Ijumaa ya Februari 16, mwaka 2017 imekuwa siku ya majonzi kwa taifa letu. Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwiilina B. Akwilini ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye daladala, wakati polisi wanapambana na waandamanaji wa Chadema.
Wiki iliyopita nimeandika makala nikitahadharisha juu ya mwenendo wa askari polisi kutumia nguvu kubwa katika masuala ya uchaguzi. Naamini nguvu wanayotumia ingetumika kuhamamisha kilimo, basi nchi yetu ingeuza na kusaza mazao ya chakula na biashara.
Sitanii, nimepata mrejesho mkubwa wa ujumbe mfupi wa maandishi SMS na simu hadi nikashangaa. Inaonyesha watu wamebanwa vifua, wanatafuta pa kupumulia. SMS zimekuwa nyingi, ila nadhani ni vyema msomaji nikushirikishe hizi chache nilizozichagua:-
- Kaka Balile mimi ni msomaji wa JAMUHURI kemeeni uvunjaji wa Katiba, demokrasia na utekaji na mauwaji ya hovyo yanayofanyika! Msomaji weni Arusha!
- Makala yako kuhusu uchaguzi kwenye gazeti la JAMHURI ina onyo la busara sana, lakini watawala wamelewa madaraka ni kama sikio la kufa. Watu ni lazima wawe huru kitendo chochote kinachowaendesha kama mifugo hakitavumiliwa. Hongera sana.
- Nimekuelewa vizuri sana leo katika makala yako SITANII “UCHAGUZI TANZANIA TUTAVUNA TUNACHOPANDA”. Asante na ubarikiwe sana.
- Deo mwaimukayoge? Nimekusoma “Sitanii” na pia Tahariri. Kwa sitanii tunacheza na moto kuungua hatuna budi. Kama si kesho ni kesho kutwa, lakini kuungua ni dhahiri kwaja.
Nirudi kwenye Tahariri… nikuulize kidogo; hivi mwanamke akiitwa “Jamvi la Wageni” inamaanisha nini? Basi usilishangae Jamvi la Habari. Hilo ni “Dodoki”. Kilichoandikwa na Jamhuri kuhusu e-passport hakikanushiki. Sijui magazeti haya [yenu] kama hayakununuliwa yote mitaani ili wengi wasiyasome.
- Lakini nina hakika Rais kasoma na anatafakari awafanyeje wateule wake “wanaompiga” hela bila woga wala aibu
- Hongera kwa makala nzuri, tulio wengi tunajiuliza Tanzania ni watu fulani tu? Basi wasio stahili mamlaka ziwaonyeshe wanapo stahili kuishi. Nakutakia uzalendo mwema hii ndiyo kazi si kusifia tu ubarikiwe sana.
- Hongera mzee kwa makala yako ya uchaguzi Tanzania Tutavuna Tunachopanda ndani ya gazeti la JAMHURI kwa ujasiri wako kusema hakika meli yetu inaenda kugonga mwamba. Vitisho, ukandamizaji, utumiaji jeshi, wananchi wana hofu itajenga chuki hatimaye meli itagonga mwamba.
- Nchi kama Marekani kwa sababu vyombo vya usalama vimeapa kulinda nchi haviwezi kushiriki kuhujumu chama chochote, moja ya majukumu yao ni kuhakikisha vyama vyao viwili vyenye nguvu vinabaki kuwa na nguvu ili watu wakichoshwa na mtawala wa chama fulani baada ya miaka minne wanampiga chini! Serikali za kidomokrasia zinawaogopa wananchi maana ndiyo waajili wao.
- Umeisoma Bibilia na Kuran Tukufu vizuri? Au ni kikundi/wewe mmeshaandaa tenki la hiyo petrol kuilipua hii nchi? Mna lenu jambo. Watanzania hatutakubali. Mbona hukuwahi kutoa maoni yoyote ya Kibiti/Staki Shari na Mkuranga? Haya juzi Kinondon ndio umeona: uzuri wake Watanzania wanakufahamu.
- Tulipenda sana gazet/Jamhuri, yanayoandikwa ndani ya gazeti hilo kila kinachoandikwa mtiririko ni mzuri, ukikribia mwisho wa habari msomaj anakutana na vitisho. Bw. Balile mbona hata hoja zako katika vipind ITV uko vizuri, sasa mh!
Ujumbe huo kutoka kwa watu 10 ni sehemu ya mrejesho kutokana na makala niliyoandika wiki iliyopita ikionya kuwa matendo ya mauaji, kupiga watu, kuzuia watu kutoa mawazo yao tunaimwagia nchi petrol.
Sitanii, nasisitiza kuwa Akwilina amefariki kwa kupigwa risasi. Tunao Watanzania wengi wanaopoteza maisha katika mazingira tata. Hali hii si ya kufurahia. Tusifurahie kuona watu wanapigwa risasi. Polisi bunduki hizi ni msalaba mkubwa kwenu.
Akwilina awe Balozi wa amani. Kama tulikuwa tunafanya majaribio, matokeo sasa tumeyaona. Tufunge breki. Hata tukisukumana hadi kufikia hatua hii ya mauaji mwisho wa siku turarejea katika meza ya mazungumzo kujadiliana mustakabali wa taifa letu. Naamini wakati ni huu. Tanzania tuzungumze kulinda amani yetu. Ni kwa amani yetu kuendelea kuwapo, tutakuza uchumi wa taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.