Na Allan Vicent, JamhuriuMedia, Tabora
Watu 18 wamepoteza maisha na wengine 26 kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea ajali iliyohususisha basi na lori la mafuta, ajali hiyo imetokea katika Kijiji Cha Undomo kata ya Uchama Wilayani Nzega Mkoani Tabora.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea ajali hiyo jana majira ya saa 5 asubuhi wakati basi hilo la Kampuni ya Alpha lililokuwa likitokea Jijini Mwanza kuelekea Jijini Dar Es Salaam lilipongongana uso kwa uso la lori la mafuta la kampuni ya GBP.
Alisema dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T612 CQD na dereva wa lori lenye namba za usajili T 481 AEB wote wamefariki papo hapo.
Kamanda alibainisha kuwa majeruhi waliokuwa na hali mbaya wamekimbizwa katika hospital ya Rufaa Nkinga kwa ajili ya kupata matibabu zaidi na wengine katika hospitali ya wilaya hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwaki Tukai ametoa pole kwa abiria waliojeruhiwa na familia za waliopata ajali hiyo na kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema na wapone haraka.
Tukai aliyekuwa Wilayani Sikonge akimwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa Hospitali ya Misheni Wilayani humo alisema amesikitishwa na ajali hiyo na ameanza safari kuelekea eneo la tukio ili kujionea hali za majeruhi na kusaidia kuwapa huduma inayostahili.
Alitoa wito kwa wananchi na wafiwa wote kuwa watulivu wakati taratibu zikiandaliwa ikiwemo kupewa taarifa za namna ya kuchukua miili ya ndugu zao.
Kamanda wa Polisi aliwataka madereva kuendesha kwa kufuata Sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali.
Alisema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kujua chanzo hasa cha ajali hiyo na hatua nyingine zitafuata.
Alibainisha kuwa hiyo ni ajali kubwa kutokea katika Mkoa huo na kuua idadi kubwa ya watu namna hiyo.