Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mei 15, 2023 Rais Samia alifanya uhamisho wa wakuu wa mikoa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala na kumteua Albert Chalamila kuchukua nafasi yake akitokea Mkoa wa Kagera…

Baada ya taarifa hiyo kutolewa mjadala mkubwa au uteuzi uliozua gumzo ukawa ni Chalamila kuletwa Dar, watu wakakumbushia vituko,mbwembwe na machachari yake yaliyomfanya kuwa mkuu wa mkoa staa kuliko wenzake, na mimi bila hiyana nikaona si mbaya nikuandalie makala inayoelezea safari yake.

Kabla ya kuingia kwenye utumishi wa umma, Chalamila amewahi kuwa mwalimu kwenye shule mbalimbali na baadae akapata nafasi ya kuwa Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa.

Safari yake ya siasa ilianza muda mrefu lakini alipata umaarufu mkubwa Desemba 05, 2017 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa baada ya kushinda katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho akichuana na vigogo kadhaa wa CCM wa mkoa huo..

Chalamila aliteuliwa kwa mara ya kwanza Julai 29, 2018 na Hayati Dkt .John Magufuli kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya akichukua nafasi ya Amos Makala ambaye alihamishiwa mkoa wa Katavi kwa wakati huo.

Chalamila alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka huo mpaka Mei 15, 2021 ambapo Rais Samia alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alipodumu kwa siku 28 tu, na kisha kutumbuliwa Juni 11, 2022

Kilichomponza Chalamila akatumbuliwa Mwanza ndani ya muda mfupi tu ni kauli yake aliyoitoa akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Samia aliyekuwa akitarajia kufanya ziara mkoani humo wakiwa na mabango yaliyoandikwa maneno yoyote.

“Nachukua nafasi hii kuwakaribisha wananchi wote tarehe 13, 14 na 15 tuweze kumpokea rais kwa mabango mengi, ya aina yoyote ile hata kama mtu ataandika tusi aandike tu” alisema chalamila

Kauli yake hiyo ilipishana vikali na maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Aprili 06, 2021 akiwa kwenye hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu aliowateua ambapo alisema endapo viongozi wa kitaifa watakutana na mabango wakiwa katika ziara zao basi atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na mkuu wilaya kwani watakuwa wameshindwa kazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Chalamila alikaa nje ya utumishi wa umma kwa takribani mwaka mmoja kabla ya kutikisa tena vyombo vya habari Julai 28, 2022 akiteuliwa kuwa RC mpya wa Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya Meja Jenerali Charles Ibuge..

Mbali na utumishi wa Umma, RC Chalamila ni mwanamuziki wa nyimbo za asili na amekuwa akiimbia sana mkoani kwake Iringa na kusifia tamaduni zake.