*DG Eric asimamisha kazi wafanyakazi 13, orodha ya wahusika yatajwa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wiki moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza watu waliohusika na ununuzi wa mifumo iliyoiingiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika hasara, bandarini sasa kunachemka, JAMHURI limebaini.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, ameanzisha uchunguzi wa kina kubaini walioshiriki kuongeza gharama za ukarabati wa ‘Tag’ ya kuvuta meli kutoka Sh bilioni 1.3 hadi Sh bilioni 6.34. Tayari wafanyakazi 13 wamesimamishwa kazi na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam amehamishiwa makao makuu.

Rais Samia amesema kuna watu walishiriki kuiingiza nchi kwenye gharama kubwa za kununua mfumo wa Enterprise Resource Planning (ERP) na mifumo mingine ila bado wapo kazini, hivyo akaagiza wachukuliwe hatua kali za kisheria.

JAMHURI limeona orodha ya watu wanaohusishwa na ununuzi wa mifumo miwili iliyolalamikiwa na Rais Samia, ambapo baadhi walikwisha kustaafu au wengine walikwisha kuacha kazi, ambapo kati yao mtumishi mmoja tu ndiye jamii iliona anachukuliwa hatua baada ya agizo la Rais mapema mwaka huu.

Aliyechunguzwa na kuchukuliwa hatua hadi kutenguliwa uongozi wake ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Injinia Deusdedith Kakoko, ilhali majina mengine yaliyomo kwenye orodha hayajasikika kutajwa popote.

Orodha hiyo yenye majina mazito imekabidhiwa kwa vyombo vya dola vya uchunguzi, ambapo JAMHURI linafahamu kuwa wengi tayari wamekwisha kutakiwa kutoa maelezo. Mfumo wa ERP umegusa watumishi 12 ambao majina yao yamekabidhiwa kwenye vyombo vya dola,  hivyo wakalazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kama ilivyotokea kwa Kakoko.

Waliosimamishwa ni Leticia Mutaki (Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Anna B. Kessy (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Kokutulage Kazaura (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Marcelina Mhando (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Juma Mwenda (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Caleb Kulwa (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Alex Seneu (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Jesse Shalli (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Evance Bahati (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Karl Wilfred (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini) na Allen T. Banda (Mjumbe wa CTB (Kikao Na. 192/2019). Hawa walikuwa wanashikilia nyadhifa hizo wakati wa mchakato wa kutoa zabuni ya ERP.

Taarifa ya uchunguzi wa mfumo wa ERP inataja pia vigogo 22 wa Bandari wakiwamo wakurugenzi wakuu watano. 

Wahusika waliokuwa watumishi wa TPA wanaotajwa kwenye taarifa ya ERP ni:-  Mhandisi Madeni Kipande (Mkurugenzi Mkuu wa TPA), Ephraim N. Mgawe (Mkurugenzi Mkuu), Mhandisi Deusdedit Kakoko (Mkurugenzi Mkuu wa TPA), Awadhi Massawe (Kaimu Mkurugenzi Mkuu) na Flavian H. Kinunda (Kaimu Mkurugenzi Mkuu).

Wengine ni Mhandisi Augustine W. Phillip (Mkurugenzi wa Manunuzi/Mjumbe wa CTB (Kikao Na. 192/2019), Phares Magesa (Mkurugenzi wa TEHAMA), Kilian Chale (Mkurugenzi wa TEHAMA), Mashaka Kisanta (Mkurugenzi wa Ununuzi), Ramadhani Mwikalo (Mshauri Mwelekezi) na Janet Ngowi (Network Support Manager).

Wamo pia Ayubu Kamti (Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA), Boniface Mbuya (Afisa Manunuzi), Casmir Lujegi (kwa niaba ya Mkurugenzi wa Ununuzi), Saleh Sapi (Meneja Uhandisi Umeme), Abdalah Mwinyi (Daktari Mkuu), Teophil Kimaro (Meneja Kitengo cha Ununuzi na Katibu wa Bodi ya Zabuni), Nelson Nanyaro (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Fransisca K. Muhindi (Mjumbe wa CTB (Kikao Na. 192/2019), Deatus Kaindi (Mjumbe wa CTB (Kikao Na. 192/2019) na Mhandisi Mussa Shilla (Mjumbe wa CTB (Kikao Na. 192/2019).

Mfumo wa ulinzi (Integrated Security System – ISS) nao haujaacha watu salama. Wafanyakazi waliokuwa bado wapo kazini wamesimamishwa kazi na wale waliokwisha kuondoka kazini uchunguzi dhidi yao umeanza.  

Watumishi wa TPA wanaotajwa kwenye taarifa ya ISS ni Kokutulage Kazaura (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Christian Chiduga (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria) na Ntandu Mathayo (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini).

Wahusika waliokuwa watumishi wa TPA wanaotajwa kwenye taarifa ya ISS, ambao sasa hawapo tena TPA ni Mhandisi Madeni Kipande (Mkurugenzi Mkuu wa TPA), Ephraim N. Mgawe (Mkurugenzi Mkuu), Hebel Nathan Mhanga (Meneja Bandari ya Dar es Salaam), Awadhi Massawe (Kaimu Mkurugenzi Mkuu), Rajab Rawson Mdoe (Naibu Mkurugenzi Mkuu), na P. D. Gawile (Mjumbe wa Bodi ya Zabuni).

Wamo pia Phares Magesa (Mkurugenzi wa TEHAMA), Kilian Chale (Mkurugenzi wa TEHAMA), Mashaka Kisanta (Mkurugenzi wa Ununuzi), Hassan. M Kyomile (Mjumbe wa Bodi ya Zabuni) Dk. Geofrey Kalokola (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Jesse Shalli (Katibu wa Kamati ya Tathmini), Kilian Chale (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini), Lucas Kiswiza (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini) na Joel Chacha (Mjumbe wa Kamati ya Tathmini).

Watumishi hawa Rais Samia amesema wale waliopo kazini haiwezekani waitie mamlaka hasara kisha waendelee na kazi bila kuchukuliwa hatua yoyote. 

Tangu ametoa agizo hili, vyombo vya dola na uongozi ndani ya Bandari umekuwa katika uchunguzi mkali kubaini nani anahusika na uingizaji wa mifumo hiyo miwili ya ERP na ISS ambayo taarifa ya ukaguzi inasema imeitia hasara Bandari.