Shirika la AGPAHI, linalojihusisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI, limezindua majengo mawili kwa ajili ya Huduma za Tiba na Matunzo kwa watu wanaoishi na vimelea hivyo.
Shirika hilo linalofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Shirika la Kimarekani (CDC) nchini Tanzania, limezindua majengo hayo kwenye Zahanati ya Kagongwa wilayani Kahama, na Kituo cha Afya cha Nindo kilichopo katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga.
Majengo hayo yamezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, aliyesema kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga inatambua mchango wa AGPAHI linalofanya kazi zake katika mkoa huo, Geita na Simiyu katika jitihada zake za kupambana na VVU.
“Natambua kuwa sote tunazifahamu athari zinazotokana na ugonjwa hatari wa UKIMWI katika jamii na pia katika maendeleo ya nchi yetu,” anasema Rufunga.
“Nawaomba sana tuvitumie vituo hivi katika huduma za upimaji na ushauri nasaha ili tuzilinde na kuzitambua afya zetu, na sisi kama Serikali tunaahidi kutoa huduma nzuri kwa wananchi wote watakaofika hapa kupata huduma.’’
Shirika la AGPAHI limetokana na shirika la kimataifa liitwalo EGPAF; taasisi ambayo inasaidia upatikanaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu wenye virusi vya UKIMWI.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Lauren Rugambwa Bwanakunu, amesema Shinyanga kuna vituo 43 vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI, na vituo 310 vinavyotoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita.
Machi mwaka huu, AGPAHI ilianza kazi zake kwa msaada wa watu wa Marekani kwa kusaidiana na Serikali ya Tanzania.
Akikabidhi msaada wa magari kwa nyakati tofauti mbele ya viongozi wa halmashauri hiyo pamoja na wabunge, Rugambwa Bwanakunu anasema magari hayo mapya aina ya Toyota Land Cruiser yametolewa kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia CDC, ya hapa nchini, huku kila moja likigharimu Sh. milioni 89 bila kodi.
AGPAHI imeshawawezesha na vifaa tiba kama dawa, vitendanishi na vifaa vya maabara ili kuboresha huduma za ufuatiliaji wa WAVIU hususani upimaji wa kinga yaani CD4.
Pia AGPAHI imekabidhi pikipiki tano ambazo zilipelekwa kwenye vituo vya Bulekela (Kishapu), Ushetu, Chambo na Bulungwa mkoani Shinyanga, na Kituo cha Afya Dutwa kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
AGPAHI imekuwa ikiboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa kukarabati na upanuzi wa jengo la zahanati ya Bulekela lililogharimu kiasi cha Sh. milioni 19 za Kitanzania.
Pia imefunga mfumo wa umeme jua (solar panels) katika vituo vya afya vya Nhobola na Bunambiyu, ambavyo vimegharimu kiasi cha Sh milioni saba.
Anasema kwamba katika kuhakikisha huduma za viwango (quality care) katika wilaya za Mkoa wa Shinyanga, AGPAHI imekuwa ikiwajengea uwezo watoa huduma na kamati za uendeshaji huduma za afya (CHMT) kupitia mafunzo ya muda mfupi yaani semina, warsha na makongamano mbalimbali.
AGPAHI yamwaga misaada Shinyanga
Jamhuri
Comments Off on AGPAHI yamwaga misaada Shinyanga
Previous Post
GST yaongeza thamani madini ya nikeli
Next Post
Wazee ‘wamaliza kazi’ CCM