Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Songwe
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia Tumshukuru Kibona (30), Mkazi wa Mji mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa lengo likiwa ni kutaka kujipatia fedha.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo inaeleza kuwa baada ya mtuhumiwa kutoweka nyumbani kwao kwa siku tatu alitumia simu yake ya mkononi kuanza kuwatumia wanafamilia ujumbe mfupi kuwa ametekwa na kilihitajika kiasi cha shilingi milioni mbili ili watekaji hao wamuachie.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Alex Mkama amesema Novemba 15, mwaka huu, jeshi hilo lilipokea taarifa ya kutekwa kwa mtuhumiwa huyo.
Amesema mtuhumiwa aliondoka nyumbani kwao tangu Novemba 12,2022 na hakurejea, lakini siku iliyofuata alianza kutumia ndugu zake ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani akihitaji kutumiwa kiasi hicho cha fedha.
“Mara baada ya taarifa hizo kufikishwa kituo cha Polisi sisi tulianza ufuatiliaji wa kina na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa katika sehemu za starehe tofauti na taarifa alizotoa awali kuwa alikuwa ametekwa” amefafanua Kamanda Mkama.
Amesema kwa sasa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi juu ya mtuhumiwa kutoa taarifa za uongo.