Mpita Njia, maarufu kama MN wiki mbili zilizopita alikuwa katika miji ya Njombe na Makambako kwa nyakati tofauti, ndani ya Mkoa wa Njombe kwa Wabena, Wahehehe, Wakinga na makabila mengine mchanganyiko ya Tanzania na hata watu wa mataifa mengine, ikizingatiwa kuwa Afrika ni moja, chambilecho Mwalimu Julius Nyerere na Azimio la Arusha.
Naam, Njombe na Makambako kuna mengi hasa! Ndiyo, ni mengi, yenye kuvutia na hata kukera, achilia mbali yanayohuzunisha kama ilivyo kwa matukio ya mauaji ya hivi karibuni ya watoto.
Katika pitapita zake, MN amekutana na mengi yaliyojiri huko na mojawapo ni vituo vikuu vya mabasi katika miji hiyo ya Makambako na Njombe. Si wakati wa mvua ama jua, hali ya vituo hivyo ni mbaya, tena mbaya kiasi cha kukera, kwa watoto wa mjini watasema ni mbaya kwa kiwango cha ‘lami’.
Kwa bahati mbaya, MN alikuwa huko katika kipindi cha mvua na kushuhudia ubaya huo wa kiwango cha ‘lami’, ambao uliwekwa bayana hata na watumiaji wa kila siku wa vituo hivyo, achilia mbali abiria wanaosafiri kuelekea maeneo mbalimbali ya nchi.
Ni tope la ujiuji, mwenye kiatu kisafi ni lazima kichafuke, na itabidi uwe na umakini uliopitiliza ili kunusuru nguo yako isichafuke kutokana na matope hayo wakati ukitembea ndani ya vituo hivyo kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Hali hii ilimshangaza MN kwa sababu kadhaa, mojawapo ni umashuhuri wa miji hii wa miaka nenda – rudi. Nani katika nchi hii hajawahi kusikia kuhusu Makambako ama Njombe, miji maarufu kwa biashara sambamba na uzalishaji wa mazao ya kilimo, ikiwamo misitu inayozalisha mbao na bidhaa nyingine zinazotokana na mbao?
Kwa hali hiyo, ni dhahiri kwamba Njombe na Makambako ni halmashauri zenye mapato ya kutosha angalau kuboresha vituo hivyo vikuu vya mabasi ili hata wale wanaotozwa ushuru kutokana na matumizi ya vituo hivyo wajihisi kutozwa kihalali, kwa kuwa watakuwa wanatoa huduma zao katika mazingira nadhifu.
Mpita Njia, alwatani kama MN, anabaki kujiuliza tena, inakuwaje hali hiyo ya matope ya ujiuji nyakati za mvua na vumbi la poda nyakati za kiangazi katika miji ambayo moja ya vyanzo vyake vya mapato ni vituo hivyo vikuu vya mabasi? Hivi ile kanuni kwamba boresha mazingira ya biashara ili uboreshe mapato yako imewapita kando watendaji wa hizi halmashauri za miji hii mikongwe nchini?
Mbona wenzao wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wameweza? Tena wameweza si kwa kuomba fedha kutoka serikali kuu, bali kwa kuweka mipango yao vema kwa imani kuwa, kwa kadiri watakavyoboresha mazingira ya kituo chao kikuu cha mabasi ndivyo ambavyo watakuwa na uhakika wa mapato.
Au bado anasubiriwa Rais John Magufuli kutoka Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam kuwapa wazo la kuboresha mazingira na mandhari ya vituo vikuu hivyo vya mabasi kwenye miji yenu ndipo muanze kugutuka?