Yapo malalamiko mengi kutoka kwa Watanzania yanayohusu kazi walizostahili kuzifanya, kuona sasa zikifanywa na wageni.

Tunawalaumu raia kutoka Kenya, China, India, Malawi, Burundi na kwingineko duniani, walioingia nchini mwetu maelfu kwa maelfu kufanya kazi mbalimbali.

Malalamiko haya ya ndugu zangu Watanzania yamenifanya nipitie kijitabu cha Tujisahihishe kilichoandikwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambaraga Nyerere, mwaka 1962.

Aya za mwisho za kitabu hicho, Mwalimu anasema hivi:

Kosa moja kubwa sana ambalo linatokana na unafsi ni kutaja makosa ambayo sisi wenyewe hatunayo, na kuficha makosa ambayo sisi wenyewe tunayo. Hili ni kosa lile lile linalotufanya tulaumu tusiowapenda, na kutolaumu tunaowapenda, bila kujali ukweli. 

Nimetaja makosa haya ili yatusaidie, siyo katika kuwahukumu wenzetu tu ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe, ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi.”

Sijui ni Watanzania wangapi wamekisoma au hawakukisoma kijitabu hiki. Mara zote sichoki kuwasihi wananchi wenzangu kukisoma ili kuvuna maarifa mengi yaliyojaa hekima ya kiuongozi na kizalendo kwa nchi yetu. Rais John Magufuli amejitahidi kuwasisitiza wakuu wa wilaya, mikoa, mawaziri na watumishi wengine kukisoma kijitabu hiki.

Nukuu hiyo ya Mwalimu, kwa muktadha wa makala hii, inalenga kuonesha namna tulivyo wepesi wa kuwasema wengine, lakini tukawa wazito wa kuukiri udhaifu wetu.

Hapa ninapoandika haya, nipo safarini katika ukanda wa kaskazini mwa nchi yetu. Kwa sababu nipo safarini, nalazimika kununua huduma za malazi, chakula na nyingine.

Jambo moja lililo wazi ambalo nimekutana nalo sehemu nyingi, ni huduma mbovu kutoka kwa wahudumu wengi Watanzania.

Watanzania tu maarufu mno wa kulalamika. Tu mashuhuri katika kuamini kuwa wenye kuibadili Tanzania yetu wapo, na wala siyo sisi wenyewe!

Juzi nilishiriki mjadala katika mtandao mmoja. Ukisoma hoja za wachangiaji wengi, utabaini kuwa wanachojua ni kwamba kazi yao ni kusema na si kutenda. Matokeo ya tabia hii ni kuibuka kwa desturi ya karibu kila Mtanzania kulalamika tu.

Nitatoa mifano kadhaa. Kwa hali ninayokumbana nayo katika migahawa, nyumba za kulala wageni, huduma za usafiri na kwingineko, nashawishika kuamini kuwa Wakenya wana haki kabisa kutunyang’anya kazi nyingi ambazo sisi wenyewe tunajiona ndiyo wenye haki ya kuzifanya.

Kwa mfano, mteja unapoingia katika mgahawa wa Tanzania, ni kawaida kabisa kukuta meza ikiwa na mabaki ya vyakula na vyombo vilivyopambwa na nzi. Meza itasafishwa mgeni akishaketi, tena wakati mwingine lazima mhudumu aitwe afanye usafi!

Unapoagiza kinywaji, mathalani soda, mhudumu atakusikiliza. Ataondoka kwenda kukichukua. Atakaa dakika tano hivi, na akirejea kwako anakuwa, ama ameshika kinywaji ambacho hukumwagiza, au anakuletea jibu la “vimeisha”.

Akiheshimu kukuletea soda, ukiuliza “mbona umeleta ya moto?” jibu atakalokupa ni la aina hii: “Sasa mimi nifanyeje wakati umeme haupo”. Unapojaribu kumwelewesha kuwa alipaswa akujibu kabla ya kukuletea, atakujibu: “Wateja wengine wasumbufu, mbona wengine wanakunywa”. 

Haya ni majibu ya wahudumu wetu ambayo ni kawaida kabisa kukutana nayo Dar es Salaam, na siyo Nairobi. Tanzania ukienda katika mgahawa, wewe ndiye mwenye shida, na wala si yule mhudumu mwenye shida ya ajira au mmiliki wa mgahawa anayepambana na umaskini!

Katika nyumba za kulala wageni hali ni hiyo hiyo. Utaambiwa: “Vyumba vyetu vina TV, maji ya moto, na kadhalika”. Ukishalipa na kuingia ndani ya chumba utakumbana na mambo tofauti kabisa – TV isiyofanya kazi na maji baridi. Ukiuliza mbona TV haifanyi kazi, utajibiwa: “Kuna upepo mkali umepita, umeangusha dishi”. Mtanzania hakosi kisingizio. Kwake kila kosa lazima liwe na sababu au jibu! Neno ‘samahani’ limeshaanza kuwa adimu kweli kweli. Ulaghai kila mahali!

Si hivyo tu, bali Watanzania tunashindwa kutumia fursa. Juzi nilikuwa mjini Musoma katika ukumbi mzuri tu ulio jirani na Magereza. Hapo tukaaminishwa tutapata chakula tunachohitaji. Mhudumu akafika na kuchukua orodha ya tunavyohitaji. Baada ya dakika 15 akarejea kwetu na kusema: “Samaki wameisha, kuleni nyama”. Tulipomwuliza kwanini samaki waishe mapema ilhali hapa tulipo na ziwani ni mita 100, jibu likawa jepesi tu: “Umeambiwa samaki hakuna, sasa unataka iweje, kama hamli nyama basi acheni.” – (maneno haya yasome kwa lafudhi ya Mara).

Kwa hali kama hiyo unashindwa kabisa kujua nani aliyewatoa ufahamu Watanzania? Je, Mkenya anaweza kutoa majibu ya kibabe kama haya? Mchina aliyetoka kwao, anayediriki kuuza mahindi ya kuchoma mitaani atakuwa jeuri namna hii?

Ndugu zangu, tunapolalamika wageni kuchukua kazi zetu, ni vema tukajiuliza sisi wenyewe kama kweli tupo tayari kutoa huduma zinazoendana na ushindani wa ulimwengu wa leo.

Lakini tatizo jingine la Watanzania ni udokozi na uvivu. Msomaji huwezi kuyajua haya hadi uwe mwajiri. Kuna Watanzania ambao kwao udokozi ni kipaji! Kampuni inaweza kuwa na nia njema ya kuhakikisha wafanyakazi wake wanakunywa chai. Itafanya hivyo mwanzoni, lakini baada ya muda itasimamisha huduma hiyo. 

Kwanini isimamishe? Inasimamisha kwa sababu baadhi ya wenye vipaji vya udokozi hudokoa sukari na hata wakati mwingine kuiba vijiko na vikombe! Nani atakuwa tayari kuona sukari inayonunuliwa ikiishia kwenye mikoba na kupelekwa nyumbani kwa wafanyakazi? Matokeo yake leo kuna ofisi utasikia wafanyakazi wakilalamika kukosa maziwa licha ya kazi wanazofanya kuwabana wanywe maziwa! Maziwa yanaibwa!

Wafanyakazi katika hoteli nyingi za Tanzania wanapekuliwa wakati wa kuondoka kazini kwa sababu bila kufanya hivyo maana yake mwenye hoteli atakuwa na kazi ya kununua vijiko, vikombe, taulo, sabuni na vifaa vingine vya hotelini. Tabia hii haipo kwa Wahindi au Wachina wengi.

Udhuru nao ni jambo jingine ambalo mwajiri katika dunia ya leo asingependa kulisikia. Mtanzania anaomba kazi akiwa mnyenyekevu kweli kweli. Anaomba kazi mikono ikiwa nyuma. Anaahidi uwajibikaji na utiifu. Akishaajiriwa baada ya siku tatu keshapata msiba. Atataka aruhusiwe aende kuzika.

Mtu kaajiriwa leo, lakini baada ya wiki mbili anaomba ruhusa kwa sababu jirani yake ana kipaimara au wanamcheza mwali! Haya mambo ya uswahili-swahili hayapo katika ulimwengu wa leo. Anapokuja mwekezaji anataka afanye kazi kwa malengo. Watu wawajibike na awalipe kulingana na kazi wanazofanya. Watanzania kila siku ni misiba, harusi, ugonjwa, ngoma, kipaimara na kadhalika. Nani anaweza kumwajiri mtu wa aina hiyo na akamwacha Mkenya ambaye likizo yake anajua ni moja kwa mwaka na wakati mwingine hata hudiriki kukataa kwenda likizo?

Dereva anapopewa lori apeleke mzigo nchi jirani au mikoani, atahakikisha anaiba mafuta. Kando ya barabara kuu zote kuna maeneo maalumu ya biashara ya mafuta yaliyoibwa kutoka kwenye malori. Watu wamejenga nyumba kwa aina hii ya wizi. Wezi hawa ni Watanzania. Wanapofukuzwa kazi kwa sababu ya wizi wao, hulalama na kudai wananyanyaswa. Watajitokeza watetezi wa kusema “acha waibe maana mishahara yao ni midogo”. Mishahara midogo vipi? Walipoomba kuajiriwa hawakujua kiwango cha mishahara?

Ndugu zangu, waajiri wengi Tanzania si kwamba wanapenda kuajiri raia wa kigeni. Nani anakubali kumlipa Mkenya mshahara wa Sh milioni 3 kwa mwezi pamoja na kumlipia vibali vya ukaazi, kwa kazi ambayo kama Mtanzania angeajiriwa, mshahara wake ungekuwa Sh milioni 2? Waajiri wanaamua kuwaajiri wageni kwa mishahara mikubwa sababu nyingi – wanajua hawana udhuru, hawana udokozi wa kipuuzi-puuzi, si walalamishi, wanawahi kazini, wana utii kwa mwajiri wao, na kwa jumla wanajua nini wanachokifanya na namna ya kukifanya.

Bila kubadilika, Watanzania wataendelea kupoteza ajira na malalamiko yao ya kwamba wageni wanapoka ajira zao yatadumu milele. Mungu akinijaalia ukwasi, sidhani kama hoteli au kiwanda changu kitakosa kuwaajiri Wakenya, Wahindi au Wachina ambao wako tayari kufanya kazi kwa kadri ya mahitaji ya ulimwengu wa leo. Watanzania tusipoacha wivu, ulalamishi, uvivu, udokozi, kupenda sherehe na mengine ya aina hiyo, wageni wana kila sababu ya kuchukua kazi zetu hata kama ni za uyaya ambazo tayari Wamalawi wameshaanza kuzikamata kwa kasi.

Tunapolalamika kuwa wageni wanachukua ajira zetu, tujikumbushe maneno haya murua ya Baba wa Taifa aliyosema: “Nimetaja makosa haya ili yatusaidie, siyo katika kuwahukumu wenzetu tu ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe, ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi.”