NA MICHAEL SARUNGI

Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umeingia katika tuhuma za kutoa ajira kwa baadhi ya wafanyakazi wake bila kufuata kanuni na taratibu za ajira.

Tuhuma hizo zimetolewa wakati Shirikisho likiwa katika mgogoro na aliyekuwa Makamu wa Rais, Michael Wambura na kujikuta akifungiwa maisha kujihusisha na soka.

Licha ya uwepo wa watumishi walioajiriwa bila ya kufuata taratibu za kisheria ndani ya TFF lakini pia ndani ya kipindi kifupi shirikisho linadaiwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha bila maelezo ya kuridhisha.

Akizungumza na JAMHURI kuhusu tuhuma hizo, Michael Wambura amesema TFF inakabiliwa na wakati mgumu kuliko wakati mwingine wowote.

Amesema tangu aingie madarakani Rais wa TFF,Wallace Karia, utoaji wa ajira ndani ya TFF umekuwa jambo la siri linalotolewa bila ya kufuata sharia za ajira ndani ya shirikisho.

Amesema kwa mujibu wa sheria za kazi, nafasi ya ajira inapotokea ndani ya taasisi ni lazima itangazwe kama taratibu zinavyotaka tofauti na hali ilivyo ndani ya TFF ya sasa.

Amesema kwa mfano walipoingia madarakani walikuta Kaimu Katibu Mkuu ni Salum Madadi kwa sababu alikuwa ni mwajiriwa wa TFF, jambo ambalo kisheria ilikuwa halali.

Wambura amesema kuna wafanyakazi ndani ya TFF ambao mikataba yao ilikuwa haijaisha lakini cha kushangaza wameajiriwa watu wengine kuchukua nafasi zao na kulazimu TFF kuvunja mikataba hiyo na kuingia hasara ya kuwalipa fidia.

Ameutaja uvunjifu wa kanuni mwingine ndani ya TFF ni kitendo cha Wilfred Kidau kupewa nafasi aliyonayo ambayo ni makosa kisheria, kwa sababu sheria za TFF zinakataza mjumbe wa Mkutano Mkuu kuajiriwa ndani ya Shirikisho.

Amesema Kidau ni mwenyekiti wa TAFCA, hawezi kuajiriwa na wakati huo huo kuwa mjumbe wa mkutano mkuu na kuongeza kuwa hiyo haikubaliki kwa mujibu wa sheria za TFF.

Amesema waajiriwa wapya ndani ya Shirikisho wamekuwa wakipatikana kwa kutegemea unaelewana na nani ndani ya shirikisho hilo huku sheria na taratibu zikiwekwa pembeni.

Akizungumzia na gazeti la JAMHURI, mmoja wa waliotajwa kuoata ajira kwa upendeleo, ambaye pia ni msemaji wa sasa wa TFF, Clifford Ndimbo, amesema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa sababu liko juu ya uwezo wake.

Wakati huo huo Kaimu Katibu Mkuu, Kidao alipohojiwa kuhusu tuhuma dhidi yake za kukaimishwa nafasi bila ya kufuata utaratibu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Rais wa TFF anena

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Rais wa Shirikisho TFF, Karia hakutaka kuzungumzia tuhuma za ajira na matumizi mabaya ya fedha lakini akasema katika kipindi chake cha uongozi shirikisho hilo limejitahidi kubana matumizi.

Amesema Kamati ya Utendaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Mkuu ameweza kupunguza wafanyakazi kutoka 44 hadi 21 hiyo yote ikiwa ni jitihada za kupambana matumizi yasiyo ya lazima.

Amesema siku za karibuni FIFA walituma timu ya uchunguzi (Investigation team) kuangalia yale yote yaliyofanyika kuanzia mwaka 2013 hadi 2017. Timu hiyo ilikaa nchini kwa muda wa wiki mbili.

Amesema timu hiyo ilifanya kazi karibu na Ofisi ya Katibu Mkuu, na yale yaliyogundulika yameacha doa kubwa, pia walitoa ripoti na maelekezo ya mambo ya kuyafanyia kazi na kuchukua hatua.

“Masharti yote haya yaliambatana na kuzuiwa kwa fedha zetu za miradi, lakini tumekosa pesa zinazoitwa Operation Cost ikiwa ni shinikizo la dola milioni 3 ambazo tulipaswa kulipwa kutoka mwaka 2015-2018,” amesema.

Amesema katika vita hii ya kupambana na udhalimu kwenye mchezo wa soka wa nchi hii, hawezi kurudi nyuma na kwamba atapambana na udhalimu wowote ndani ya shirikisho hilo.

Takukuru

Msemaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Musa Misalaba alipoulizwa kuhusu madai hayo alishindwa kukataa au kukubali kuyafahamu.

Misalaba amesema jambo hilo yawezekana lipo ngazi ya juu zaidi na kuongeza kuwa hata yeye jambo hilo amelisikia kupitia vyombo vya habari alipokuwa safarini na kuahidi kulifanyia kazi.

Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa amesema ni jukumu la mlalamikaji yeyote, taasisi au mtu binafsi kutoa taarifa kwa mamlaka husika kama kuna jambo linaloonekana kuwa kinyume.

Amesema mgogoro uliopo ndani ya TFF haujawafikia ofisini na kwamba Jeshi halifanyi kazi bila ya mamlaka husika kwenda kutoa taarifa juu ya tukio linalolalamikiwa.