Mvua zimekuwa jambo la kutia aibu katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa wengi jijini Dar es Salaam, kama ni suala la kuchagua kati ya mvua na jua ili kutunza aibu ya uongozi wa jiji hilo, basi ni afadhali kuvumilia joto la kiangazi kuliko mvua za wakati wa msimu wa masika.
Mvua zimekuwa zikiumbua udhaifu wa viongozi wa Jiji la Dar es Salaam na halmashauri zake katika suala la miundombinu mibovu. Wakati wa mvua kama ilivyodhihirika hivi karibuni, baadhi ya barabara tena katikati ya jiji zimekuwa na madimbwi. Ni madimbwi kama ambavyo Mpita Njia ama maarufu MN alivyoshuhudia katika pilikapilika zake za kuwajibika kwa manufaa ya taifa hili.
Kama anavyotamka mara kwa mara Rais Dk. John Magufuli, haya yanatokea wakati Mkuu wa Mkoa yupo…Mkurugenzi wa Jiji yupo, wakuu wa wilaya wapo, sambamba na wakurugenzi wao. Wote hawa wapo, miongoni mwao wanapita katika barabara hizo hizo zenye madimbwi, aibu ya jiji kuwa na ‘vijibwawa’ katika barabara zake mashuhuri katikati ya mji kwao si shida, ni jambo la kawaida. Wamezoea. MN anaona kama vile viongozi hawa wamefikia ukomo wa tafakuri. Hawaoni mbadala.
Katika hilo, mvua inapozidi baadhi ya mitaa vijana wasio na ajira hujitokeza kuvusha watu kwa kuwabeba migongoni au kuweka ‘ubao’ wa kuvukia na kutoza fedha kidogo.
Aibu hii ni dhahiri katika Mtaa wa Pamba, Mtaa wa Ohio mkabala na jengo la Maarifa, eneo la Kitega Uchumi kuelekea Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Barabara ya Morogoro mkabala na ofisi za Halmashauri ya Jiji ambako wakati mwingine watu hubebwa migongoni ili kuvushwa kwenye madimbwi hayo ya maji.
Anachojiuliza Mpita Njia ni kwamba, viongozi hawa licha ya kusafirishwa kwa fedha za umma katika miji mbalimbali mikubwa duniani, hawajajifunza namna ya kuweka mikakati ili angalau katikati ya jiji hilo kuwe na haiba inayoridhisha wakati wote – kiangazi ama masika? Aibu tupu hii. Rais Magufuli, baba tazama wateule wako na hata kuwakumbusha wajibu wao, wasikutwishe mzigo usiostahili.