Na Tatu Saad, Jamhuri Media
Mwili wa aliyekuwa beki wa mtibwa Sugar Iddy Mobby umezikwa leo katika makaburi ya mshikamano, Ngokolo mjini Shinyanga.
Mwili huo umehifadhiwa katika nyumba yake ya milele baada ya kufanyiwa ibada katika msikiti wa Madrasatu Aqswa huko Ngokolo.
Mwili wa Mobby uliwasili salama jijini Shinyanga usiku wa jana ukisindikizwa na baadhi ya wachezaji kama Mohammed Makaka akiambatana na Vitalisy Mayanga na kupokelewa na mashabiki na wapenzi wa soka wa mji huo.
Majirani, ndugu, jamaa na viongozi wa klabu alizowahi kuzitumikia akiwemo Thobias Kifaru Afisa habari wa klabu ya Simba, wamemuelezea Marehemu kwa undani kuwa alikuwa mtu mwema mwenye kuchangamana na watu.
“Alikuwa ni mtu wa mazoezi ambaye aliishi vizuri sana ana wachezaji wenzake, viongozi na mashabiki, alikuwa Kijana mwenye nidhamu kubwa sana ndani na nje ya uwanja”.Alisema Kifaru.
Mobby alifariki Machi 5 mwaka huu katika hospitali ya Benjamin Mkapa huko Dodoma, na kusafirishwa jana Machi 6 kuelekea mjini Shinyanga ambapo Ndipo mazishi yalipofanyika.