Shehena ya nafaka zinazohifadhiwa kwenye maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imepungua sana miaka ya hivi karibuni na kwa karibu miaka minne mfululizo imekuwa chini ya tani 100,000, JAMHURI limebaini.

Takwimu za hivi karibuni za taasisi hiyo zinaonyesha kuwa hadi mwezi Novemba mwaka jana NFRA ilikuwa na akiba ya chakula kiasi cha tani 52,726.9 ambazo ni kiasi kidogo sana katika kipindi cha miaka mitano.

Kiasi hicho ni sawa na asilimia 21 tu ya uwezo wa maghala yote 34 yanayomilikiwa na NFRA ambayo kwa hivi sasa ni tani 251,000.

Kwa mujibu wa wataalamu wake, kiasi hicho hakiwezi kukidhi mahitaji ya dharura ya chakula ya taifa kwa miezi mitatu mfululizo. Mwezi uliopita wataalamu wa NFRA waliwaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa ili nchi iwe salama, NFRA inahitaji kuwa na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi akiba isiyopungua tani 700,000 za nafaka.

Wataalamu hao walitoa ufafanuzi huo tarehe 14, Januari mwaka huu wakati kamati hiyo ilipokwenda kukagua mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka unaojengwa na NFRA jijini Dodoma yalipo makao makuu yake.

“Kamati hiyo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Khalfan Hilaly, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, imeridhishwa na mpango huo wa serikali katika kukabiliana na uwezo mdogo wa kuhifadhi nafaka,” NFRA ilisema kwenye taarifa kuhusu ziara hiyo.

“Kadhalika akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge alisifu mradi na kusema ni moja kati ya miradi yenye tija kwa maendeleo ya nchi, kwani mara baada ya mradi huo kukamilika uwezo wa kuhifadhi wa Wakala wa Taifa utakuwa mara mbili ya uwezo wa sasa, yaani kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000 huku ikitarajiwa kufikia tani 700,000 kufikia mwaka 2025,” taarifa hiyo inaendelea kusema.

Kwa mujibu wa NFRA, mikataba ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula ilisainiwa na kuanza kazi Disemba 9, mwaka 2017 kati ya NFRA na kampuni mbili kutoka Poland, Feerum SA na Unia Spzo.O.

Gharama ya kutekeleza mradi huo ni dola milioni 55 za Marekani ambazo kwa viwango vya soko vya sasa hivi ni sawa na Sh bilioni 127.

Wakala hutekeleza majukumu yake nchi nzima kupitia kanda zake saba zilizoanzishwa kimkakati ambazo ni Arusha, Kipawa (Dar es Salaam), Dodoma, Shinyanga, Makambako, Sumbawanga na Songea.

Mikoa inayohudumiwa na kanda hizi ni kama ifuatavyo: Arusha – Arusha, Kilimanjaro na Manyara; Kipawa – Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro, Mtwara na Lindi; Dodoma – Dodoma na Singida; Sinyanga – Shinyanga, Tabora, Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu na Kigoma; Makambako – Iringa, Mbeya, Njombe na Songwe; Songea – Ruvuma; na Sumbawanga – Rukwa na Katavi.

Kwa hivi sasa, mazao yanayonunuliwa na NFRA ni mahindi, mtama na mpunga. Mazao haya hununuliwa kupitia Kanda za Wakala katika maeneo yaliyobainika kuwa na uzalishaji wa ziada wa chakula, hususan vijijini.

Nafaka zilizokuwa zimehifadhiwa mwezi Novemba mwaka jana pia zilikuwa kiasi cha chini sana tangu Januari 2019 wakati shehena nzima ya chakula kwenye maghala ya NFRA ilikuwa tani 85,524.5.

Kiwango cha juu kwa mwezi Novemba katika kipindi cha miaka mitano kilikuwa tani 238,133.6 mwaka 2015 kabla ya kushuka hadi tani 90,900 mwaka uliofuata na baadaye kupanda mpaka tani 93,353.7 Novemba 2017 na tani 92,402 mwaka 2018.