Watu wote 157 waliokuwa safarini katika ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, Boeing 737, wamepoteza maisha baada ya ndege hiyo kuanguka.
Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kuelekea mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ethiopia, abiria waliokuwamo kwenye ndege hiyo ni 149 na watu wengine wanane ni watumishi ndani ya ndege hiyo.
“Tunathibitisha kwamba ndege yetu iliyokuwa na ratiba ya kuruka kutoka Addis Ababa kwenda Nairobi imepata ajali leo,” taarifa ya shirika hilo la ndege imeeleza na kuongeza: “…inaamika kulikuwa na abiria 149 na watumishi wanane wa ndani ya ndege, tutazidi kutoa taarifa zaidi kuhusu ajali hii.”
Ndege hiyo ilianza kuruka saa mbili na dakika 38 asubuhi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole na kupoteza mawasiliano dakika sita baadaye karibu na mji wa Bishoftu, ulioko umbali wa takriban kilomita 60 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Addis Ababa.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, Jumapili asubuhi alitoa taarifa kupitia mtandao wa twitter kwa kuandika: “…natoa salamu zangu za rambirambi kwa familia za wote waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya ndege Boeing 737 ya Shirika la Ndege la Ethiopian iliyokuwa katika ratiba zake za kawaida kuelekea Nairobi, Kenya asubuhi hii.”
Naye Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliziombea faraja familia za waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
“Tumehuzunishwa sana na taarifa za ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines iliyotokea dakika sita tu baada ya ndege hiyo kuruka kwa ajili ya safari yake kuja Kenya. Sala zangu nazielekeza kwa familia, jamaa na marafiki wa waliopoteza maisha katika ajali hii,” aliandika Kenyatta katika mtandao wake wa twitter.
Ndege aina ya Boeing 737 – 800MAX ni sawa kimuundo na ile ya Shirika la Ndege la Indonesia, Indonesian Lion Air, iliyopata ajali mwezi Oktoba mwaka jana, dakika 13 baada ya kuruka kutoka mji wa Jakarta na kuua watu wote 189 waliokuwamo kwenye ndege hiyo.
Ajali kubwa zaidi ya ndege katika Shirika la Ndege la Ethiopia ni ile iliyohusisha ndege aina ya Boeing 737-800 iliyolipuka wakati ikianza safari yake kutoka Lebanon mwaka 2010 na kuua abiria 83 na watumishi saba wa ndani ya ndege hiyo.