Meneja wa Fedha wa kampuni za ujenzi za Dott Services (TZ) Ltd na General Nile Company for Roads and Bridges/Dott Services JV, Suresh Kakolu, amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni moja, hivyo kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kutoa rushwa.

Kakolu amekiri kumhonga Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania mkoani Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, dola 2,000 za Marekani (Sh milioni 4.6 kwa viwango vya kubadilisha fedha wiki iliyopita).

Kakolu alikamatwa na makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Novemba 15, mwaka huu katika ofisi za TRA mkoani Kilimanjaro.

Ilielezwa kuwa alitoa kiasi hicho cha fedha kwa meneja ili apitishiwe maombi ya msamaha wa kodi wa ya Sh bilioni 6.604.

Kampuni hizo mbili zinadaiwa kodi hiyo tangu mwaka 2013 hadi Oktoba, mwaka huu. Alifikishwa mahakamani Novemba 16, mwaka huu.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi, Sophia Massati, alisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Rehema Mteta, kwa kosa moja la kutoa rushwa ya dola 2,000 kinyume cha Kifungu cha 15(1), (b) na Kifungu kidogo (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Alikana mashtaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Novemba 30, mwaka huu ambapo alikiri kosa lake na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni moja. Mshtakiwa alilipa faini.

Baada ya hukumu hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, aliliambia JAMHURI kuwa dola 2,000 zilizotolewa na Kakolu serikali imezitaifisha.

Ametoa mwito kwa watumishi wa umma na taasisi za serikali kutofumbia macho vitendo vya rushwa.

Wakati huo huo, maofisa wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, James Merisho na Mathias Gungumka, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rombo kwa kosa la kudai na kupokea rushwa kutoka kwa mmiliki wa kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mashati Oil Investment, Sabas Shirima.

Merisho ni mwakilishi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Wilaya ya Rombo; na Gungumka ni Ofisa Mazingira na Taka Ngumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

Washtakiwa hao walikifikishwa mahakamani wiki iliyopita mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Regina Futakamba, na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Barry Galinoma.

Wanatuhumiwa kudai na kupokea rushwa ya Sh 100,000 kutoka kwa Sabas Patrick Shirima katika tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 22, mwaka huu.

Watuhumiwa walikana mashtaka na wako nje kwa dhamana hadi Januari 16, mwakani shauri litakapopelekwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Kabla ya kuwapo madai ya rushwa, Novemba 5, mwaka huu, Mkaguzi kutoka TFDA Kanda ya Kaskazini, Halifa Sume, akiwa na mshtakiwa wa kwanza, Merisho walifanya ukaguzi katika kiwanda hicho na kubaini upungufu kadhaa.

Miongoni mwa upungufu huo ni eneo la uzalishaji kutumika kuhifadhi malighafi na kutokuwapo mashine za kupima ujazo mbalimbali wakati wa kujaza mafuta katika vifungashio.

Taarifa ya TAKUKURU kwa vyombo vya habari ilisema James alishinikiza kiwanda hicho kifungwe, lakini Mkaguzi wa TFDA alitoa muda kwa wamiliki kurekebisha kasoro hizo.

Novemba 22, mwaka huu, Merisho alimpigia simu mmiliki wa kiwanda hicho akimjulisha kuwa yeye na mwenzake wanakwenda kukagua utekelezaji wa maagizo ya TFDA huku akitaka waandaliwe Sh 100,000 kwa ajili ya kazi hiyo.

Mmiliki alitoa taarifa TAKUKURU na ukawekwa mtego na baada ya washtakiwa hao kufika kiwandani walifanya ukaguzi na kupewa fedha walizotaka.