KAMPUNI ya Airpay imekabidhi vishkwambi kwa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) ili viweze kutumika katika usajili na uombaji wa mikopo kwa njia ya kidijitali.
Airpay na ZEEA kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha imetengeneza mfumo wenye lengo la kuwarahisishia wajasiriamali wa Zanzibar kupata mikopo kidijitali hivyo uwepo wa vishkwambi hivyo vitarahisisha shughuli hiyo.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Airpay, Kunal Jhunjhunwala ndiye aliyekabidhi vishkwambi hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan ambaye pamoja na timu yake ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) imefanya ziara ya siku tatu nchini India ili kujionea uwezo wa mifumo hiyo ya kidijitali ya Airpay inavyofanyakazi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kwa vishkwambi hivyo nchini India , Mkurugenzi Mtendaji wa Airpay Tanzania, Yasmin Chali amesema lengo la kutoa vitendea kazi hivyo zikatumike katika kurahisisha usajili, utoaji mikopo kidijitali na kusaidia kuwafikia wajasiriamali wengi kwa urahisi.
“Tunaamini kupitia vishkwambi hivi itarahisisha watu wengi kufikiwa kwa urahisi, tunaomba wajasiriamali wenye vigezo wasisite kujitokeza kufanya maombi ya mikopo kwa njia ya kidijitali,” amesema Chali.

Naye Burhan amesema anaishukuru Kampuni ya Airpay kuwapatia vishkwambi hivyo ambavyo ameahidi kuwa vitapelekwa kwenye mabaraza ya miji na halmashauri zote za Unguja na Pemba.
Amesema mikopo ya kidijitali ni mkombozi kwa wajasiriamali hivyo amewataka kuendelea kujitokeza kwa wingi kuomba ili waweze kujikwamua Kiuchumi.
“Tunaishukuru Airpay kwa kutoa vishkwambi, tutaendelea kufanyakazi kwa ukaribu na kutoa ushirikiano utakaohitajika,” amesema Mohamed.

