Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Tunduru

MFANYABIASHARA aliyetambulika kwa jina la Hery Sanga mkazi wa kitongoji cha Kigamboni, kijiji Biasi, kata ya Nakayaya,Wilaya ya Tunduru, amejinyonga hadi kufa chanzo kikidaiwa ni matokeo mabaya ya mechi ya kirafiki kati ya timu ya Yanga na Veipers ya Uganda.

Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mdogo wa marehemu, Victor Sanga amesema, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 8,mwaka huu,baada ya siku ya mchezo huo marehemu huo.

Amesema kuwa siku hiyo marehemu alionekana akiwa na furaha lakini baada ya matokeo aliondoka akiwa amenyong’onyea hali ambayo imewafanya wahisi kuwa ndiyo chanzo cha kifo chake.

Akifafanua taarifa hiyo Sanga amesema kuwa marehemu kaka yake alikuwa ni mfanyabiashara wa kuuza mikeka na alikuwa mpenzi sana wa timu ya Yanga.

“Tukilinganisha na jinsi ilivyokuwa tunaona ni kutokana na matokeo ya mechi ya kirafiki ambapo timu ya Yanga ilifungwa,” amesema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kigamboni Sharif Mohammed Sharif amethibitisha kutokea kwa tukio ambapo amesema kuwa baada ya kupokea taarifa za tukuo hilo alikwenda nyumbani kwa marehemu na kukuta mlango ukiwa umefungwa huku kufuri likiwa imewekwa kwa nje.

Amesema kuwa baada ya kusukuma mlango ulifunguka na alipoingia ndani alishuhudia mwili wa marehemu ukiwa unaning’inia sebuleni huku shingo yake ikiwa imefungwa na kitanzi cha kamba ya katani kutoka juu ya mbao za kenchi.

Amesema baada ya tukio hilo alikwenda Polisi kutoa taarfa na baada ya muda Polisi walifika na kuuchukua mwili huo na kwenda kuhifadhi katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya kwa ajili ya taratibu za kisheria.

Naye Diwani wa Kata ya Nakayaya Daud Amlima amesema tukio hilo limewashtua wengi kwani marehemu alikuwa hana matatizo na majirani zake na alikuwa akifyatua matofari kwa ajili ya kufanya ukarabati wa nyumba yao na mdogo wake na hata ujumbe aliouacha ulisema ‘Dogo endelea kupambana mimi naondoka’ haukuonesha kama alikuwa na makwazo yoyote na mtu.

Kufuatia tukio hilo diwani huyo amewaasa wananchi kushirikisha ndugu au jamanii pindi wanapopitia katika mambo magumu ili kupata ushauri na kuepukana na vifo vya njia hiyo.

Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kwamba tararibu zingine za kisheria bado zinaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho.