Na Manka Damia,JamhuriMedia,Mbeya
Watu wawili wamefariki dunia mkoani Mbeya na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali baada basi dogo kufeli breki katika mteremko mkali wa Mbalizi na kugonga magari mengine matatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 9,2022, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya ,Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea leo asubuhi katika eneo la mlima Iwambi nje kidogo ya Jiji la Mbeya barabara kuu ya Mbeya Tunduma.
Amesema kuwa basi lenye namba za usajili T.601 DXC aina ya fuso linalofanya safari zake kati ya Mbeya – Tunduma na Sumbawanga ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya liligonga gari namba T.452 DHD aina ya Toyota Raum.
Kwa Mujibu wa Kamanda Kuzaga amesema kuwa katika ajali hiyo walikufa watu wawili ambao ni watoto wadogo wa familia moja waliokuwa kwenye gari ndogo namba T.452 DHD aina ya Toyota Raum na majeruhi watatu ambapo kati yao mwanaume mmoja na wanawake wawili ambao walikimbizwa hospitali.
Amesema kwamba gari namba T.601 DXC fuso liliendelea kugonga gari jingine lenye namba za usajili T.673 DMW lenye tela namba T.362 DMG aina ya scania lililokuwa linaelekea mkoani Mbeya na gari namba DAD 3981 na Tela lake ABF 75591 aina ya Dofeng lililokuwa limebeba madini ya aina ya Sulpha.
Aidha Kamanda Kuzaga amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi katika eneo lenye mteremko mkali jitihada za kumtafuta dereva wa basi zinaendelea, na majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa Mbeya .
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepuka na kutoa wito kwa madereva kufuata utaratibu uliowekwa wa kupitisha magari ya abiria na malori kwa muda tofauti katika maeneo yenye Milima na miteremko mikali ili kuepuka ajali na madhara makubwa yasitokee kwa abiria.