Mchezaji wa mpira wa miguu wa wanawake wa Tanzania Aisha Masaka amejiunga na klabu ya Brighton & Hove Albion ya Ligi Kuu England.

Brigton @ Hove Albion imemtambulisha Aisha kupitia mitandao yake na kijamii.

“Tunafurahia kutangaza usajili wa mshambuliaji Aisha Masaka kutoka BK Hachen kwa masharti yasiyofichuliwa, kutegemea michakato ya kawaida ya kisheria.” imesema taarifa ya Brington.

Akizungumza baada ya kusajiliwa Aisha amesema anafurahi kukipiga Ligi Kuu wanawake England.

“Halo mashabiki wa Brighton. Ni Aisha Masaka hapa. Ninafuraha sana kujiunga na klabu na natarajia kukutana nanyi wote. Kwaheri!”, amesema Aisha katika video kwenye mitandao ya Brighton.

Mkurugenzi Mtendaji wa soka la wanawake na wasichana wa Albion, Zoe Johnson, amesema klabu inafurahia kumkaribisha Aisha katika timu.

Johnson ameongeza kusema: “Ameshindana katika kiwango kikubwa nchini Sweden na pia ameiwakilisha Hacken katika Ligi ya Mabingwa.Ni mshambuliaji mwenye nguvu, anayetawala mpira na mfunga mabao wa asili.”

Aisha mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Hacken mwaka 2022 akitokea Yanga, ambapo awali alikuwa akicheza Alliance ya Mwanza.

Safari ya Aisha Masaka kutoka ligi za mitaa za Tanzania hadi Ligi Kuu England ni ushahidi tosha wa kipaji, bidii na dhamira yake.

Mafanikio ya juhudi zake yatawahamasisha wanasoka wasichana Tanzania kuona kwamba kwa kujitoa na uvumilivu, inawezekana kufika hatua kubwa kimataifa.

Katika misimu yake miwili Hacken, Aisha alisaidia timu hiyo kumaliza ya pili katika Ligi ya Sweden na kufika robo fainali za Ligi ya Mabingwa ya UEFA msimu uliopita kabla ya kufungwa na PSG.

Wakati akicheza Ligi Kuu ya Tanzania, alishinda tuzo ya mfungaji bora katika msimu wa 2020/21 baada ya kufunga mabao 35 katika mechi 20 akiwa kwa Yanga.

Katika kiwango cha kimataifa, amecheza mechi 15 na timu ya taifa ya wanawake Tanzania(Twiga Stars), akifunga magoli 9 tangu alipojiunga nayo mwaka 2021.

Masaka pia aliwakilisha nchi katika Kombe la COSAFA chini ya umri wa miaka 17 ambapo Tanzania ilishinda mashindano hayo na yeye akawa mfungaji bora.

Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Tanzania kilichofuzu kwa WAFCON 2024 na ataelekea Morocco msimu ujao

Timu 12 zitashiriki Ligi Kuu ya wanawake England msimu wa 2024/2025.

Timu hizo ni Arsenal, Aston Villa, Brighton & Hove Albion, Chelsea, Crystal Palace, Everton, Leicester City, Liverpool, Manchester City, Manchester United, Tottenham Hotspur na West Ham United.

Please follow and like us:
Pin Share