Tangu nchi yetu iliporuhusu tena mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, imeendelea kushuhudia mengi – mazuri na mabaya. Ninamuomba Mungu aendelee kutuepusha na hayo mabaya.

Binafsi ninafurahia ukuaji wa demokrasia hapa Tanzania, ambayo inanipa hata mimi haki yangu ya kimsingi ya kuwa na uhuru wa kutoa mawazo yangu na kutenda jambo bila ya kuvunja sheria na taratibu za nchi.

 

Uhuru wa mawazo na matendo vina mipaka yake. Siwezi kukurupuka asubuhi na kuamua kuingia mitaani na kuanza kupanga mawe barabarani kuzuia magari. Kwa kitendo hicho nitakuwa nimevunja sheria.

 

Ninamaanisha kuwa moja ya fursa tunazozipata katika demokrasia ni kuimarishwa kwa haki za msingi za binadamu zenye kulindwa na sheria zilizopo. Haki tulizonazo huenda sambamba na wajibu wetu kama raia wa kuheshimu na kutii sheria hizo.

 

Uwepo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini umenipa fursa ya kujifunza mengi. Nimepata fursa ya kuona watu wakiwa huru kujiunga na kuondoka chama fulani. Nimeshuhudia kuona viongozi wakuu wa vyama ama wakichaguliwa, au kuenguliwa lakini yote ni katika kuimarisha demokrasia nchini.

 

Nimeshuhudia sera lukuki zenye mwelekeo na zisizo na mwelekeo katika mustakabali wa Taifa letu. Nimeshuhudia Mahakama zetu ama zikifungua, au zikifuta kesi mbalimbali zinazohusu chaguzi ndogo na kubwa za vyama vya siasa. Nimeshuhudia maandamano na mikutano mbalimbali ya vyama vya siasa.

 

Nimeshuhudia vurugu zinazohusisha wafuasi wa chama kimoja na kingine. Vurugu zinazohusisha wanachama na polisi. Orodha ya ushuhuda ni ndefu, lakini yote haya nimeshuhudia yakitokea katika Tanzania inayojaribu kuimarisha demokrasia ya kweli kwa manufaa ya kizazi cha leo na vijavyo.

 

Katika makala yangu ya leo nataka nitoe ushuhuda wa kile nilichokisia kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, wakati akitoa tamko rasmi la chama chake baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu, kilichofanyika Julai 6 na 7 jijini Dar es Salaam.

 

Nawapongeza kwa uhodari na uwajibikaji mzuri wa Kamati Kuu ya Chadema kwa kukaa muda mfupi na kutoka na azimio zito kwa manufaa ya chama na wanachama wao, na pengine Taifa kwa ujumla. Nawapongeza kwani wameokoa fedha nyingi ambazo endapo kikao kingechukua wiki moja kujadili mambo nyeti ya chama chao kitaifa, kingeweza kutumia fedha nyingi za chama ambazo zingehitajika katika uendeshaji wote wa vikao hivyo.

 

Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Mbowe alifafanua masuala mbalimbali ambayo Kamati Kuu iliyajadili na kuyatolea maazimio. Miongoni mwa hayo, Mbowe alisema Chadema imeamua kuanzisha kambi za mafunzo ya ulinzi nchi nzima kwa kuwa chama chao hakina imani na Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa wala Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kwa kifupi hawana imani na ulinzi uliopo nchini kwa misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

 

Mafunzo hayo kwa mujibu wa Mbowe, yatatolewa kwa walinzi wa chama “Red Brigade”. Nanukuu, Mafunzo ya ulinzi yamelenga kukabiliana na walinzi wa CCM “Green Guards”.

 

Mbowe alisema, “Ni wajibu wa chama kutafuta njia za kujilinda, hatulindwi na Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Usalama wa Taifa, watu wetu wanapigwa na wanauawa hata tukienda polisi hatupati haki yetu. Ni bora tuanzishe mafunzo na tujilinde wenyewe kwani tukiendelea kupiga magoti na kulia tutakuwa wajinga.”

 

Hofu yangu hapa ni kwamba endapo Chadema itachukua nchi, hakuna askari atakayebaki na ajira serikalini. Majeshi yote ya nchi yataundwa upya kwa kutumia walinzi wa kutoka “Red Brigade” ambao hadi kufikia 2015 sidhani kama watakuwa tayari wana weledi wa kutosha wa kuendesha shughuli za Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na JWTZ.

 

Ninasema hivyo kwa sababu endapo majeshi yataundwa upya kuanzia chini, basi sitarajii utulivu ndani ya nchi. Hii ni hofu nyingine niliyonayo kwa sababu watakaoondolewa kwa kuhofiwa ni mabaki ya CCM, hawatakubali kuona ukomo wa ajira yao unatokana na kuingia Chadema madarakani. Na wao wataunda vikosi kwa jina watakalochagua.

 

Nchi zote duniani zenye mfumo wa vyama vingi vinavyoheshimu demokrasia ya kweli, wapinzani mara nyingi hawafanyi mzaha na vyombo vya usalama wa taifa hata kidogo. Kwa nini, kwa sababu wanajua endapo watashika dola vyombo hivyo mara moja vitatakiwa kutii na kuheshimu chama na serikali iliyochaguliwa na wananchi hata kama wao hawakuridhika. Wasiporidhika wachache hufanya mapinduzi ya kijeshi.

 

Mgogoro uliopo sasa ni baina ya Chadema na CCM. Sioni sababu ya kuingiza vyombo vya ulinzi na usalama kwenye tuhuma hizi. Kuna mamilioni ya Watanzania ambao si wanachama  wa chama chochote cha siasa. Wanachotambua ni kwamba nchi yao ina majeshi ya ulinzi na usalama, hivyo wana uhakika wa kufanya shughuli za kujenga taifa kwa amani na utulivu. Na jeshi halipaswi kuwa na upendeleo kwa chama chochote cha siasa.

 

Naendelea kujiuliza uamuzi huo wa kuanzisha mafunzo ya namna ya kujilinda dhidi ya chama kingine au vingine utaishia hapo tu, au vijana hao wa Red Brigade watapewa kazi ya kulinda mipaka ya nchi na sehemu nyingine ili CCM isiweze kufanya hujuma yoyote ile dhidi ya Chadema?

 

Kwa sababu katika chaguzi zilizopita tulishuhudia tuhuma mbalimbali za wizi wa karatasi na masanduku ya kupigia kura. Kwa mtazamo wangu, huu ni uamuzi wa haraka mno, ambao ulihitaji kwanza kupata baraka za wanachama wa Chadema kwa kupitia kura za maoni.

 

Je, ni kweli wanachama wote wameliunga mkono hili? Je, ni wapi walipokutana na kulijadili hili suala? Je, huu unaweza kuwa ni uamuzi wa watu wachache ambao labda Chadema ni chao na wengine si chao kutokana na historia ya kuanzishwa kwake?

 

Je, Chadema wameona hakuna fursa za ajira kwa vijana hivyo wameamua kuanza na utoaji wa ajira kwa kupitia kitengo chao cha ulinzi? Je, vijana wangapi wa kizazi hiki ambao wako tayari kuajiriwa ili kuhakikisha wakubwa wao hawapati madhara yoyote ilimradi wao waendelee kuwa mbuzi wa kafara kama alivyosema Mbowe mwenyewe?

 

Je, vijana wa Taifa hili hawana ufumbuzi mwingine wa ukombozi wa maisha yao hadi wategemee kutengewa ajira ya ‘ukamando’ na Chadema, tena kwa kukiuka misingi ya Katiba ya nchi?

 

Katika sura ya tisa ya Katiba Ibara 147 (i) “Ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote.”

 

Ninatambua uwezo wa vyombo binafsi vya ulinzi kama vile Knight Support, na vingine vingi tu ambavyo vimesajiliwa na vinaendesha shughuli za ulinzi hapa nchini. Ninatambua uwepo wa ulinzi wa vijana wa Kimaasai katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Ninatambua uwepo wa ulinzi wa Sungusungu katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

 

Vyombo hivi vipo kwa ajili ya kulisaidia Jeshi la Polisi katika jukumu la kulinda raia na mali zao. Havipo kwa maslahi ya chama chochote cha siasa. Sasa kwanini Chadema wasitumie mojawapo ya vyombo hivi kama hawana imani na vyombo vya dola hadi wafikie hatua ya kuunda vikosi ndani ya chama chao?

 

Kwa mantiki hii, naweza kusema wazi kuwa tamko la Chadema la kutaka kuanzisha kambi nchi nzima si tamko halali kikatiba na linalenga kuupotosha umma wa Watanzania na kutaka kuwaingiza vijana matatani kwa kuwachonganisha na Serikali iliyopo madarakani.

 

Natambua wazi kwamba kila raia wa nchi hii ni mlinzi wa Taifa lake. Uamuzi wa kuanzishwa kwa majeshi ya mgambo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni kumfanya kila raia aweze kuwa na uwezo wa kujihami dhidi ya maadui na kuwafanya Watanzania waweze kufanya kazi za kujenga Taifa kwa mshikamano. Hakuna uamuzi wa kutengeneza walinzi wa CCM na viongozi wake.

 

Tuhuma zinazotolewa na Chadema kwa vijana wa “Green Guards” wa CCM haziwezi kupuuzwa. Kama ni kweli CCM wanatoa mafunzo kwa vijana wao kwa lengo la kujifunza mbinu za kushambulia, basi namuomba John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, atoe ufafanuzi juu ya hili, atueleze masharti ya usajili yanaruhusu vyama vya siasa kujiundia vikosi vya ulinzi mbadala na kudharau vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria?

 

Asipofanya hivyo wakati utamhukumu kwa kuwa yeye ana wajibu wa kufuatilia mienendo ya vyama vyote vya siasa bila kujali kipo madarakani au la.

 

Kamati Kuu ni chombo kikubwa ndani ya chama. uamuzi unaotolewa na chombo hicho ndiyo dira ya chama chenyewe. Kupotea au kuwapo kwa dira hiyo ndiyo kudorora au kuimarika kwa chama husika.

 

Hivyo, rai yangu kwa vyama vyote vya siasa ni kwamba vijaribu kuwa na mitazamo ya kujenga na si kubomoa Taifa. Sitaki kuyapuuza malalamiko ya Chadema ila tahadhari yangu ni wao kujiepusha na misimamo ambayo itasababisha migogoro nchini.

 

Chadema imeshatoa tangazo la ajira kwa vijana. Kilichobaki ni utayari wa vijana hao kuchangamkia fursa hiyo kwa masharti ya chama hicho na si kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ndiyo demokrasia yetu. Mungu ibariki Tanzania

 

Simu: 0763 400283

[email protected]