Mwanamume mmoja raia wa Uganda anayedaiwa kupatikana na mafuvu 24 ya vichwa vya binadamu huenda alikuwa akiyatumia kutoa kafara ya binadamu na anaweza kufungwa jela maisha, polisi wameiambia BBC.
Msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema mshukiwa, Ddamulira Godfrey, atafunguliwa mashtaka chini ya Sheria ya Kuzuia na Kukataza Kafara za Kibinadamu.
Mabaki ya wanyama na ngozi pia yalipatikana katika hekalu la Bwana Godfrey katika viunga vya mji mkuu, Kampala.
Polisi wangali wanasaka madhabahu ya Bwana Godfrey kwa matumaini ya kupata mabaki ya binadamu zaidi.
Onyo: Taarifa hii ina picha ambayo baadhi ya watu wanaweza kuiona ya kuhuzunisha
“Tunamshtaki kwanza chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupiga Marufuku Kafara ya Binadamu, ambayo [inakataza] mtu kuwa na sehemu za mwili wa binadamu na vifaa vinavyoonyesha kafara ya binadamau,” Bw Onyango alisema.
“Iwapo atapatikana na hatia, atatumikia kifungo cha maisha jela.”
Bwana Godfrey anadai kuwa ni mganga wa kienyeji na mitishamba. Hata hivyo, Chama cha Waganga wa Jadi nchini humo kimejitenga naye.
Hii si mara ya kwanza kwa ugunduzi huo wa kushtua kufanywa nchini Uganda katika wiki za hivi karibuni.
Mwezi uliopita, polisi walipata mafuvu 17 ya vichwa vya binadamu kutoka kwenye kaburi moja katika wilaya ya kati ya Mpigi, yapata kilomita 41 kutoka Kampala.
Ugunduzi huo wote umehusishwa na kafara ya binadamu kwa madhumuni ya kitamaduni.
Baadhi ya watu katika nchi nyingi za Kiafrika wanaamini kwamba hirizi za uchawi zinazotengenezwa kutoka kwa viungo vya mwili wa mwanadamu zitawaletea bahati nzuri, kwa mfano utajiri, au kulaani adui zao.