*Ni Naomi na Sara ambao walipata majanga siku 11 tu baada ya kuzaliwa

*Aishi nao chumba chenye giza, bila huduma ya maji, wala lishe bora

*Asema hajawahi kuwa na Bima ya Afya, sembuse watoto hao!

BUKOBA

Na Phinias Bashaya

Naomi na Sara ni watoto mapacha ambao matatizo katika malezi na makuzi yao yameanza siku 11 tu baada ya kuzaliwa; walipompoteza baba yao mzazi.

Majukumu yote ya malezi yakabaki upande wa mama yao, Violeth Joseph, ambaye naye amefariki dunia miezi miwili iliyopita akiwa safarini kusalimia ndugu zake huko Karagwe.

Alikuwa mwanamke mjasiriamali aliyeonekana mara kwa mara mitaa ya mjini Bukoba akitembeza mboga kutafuta riziki ili kutunza familia.

Kwa kuwa mume wake ambaye wangegawana majukumu ya malezi alifariki dunia siku chache baada ya kujifungua, alilazimika kufanya kazi maradufu kukidhi mahitaji ya mapacha wake.

Baada ya taratibu za mazishi ya mama yao, Naomi na Sara wamekabidhiwa kwa bibi yao mzaa baba, Catherine Kazoba, mwenye umri wa miaka 76; awatunze na kuwalea.

Bibi huyo anasema kabla ya kuondoka msibani, aliuliza suala la malezi ya watoto hao, akaambiwa aondoke nao!

Baada ya kurejea Bukoba akitokea Karagwe, watoto wakiambatana na bibi yao, sasa wameanza ukurasa mpya wa malezi bila kusikia sauti ya mama.

Kwa umri na uzee wake, akitembea kwa mkongojo, huu kwake ni mtihani mkubwa unaoamsha kwikwi na majeraha aliyopitia kwa miaka 76.

Ni mtihani unaomrudisha akikumbuka vifo vya watoto wake tisa waliofariki dunia katika vipindi tofauti na kubakia na wawili tu.

Watoto wote wa kiume walifariki dunia na kuacha wajukuu ambao alitakiwa kutoa mchango wa malezi yao kwani watoto wake wawili waliosalia, pamoja na umri wao mkubwa, hawana uwezo wa kumsaidia.

Anaangua kilio na kusitisha mahojiano anapokumbuka kifo cha mmoja wa mabinti wake aliyefariki dunia mwaka 2015 akiwa mjini Bukoba kutokana na matatizo ya uzazi.

“Siwezi kutembea bila msaada wa fimbo. Miguu inauma na kutetemeka. Sina mradi wowote wa kuingiza kipato, nategemea misaada kuwatunza wajukuu wangu,” anasema bibi Catherine.

Anasema baba wa watoto hao hakuacha mali ambazo pengine zingetumika kusaidia malezi hali iliyosababisha hata mama yao kuomba misaada, na sasa majukumu yote anayabeba mwenyewe.

Catherine yupo kwenye kundi la wazee ambao uwezo wao wa kumudu maisha ni mdogo; kwa upande wa pili akiwa na jukumu la kuhakikisha usalama na malezi ya Naomi na Sara.

Ni mzee ambaye yeye na wajukuu wake kwa sasa hawawezi kunufaika na Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kuwa haitekelezeki baada ya kutotungiwa sheria.

Sera hiyo pamoja na mambo mengine inasema wajibu wa Serikali za Mitaa ni kufanya utambuzi wa mahitaji ya kundi hilo katika jamii, kutoa ulinzi na matunzo.

Bibi Catherine anasema pamoja na changamoto anazopata kuanzia kumudu maisha yake na wajukuu, bado hakuwahi kupata fursa ya kujumuishwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa kupitia TASAF.

Chumba kimoja na sebule anamoishi vinachora ramani ya changamoto za maisha yake na kuonyesha ugumu wa safari ya Naomi na Sara tangu vifo vya wazazi wao.

Wenyewe, Naomi na Sara, wamemzoea bibi yao wakiwa na furaha ya kitoto ingawa nyuso zinaonyesha maswali mengi kichwani kwa kutomuona tena mama yao.

Hawasikii sauti yake na hawaoni zawadi zilizokuwa zikiletwa na mama aliporejea nyumbani kutoka kwenye shughuli zake za ujasiriamali.

Shughuli za upishi zinafanyika kwenye jiko la mkaa sebuleni kwani hakuna jiko lililojengwa nje kwa ajili ya kazi hiyo, jambo linaloweza kuiingiza familia hiyo katika janga la moto!

Hili linakwepeka kama watu wengine wataamua kutoa msaada.

Kutokana na umri wa bibi Catherine na kutembea kwa mkongojo, bila shaka ni kazi ngumu kwake kulihamishia nje jiko hilo na kulirejesha ndani kila siku!

Chakula cha usiku kwa ajili yake na wajukuu lazima kiandaliwe mapema kwani nyumbani hapo hakuna taa, ila kibatari tu.

Eneo analoishi halina maji ya bomba na wao hupata huduma kutoka kwa wasamaria wema wanaomletea kutoka mtoni; wengine humpa ndoo ya maji.

Naomi na Sara waliozaliwa Januari 11, 2019, wanahitaji sana maji; tena mengi, kwa ajili ya usafi, matunzo na matumizi mengine. Hili halikwepeki.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Anna Ndile, anaifahamu familia hiyo duni na ameliambia JAMHURI kuwa aliitembelea iliporejea kutoka Karagwe, msibani.

Anna anakiri kuwa mazingira wanayoishi si rafiki kwa watoto na hata kwa mlezi wao.

“Hata jana asubuhi (wiki iliyopita) nimepita pale nikamkuta bibi anawaogesha wajuu zake, nikamuuliza kama kazi hiyo anaiweza? Akasema; ‘nitafanyaje? Maana baada ya mazishi hakuna aliyejitolea kuwalea!’ Inasikitisha sana kwa kweli,” anasema Anna.

Kadiri umri wa Sara na Naomi utakavyosogea, mahitaji yataongezeka na kuwa makubwa ikiwa ni pamoja na elimu na uangalizi wa karibu zaidi.

“Hapa tunapoishi hakuna maji na nyumba haina umeme, sina msaada mwingine ni mimi mwenyewe ninaendesha maisha kwa kuomba. Siwezi kupikia nje, hakuna jiko,” anasema bibi Catherine.

Anasema changamoto ya malezi ya wajukuu wake inakuwa kubwa zaidi kwa kuwa hana msaidizi nyumbani hapo; huku akitakiwa kutafuta chakula na mahitaji mengine.

Miongoni mwa gharama za matunzo ya watoto hao ni lishe na mavazi ya kitoto; mambo mazito kabisa kwa mzee huyu.

Pamoja na kuhitaji wasamaria wa kumsaidia kupata nishati ya umeme na maji nyumbani, pia anahitaji mfanyakazi wa kulea watoto. Vyote hivi ni fedha.

Anapaza sauti kwa umma kumpatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili hasa Naomi na Sara. 

 Watoto hawa wapo kundi la wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wako kwenye hatari ya kunyemelewa na magonjwa mbalimbali; na hawana Bima ya Afya kwa ulinzi wa afya yao.

“Hata mimi ninatamani kuwa na Bima ya Afya. Hiki kitu sijawahi kukipata maishani mwangu. Sina kipato. Siwezi kuwakatia bima wajukuu wangu,” anasema kwa uchungu.

Akizungumzia mazingira hayo, Mhadhiri Msaidizi Kitengo cha Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shagembe, anasema suala la Naomi na Sara lina madhara makubwa katika makuzi yao hasa kama hawatapata msaada mapema wangali wadogo.

“Ni watoto ambao hawakuchagua kuishi katika hali hiyo. Ni wazi hawawezi kusema, lakini tayari wanaathiriwa kwa kuwakosa wazazi ambao hawakubahatika kuonja hata upendo wao, hasa wa baba,” anasema Shagembe.

Mhadhiri huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasaikolojia nchini, anasema Naomi na Sara wanakulia kwenye mazingira tofauti na watoto wengine wenye umri sawa na wao; mazingira ambayo si rafiki.

Anasema akili za watoto hunasa mambo haraka na tayari zimeanza kupokea mambo haya mazito yanayoweza kuathiri ukuaji wao.

“Kwa hisia kuna hali ngumu wanaipitia kwa kutokumuona mama yao. Kimwili, unaweza kuwaona wako sawa, lakini wanatakiwa kusaidiwa kwa ajili ya ustawi wao na wa taifa,” anasema Shagembe.

Suala la malezi ya Naomi na Sara linaendelea kubaki mikononi mwa bibi huyu maskini! Hakika jamii inapaswa kuwafuta machozi watoto hawa na kuwajengea msingi bora wa maisha yao ya usoni.

0767489094


Catherine Kazoba (76) akiwa na wajukuu wake mapacha anaowalea, Naomi na Sara, Kilimahewa mjini Bukoba.