Aliteswa na uvumbuzi wake

Umewahi kumsikia mtu aliyejirudi, akabadilika kutoka mtu mbaya katika jamii na kufariki dunia akiacha sifa nzuri lukuki nyuma yake? 

Mmoja wa watu hao ni Mtume Paulo, ambaye kabla ya kuongoka na kuwa ‘Mtu wa Mungu’, aliongoza kati ya askari ambao walikuwa na kazi ya kuwakamata, kuwatesa na kuwaua watu waliokuwa wakieneza dini ya Ukristo.

Hiyo ilikuwa ni zamani sana. Katika miaka ya hivi karibuni, mtu anayeitwa Alfred Nobel naye anaweza kuwekwa katika orodha hiyo.

Huyu ndiye mwanzilishi wa ‘Tuzo ya Amani ya Nobel’, ambayo ni moja ya tuzo maarufu duniani. Alfred alianzisha tuzo hii kutokana na makosa yaliyofanywa na moja ya mgazeti huko Ufaransa.

Alfred alikuwa mvumbuzi, mwanasayansi ambaye moja ya vitu aivyovumbua ni baruti, ambayo ilitumika kutengeneza mabomu na kuwa chanzo kikubwa cha watu kuuawa katika vita na milipuko mingine.

Kutokana na hilo, watu wengi walimchukia wakiamini kuwa bila yeye kugundua baruti, maisha ya watu wengi yasingepotea.

Alfred alikuwa mwanasayansi raia wa Sweden, ambaye alivumbua vitu vingi na kuviwekea hati miliki na kati ya hivyo baruti ilikuwa ni uvumbuzi wake mkubwa. Kwa ujumla alikuwa na hati miliki ya vitu 355 alivyovumbua.

Maisha ya Alfred yalibadilika baada ya gazeti moja nchini Ufaransa kufanya makosa ya kuandika tanzia yake wakiamini kuwa alikuwa amefariki dunia, lakini kumbe aliyekuwa amefariki dunia alikuwa kaka yake.

Mwaka 1888, kaka wa Alfred aitwaye Ludvig alifariki dunia wakati akiwa ziarani Cannes, Ufaransa. Kwa bahati mbaya, gazeti moja nchini Ufaransa likadhani kuwa aliyefariki dunia ni Alfred, hivyo wakachapisha tanzia ya Alfred. Tanzia hiyo ilimlaani Alfred kutokana na uvumbuzi wake wa baruti ambayo ndiyo ilikuwa malighafi ya kutengeneza mabomu na milipuko. Akaonekana mtu ambaye uvumbuzi wake ulichochea vita katika maeneo mengi duniani na kusababisha vifo vya watu wengi.

Aliposoma tanzia hiyo, Alfred alihuzunika sana baada ya kubaini kuwa dunia ilimchukulia kama mtu mbaya. Hadi wakati huo yeye mwenyewe alikuwa anajivunia uvumbuzi wake wa baruti, akiamini kuwa ni jambo kubwa la kujivunia.

Baada ya kubaini hivyo, akaamua kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yake na akaanza harakati za kuhimiza amani duniani. Tuzo ya Amani ya Nobel ni moja ya mazao ya harakati zake za kuhakikisha anasafisha jina lake na kuiacha dunia ikiwa sehemu salama.

Maisha yake

Alfred Nobel alizaliwa Oktoba 21, 1833 Stockholm, Sweden na kufariki dunia Desemba 10, 1896 akiwa na umri wa miaka 63. Alifariki Sanremo nchini Italia na kuzikwa Stockholm.

Alikuwa mtoto wa tatu wa Immanuel Nobel (1801–1872), mvumbuzi na mhandisi na Karolina Andriette Nobel (1805–1889).