WATU 38 wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 100 bado hawajulikani walipo nchini Kongo baada ya kivuko kilichozidisha mzigo kilichokuwa kimejaa watu waliokuwa wakirudi nyumbani kwa ajili ya Krismasi kupinduka katika mto Burisa Ijumaa usiku, kulingana na maafisa wa eneo hilo na mashuhuda.

Kivuko hicho kilikuwa kinasafiri kaskazini-mashariki mwa Kongo kama sehemu ya msafara wa vyombo vingine, na abiria walikuwa hasa wafanyabiashara waliokuwa wakirudi nyumbani kwa ajili ya Krismasi, alisema Joseph Joseph Kangolingoli, meya wa Ingende, mji wa mwisho kabla ya eneo la ajali. Watu ishirini wamethibitishwa kuokolewa hadi sasa.

Kupinduka kwa kivuko hicho kumetokea chini ya siku nne baada ya boti nyingine kupinduka kaskazini-mashariki mwa nchi, na kusababisha vifo vya watu 25.

Kwa mujibu wa Ndolo Kaddy, mkazi wa Ingende, kivuko hicho kilikuwa na “zaidi ya watu 400 kwa sababu kilisimama katika bandari mbili, Ingende na Loolo, njiani kuelekea Boende, hivyo kuna sababu ya kuamini kwamba kulikuwa na vifo zaidi.”

Maafisa wa Kongo mara nyingi wameonya dhidi ya kuzidisha mzigo na kuahidi kuchukua hatua dhidi ya wale wanaokiuka hatua za usalama wa usafiri wa majini. Hata hivyo, katika maeneo ya mbali ambako abiria wengi wanatoka, wengi hawawezi kumudu usafiri wa umma kwa barabara chache zinazopatikana.

Watu wasiopungua 78 walikufa maji mwezi Oktoba wakati boti iliyozidisha mzigo ilipozama mashariki mwa nchi hiyo, huku watu 80 wakipoteza maisha katika ajali kama hiyo karibu na Kinshasa mwezi Juni.