Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limemfikisha mahakamani binti aliyejitambulisha kwa jina la Pendo Paul Elikana (19) akidaiwa kutoa taarifa za uongo na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii.
Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe imeeleza kwamba binti huyo mkazi wa Kijiji cha Mbuga ya Banya wilayani Meatu mkoani Simiyu, alitoa taarifa za uongo kuwa alipewa kazi ya kumuua kiongozi wa kisiasa.
Aidha, katika taarifa ambayo binti huyo aliisambaza kwenye mitandao ya kijamii, alieleza kwamba alikuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) jambo ambalo pia, si kweli.
Kamanda Swebe alisema baada ya binti huyo kutoa taarifa hizo, walianza upelelezi na ilibainika taarifa zote alizotoa na kuzisambaza hazikuwa na ukweli.
“Uchunguzi umebaini kuwa binti huyo hakuwa askari wa JWTZ kama ambavyo alijitambulisha bali alipata mafunzo ya mgambo, hata hivyo alitoa taarifa ambazo hazikuwa na ukweli wowote kuhusiana na tukio hilo,” alisema.
Kamanda Swebe alisema katika uchunguzi, imebainika binti huyo alifanya hivyo kwa masilahi yake na kutaka kupotosha umma.
Katika maelekezo yake, binti huyo alidai kuwa alipigiwa simu na mtu mmoja (jina linahifadhiwa) akimtaka kwenda kutekeleza shambulizi kwa mbunge wa jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina.
Alidai kwamba katika kutekeleza kazi hiyo, aliahidiwa na mtu huyo kwa kupigiwa simu kwamba atapewa kiasi kikubwa cha fedha ikiwa atafanikisha kutekeleza shambulizi hilo.
“Huyo mtu aliniahidi kuwa atanilipa pesa nyingi, ikiwa nitafanikiwa kutekekeza shambulizi hilo, lakini nilikataa nikamwambia kuwa mimi siwezi kufanya hivyo na hizo pesa zako wapelekee masikini,” alisema katika sehemu ya video hiyo.
