DAR ES SALAAM
Na Alex Kazenga
Matukio ya ajali za barabarani yakihusisha magari, pikipiki, Bajaj, baiskeli, guta na watembea kwa miguu yamepungua kwa kiwango kikubwa nchini.
Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa, anasema:
“Ajali zinatokea kila siku lakini mpaka sasa tumefanikiwa kudhibiti yale matukio ya ajali za kulitetemesha taifa. Hakuna ajali inayotokea sasa hivi tunayoweza kusema imesababisha vifo vya mamia ya watu.”
Pamoja na mafanikio hayo, Mutafungwa anasema furaha ya jeshi hilo ni kuzidisha usimamizi na kudhibiti ajali za barabarani pengine zisitokee kabisa.
“Jukumu la kwanza ni kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, tusingependa hata mmoja apoteze maisha au kupata ulemavu kwa sababu ya ajali,” anasema Kamanda Mutafungwa na kubainisha kuwa juhudi wanazotumia kudhibiti matukio hayo zimeonyesha kuzaa matunda japo kuna changamoto ya watu kutozingatia sheria za usalama barabarani.
Anasema kwa tathmini ya matukio ya ajali kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka jana ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka huu, matukio yamepungua kutoka 978 mwaka jana hadi ajali 760 mwaka huu.
Tathmini hiyo inabainisha kuwa vifo vilivyotokana na ajali za barabarani kwa kipindi hicho ni watu 616 mwaka jana na 544 mwaka huu.
Mbali na vifo, majeruhi walioripotiwa katika kipindi hicho mwaka 2020 walikuwa 1,128 na mwaka huu wamepungua hadi 844.
Kamanda Mutafungwa anasema hatua hiyo imetokana na ushirikiano kati ya jeshi hilo na wadau.
“Hatusemi tumefanikiwa, lakini endapo watumiaji wa barabara watafuata sheria za barabarani bila shuruti, ninaamini ajali zitapungua,” anasema Kamanda Mutafungwa.
Anazitaja sababu kubwa zinazosababisha ajali kuwa ni mwendokasi, magari kupishana pasipo madereva kuchukua tahadhari, matumizi mabaya ya alama za barabarani na uchovu wa madereva.
Visababishi vingine ni ulevi wa madereva, barabara mbovu na hali ya hewa, kwamba ukungu husababisha magari kugongana.
Kwa mujibu wa takwimu za ajali nchini tangu mwaka 2011 hadi mwaka jana, Kamanda Mutafungwa anasema mwelekeo ni mzuri kwani zinapungua mwaka hadi mwaka.
Anasema mwaka 2011 kulikuwa na ajali 23,986 nchini; vifo vilikuwa 3,981 na majeruhi 20,802.
“Hali haikuwa tofauti sana mwaka 2012 ambapo kulikuwa na ajali 23,572; vifo 3,969 na majeruhi 20,111,” anasema.
Mwaka 2013, ajali 23,842; vifo 4,002 na majeruhi 20,689.
Mwaka 2014, ajali 14,360; vifo 3,760 na majeruhi 14,530.
Mwaka 2015, ajali 8,337; vifo 3,468 na majeruhi 9,383.
Mwaka 2016, ajali 9,856; vifo 3,256 na majeruhi 8,958.
Mwaka 2017, ajali 5,578; vifo 2,581 na majeruhi 5,489.
Mwaka 2018, ajali 3,732; vifo 1,788 na majeruhi 3,748.
Mwaka 2019, ajali 2,704; vifo 1,439 na majeruhi 2,834.
Mwaka 2020, ajali 1,714; vifo 1,270 na majeruhi 2,126.
“Hadi kufika hapa kuna mipango na mikakati ambayo Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kimetekeleza,” anasema.
Anautaja mpango wa kwanza kuwa ni utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa wadau wanaotumia barabara.
Elimu ya usalama barabarani inatolewa kupitia madawati yaliyoanzishwa kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Kwenye vituo vya mabasi tunawaelimisha madereva na abiria umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
“Abiria tunawahamasisha kupaza sauti au kutoa taarifa kituoni kupitia namba za simu tunazowapa wakiona vitendo vya dereva vinaweza kusababisha ajali,” anasema Kamanda Mutafungwa.
Kwa upande wa vituo vikubwa vya mabasi, jeshi hilo hutoa elimu kwa mafundi wa ukaguzi ili wawe wakaguzi wa kwanza kabla ya ukaguzi wa polisi.
“Mafundi ni watu muhimu. Tunawasisitiza kuyakagua na kutoa ripoti ya ukaguzi kwa askari wa usalama barabarani kabla ya kuanza safari,” anasema.
Kwenye utoaji elimu ya usalama barabarani, SACP Mutafungwa anasema waendesha pikipiki wamepewa kipaumbele kwa sababu wamekuwa chanzo cha ajali nyingi.
“Tunawaelimisha juu ya uvaaji wa kofia ngumu (helmet) na kutopakia zaidi ya mtu mmoja.
“Madhara ya ‘kubebana mshikaki’ ni makubwa, ikitokea ajali idadi ya watu wanaoumia huwa kubwa,” anasema.
Hadi sasa vijiwe 8,073 vya madereva pikipiki vimeundwa na madereva 166,354 wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani nchi nzima.
Mkoa wa Njombe, madereva pikipiki 500 wamepata mafunzo hayo; Mbeya zaidi ya 3,000 wamepata elimu na leseni za udereva.
Elimu kama hiyo sasa imeelekezwa kwa madereva pikipiki wa Katavi na Kigoma; lengo likiwa ni kuwafikia bodaboda wote nchi nzima.
“Mpango huu upo pia kwa madereva wa Bajaj na watembea kwa miguu, hasa watoto wa shule,” anasema.
Kupitia mpango wa ‘Junior Patrol’, wanafunzi 366,472 wa shule za msingi wameelimishwa namna ya kutumia alama za waenda kwa miguu salama na namna ya kuvuka barabara kwa usalama.
Elimu ya usalama barabarani imetolewa hadi kwa waendesha maguta na baiskeli.
Anawataja madereva wa serikali nao kuwa wanufaika wa elimu hiyo kwa sababu wamekuwa wakilalamikiwa kutoheshimu sheria za barabarani na kuendesha magari kwa kasi.
“Tumewafuata maofisa tawala wa mikoa na wilaya, kuna baadhi waliwakusanya madereva wao tukazungumza nao.
“Hadi kambi za Jeshi la Wananchi (JWTZ) wamejitokeza na kuwa mstari wa mbele kupatiwa elimu ya mafunzo ya usalama barabarani,” anasema.
Mpango wa pili katika kuzuia ajali ni kusimamia sheria za usalama barabarani.
“Eneo la usalama barabarani ni nyeti. Kila mtu ni mdau wa usalama barabarani. Hakuna anayefanya shughuli zake bila kutumia barabara au chombo cha usafiri,” anasema.
Kwa sababu hiyo anasema suala la kuzingatia sheria, miongozo, kanuni, taratibu na alama sahihi na salama ni jukumu wanalolisimamia kwa nidhamu kubwa.
Mtafungwa anasema kupitia wadau wa barabara wa serikali kama Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) wamewasaidia kuweka alama sahihi na salama zinazoonyesha matumizi sahihi ya barabara.
Kwa watu wanaokiuka na kuzivunja sheria hizo, anasema huchukuliwa hatua na ili kufanikisha usimamiaji wa sheria, hutumia vitendea kazi kama tochi mbalimbali.
“Tuna utaratibu wa kuweka polisi wa kutosha barabarani, utaratibu huo tunauita ‘high police visibility’. Kuna askari wanapangwa kufanya doria za magari kila baada ya kilometa fulani na wengine wanakuwa kwenye ‘check points’,” anasema.
Vifaa wanavyokuwa navyo askari wa usalama barabarani ni cha kupimia ulevi ambapo hukitumia kuwapima madereva wanaohisiwa kuendesha magari wakiwa wamelewa.
“Kuna kipindi tunalazimika kupima ulevi kwa kila dereva aliyepo barabarani hasa nyakati za sikukuu. Nyakati hizo tunakuwa makini kuliko kawaida kwa sababu watu wanajisahau na kuvunja sheria kwa makusudi,” anasema.
Mbali na hilo, pia askari wa usalama barabarani wanadhibiti mwendokasi wa magari kwa kutumia tochi, yaani ‘speed reader’.
Tochi hizo zipo nchi nzima na zimewekwa maeneo ambayo dereva hatakiwi kuzidisha mwendo wa kilometa fulani kwa saa.
Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu (LATRA) imewarahisishia kazi ya kusimamia mabasi kwa kufunga kifaa cha kufuatilia mwenendo katika magari hayo (Vehicle Tracking System – VTS).
Akiuzungumzia mfumo wa VTS, Mkurugenzi wa Usafiri wa Barabara LATRA, Johansen Kahatano, anasema hutumika kudhibiti mwendokasi kwenye mabasi.
Kahatano anasema jumla ya mabasi 5,800 yamefungiwa VTS.
“Tunashirikiana na polisi kuuendesha, madereva wanaozidisha spidi zaidi ya kilometa 80 wakibainika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua,” anasema Kahatano.
Anasema wameuunganisha kwenye kompyuta na simu za baadhi ya maofisa wa polisi ili hata wao waone jinsi mabasi hayo yanavyotembea.
Mpango wa tatu wa kudhibiti ajali nchini kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa ni kuendesha operesheni mbalimbali barabarani.
Mpaka sasa zipo operesheni nyingi zinaendelea, akiitaja ile ya kukamata magari mabovu yanayotembea barabarani.
“Kwa ukamataji wa magari mabovu mara kwa mara tunazuia ajali kwani magari mabovu yakiachwa yatembee yatasababisha ajali,” anasema.
Kupitia mpango huo kumekuwapo na kaulimbiu kadhaa, mojawapo ni kampeni ya kuhamasisha matumizi ya viakisi mwanga (reflectors).
“Kanuni ya usalama barabarani inasema gari lolote lenye uzito wa zaidi ya tani tatu linatakiwa kuwekewa viakisi mwanga kulia, kushoto, mbele na nyuma.
“Kanuni hii pia inatuambia gari lolote likiharibika barabarani sharti liwekewe ‘reflector’ na si majani, na liondolewe haraka ndani ya muda mfupi baada ya kuharibika,” anasema.
Anaeleza kuwa zimejitokeza ajali nyingi za magari kujibamiza kwenye magari mabovu yanayosimama barabarani pasipo kufuata taratibu.
Mbali na operesheni hiyo, Mutafungwa anasema sasa hivi jeshi hilo limo kwenye mkakati wa kuwakamata madereva pikipiki wasiofuata sheria za usalama barabarani.
“Operesheni ya kuwakamata bodaboda sasa hivi inaendelea nchi nzima. Tunawakamata bodaboda wote wanaopita kwenye taa nyekundu.
“Bodaboda anaweza kupita kwenye taa nyekundu akawa salama lakini kitendo hicho kikahatarisha maisha ya wengine kwa kusababisha ajali,” anasema.
Anasema bodaboda wasiosimama kwenye vivuko vya watu wanaotembea kwa miguu (zebra) nao hukamatwa kwa sababu huhatarisha usalama wa watu.
Kutosimama kwenye zebra na kupakia watu zaidi ya mmoja kumesababisha ajali nyingi na kusababisha watu wengi kupata majeraha.
“Tukio la bodaboda mmoja kubeba abiria watano ikitokea ajali litasababisha wote wawe maskini kwa kupoteza viungo vyao kuharibika au kupoteza maisha.
“Bodaboda anayebeba mshikaki uwezekano wa watu kuokoka ajali inapotokea huwa mdogo sana,” anasema.
Anasema katika operesheni hiyo, madereva bodaboda wasiovaa kofia ngumu na viatu nao hukamatwa.
Kupitia makosa hayo, Mutafungwa anasema wanaokamatwa wanachukuliwa hatua ikiwamo kutozwa faini, kuonywa kimaandishi ama kufikishwa mahakamani.
Ukaguzi wa magari wa mara kwa mara katika vituo vya mabasi anasema kuwa ni mpango mwingine ambao jeshi hilo linafanya ili kudhibiti matukio ya ajali za barabarani nchini.
Anasema ukaguzi huo unalenga kuhamasisha wamiliki na madereva kuyakagua na kuyahakiki magari yao kabla ya kuyaingiza barabarani.
“Hatua zinazochukuliwa pale ukaguzi unapofanyika na kubaini kasoro, wakaguzi wetu hawataruhusu gari kuendelea na safari.
Pia kupitia ratiba zilizotengenezwa na LATRA zenye muda maalumu unaoonyesha muda sahihi wa mabasi kusafiri na kuwasili vituoni umesaidia kuhusu ajali zinazotokana na mwendokasi.
Ukaguzi wa kushitukiza nao anautaja kusaidia kupunguza matukio ya ajali nchini, ambapo anasema kupitia doria ya ‘high way patrol’ maofisa wa mikoa na makao makuu hushiriki kwa pamoja kufanya ukaguzi.