizi mengine yaliyosababisha vifo vya watu wanaodaiwa kuwa majambazi kufanyika eneo la Nyashana.

Hivi karibuni watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi eneo la Igogo – Mulungushi, Wilaya ya Nyamagana jijini hapa.

Polisi inasema watu hao walikuwa wakijaribu kuvunja ghala la kuhifadhia vifaa mbalimbali, wakiwa na nia ya kuiba.

Katika tukio hilo bunduki aina ya shotgun, risasi, mkasi wa kukatia vyuma na kufuli, mapanga na funguo mbalimbali vilinaswa.