Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limethibitisha kumkamata mwanamke mmoja aitwaye Khadija Juma (24) Mkazi wa kijiji cha Sengerema Wilaya ya Uyui Mkoa wa Tabora, akiwa na mtoto mchanga wa kike aliyemuiba kwenye kituo cha afya Ushetu mnamo Agosti 20, 2024.

Mtoto huyo ambaye baada ya kuzaliwa Agosti 17, 2024 aliendelea kubaki hospitalini kwa ajili ya uangalizi maalum, aliibiwa baada ya mama yake mzazi kutoka nje kufanya mazoezi na kumuacha wodini akiwa amelala ndipo mtuhumiwa alipoingia na kutekeleza tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema taarifa za tukio hilo ziliripotiwa kituo cha Polisi Nyamilangano Agosti 21,2024 na ufuatiliaji wa haraka ulifanyika, na Agosti 22,2024 saa tatu usiku Polisi walifanikiwa kumkamata Mtuhumiwa na kumuhoji, ambapo amekiri kutenda kosa hilo, hivyo taratibu za kumfikisha mahakamani zinakamilishwa

“Mtuhumiwa huyo baada ya kumhoji amekiri kuwa aliiba mtoto baada ya kuolewa mara mbili bila ya kufanikiwa kupata mtoto ambapo aliolewa Ushetu miaka miwili hakupata mtoto akaolewa Wilaya ya Uyui hakupata Mtoto hivyo aliamua kuiba Mtoto” amesema.

Kamanda Janeth ametoa wito kwa wanawake wanaopata changamoto ya uzazi wakutane na wataalamu wa afya ili wasaidiwe zaidi na waweze kupata watoto kuliko kukimbilia kuiba.

Please follow and like us:
Pin Share