Kwa jinsi ilivyotekeleza maagizo ya Rais John Pombe Magufuli, Bohari ya Dawa nchini (MSD) imedhihirisha kuwa watumishi wa umma wakiongozwa vyema, Tanzania inaweza kupata maendeleo ya kasi.

Taarifa zilizoifikia JAMHURI zinaonesha kuwa baada ya Rais Magufuli kuagiza zilizokuwa fedha za sherehe bungeni zipunguzwe kutoka Sh milioni 275 hadi Sh milioni 24, kiasi cha Sh milioni 251 kilichosalia kiliwekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya MSD kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli alipoagiza MSD kufungua maduka ya dawa katika hospitali na kuuza dawa kwa bei nafuu, mwanzo wafanyakazi wa MSD walimshangaa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, alipojipa muda wa wiki moja kuhakikisha duka la dawa la MSD linafanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Bosi Bwanakunu alipomwambia Katibu Mkuu Kiongozi [Balozi Ombeni Sefue] kuwa duka la dawa la MSD lingekamilika ndani ya wiki moja, tulitaka kupasuka. Tulijiuliza atawezaje kuikamilisha kazi hii? Tukasema inawezekana hajui urasimu wa serikalini na kwa kuwa ametoka sekta binafsi ndiyo maana ametoa ahadi ya kukamilisha duka katika muda mfupi kiasi hicho, hivyo tulidhani linamfunga…lakini bwana wee acha tu, ameweza,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa MSD.

 Baada ya kuapishwa Novemba 5, siku nne baadaye Rais Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuta wagonjwa wamelala chini, tukio lililomhuzunisha kwa kiwango kikubwa.

 Kilichofuata, alikwenda kuhutubia Bunge, ambapo kila Bunge linapozinduliwa huwa wabunge wanasherehekea, lakini zamu hii Rais Magufuli amekata bajeti ya sherehe kutoka milioni 275, hadi Sh milioni 24. Rais aliagiza Sh 251 zilizosalia zitumike kununua vitanda kwa ajili ya wagonjwa wanaolazwa chini Muhimbili.

 Mkurugenzi Mkuu wa MSD Laurean Bwanakunu alikabidhiwa orodha ya vifaa vilivyopaswa kupelekwa Muhimbili mara moja ikiwa ni pamoja na vitanda 300, magodoro 300, viti maalum (wheelchairs) 30 vya kusukuma kwa ajili ya wagonjwa, vitanda maalum (stretchers) 30 vya kubebea wagonjwa, shuka 1,695 na mablanketi 400.

Agizo la Rais lilitolewa Novemba 20, ambapo MSD ililipa kipaumbele cha hali ya juu na kuhakikisha inakusanya vitanda kutoka maduka na bohari zake nchi nzima usiku na mchana. “Kuna baadhi ya vitanda tulivichukua hadi bohari za Kanda ya Ziwa vikasafirishwa usiku na mchana kufanikisha agizo hili,” anasema Bwanakunu.

 Kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa umma, Serikali inaponunua bidhaa kutoka katika duka inalolimiliki, hailazimiki kufuata mlolongo wa taratibu za ununuzi wa umma kwa njia ya zabuni na hili ndilo lililowezesha vitanda kupatikana ndani ya siku nne.

 Novemba 23, 2015, MSD ilikabidhi rasmi vifaa hivyo, ambapo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Sefue alivikagua na kuvikabidhi Muhimbili. Katika historia ya nchi hii, hakuna agizo lililopata kutolewa na kiongozi yeyote likatekelezwa kwa ufanisi na uharaka wa aina hii.

Bohari ya Dawa ndiyo taasisi pekee inayonunua, kutunza na kusambaza dawa na vifaa tiba vya Serikali. MSD inazo kanda za Mbeya, Iringa, Moshi, Dodoma, Mtwara, Tabora, Mwanza na Dar es Salaam. Pia ina vituo viwili vya mauzo vya Muleba na Tanga.

 Wakati anapokea vitanda na vifaa tiba vilivyotajwa, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue alisema Rais Magufuli anakerwa mno na suala la wananchi kukosa dawa wanapokwenda kupata matibabu hospitalini, hivyo akaagiza MSD kuanzisha maduka ya dawa kwa kuanza na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

 Ghafla, Sefue alipomhoji Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bwanakunu, kazi hiyo ingekamilika ndani ya muda gani, Bwanakunu akasema ndani ya wiki moja.

 “Nilipotoa kauli hiyo mbele ya Katibu Mkuu Kiongozi nilimaanisha kuwa lazima tumalize kazi hii ndani ya muda niliousema. Nilisimamia mwenyewe kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu na ikawezekana.

 “Kwa sisi tuliozoea kwenye private sector (sekta binafsi) utendaji wa aina hii ndiyo wa kila siku. Sisi kuamka saa 8 usiku ukaanza safari ni jambo la kawaida na najitahidi kujenga culture (utamaduni) hii kwenye taasisi ninayoiongoza. Ufanisi, uaminifu na kujituma kwangu ni kipaumbele na naamini tunaofanya kazi wote wananielewa hivyo,” anasema Bwanakunu.

Agizo hili limeendana na Mpango Mkakati wa MSD kufungua maduka kwenye mikoa yote yenye kanda za MSD, ingawa baadhi ya mikoa isiyo na kanda pia imeomba kupewa fursa ya kufungua maduka ya dawa ya MSD na iko tayari kutoa vyumba vya kuweka maduka hayo.

 MSD inalenga kufungua maduka ya dawa karibu au ndani ya hospitali za rufaa, mikoa na wilaya, lengo kuu likiwa kuhakikisha dhima ya “Kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora kwa bei nafuu kwa Watanzania wote” inatekelezwa kwa vitendo.

 

 Duka la MSD Muhimbili

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Donald Mbando amelizindua duka hili Novemba 2, 2015. Duka hilo limewaonesha wananchi sura wasiyoijua kwani kuna baadhi ya dawa linazoziuza Sh 1,200 wakati dawa sawa na hizo kwenye maduka binafsi zinauzwa hadi Sh 18,000.

Duka hili ni ofisi iliyokamilika, ambayo ina watendaji wakuu wanne ambao ni Msimamizi Mkuu wa duka ambaye ni Mfamasia kitaaluma, Mhasibu, Afisa Huduma kwa wateja na Afisa Mauzo. Maduka mengine yote ya MSD yatakuwa na watendaji wa aina hiyo.

 

 

Duka la MSD Mbeya

Katika mwaka huu wa fedha, tayari MSD imeanzisha duka kama hilo mkoani Mbeya, ambalo tayari limeanza kutoa huduma kwa wadau wote. Mbali na kuuzia wananchi, duka hili linaziuzia dawa hospitali zote zinazotoa huduma za Bima ya Afya.

 

Mipango ya kupanua huduma

Dodoma

Mkurugenzi Mkuu anasema MSD imefanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma, Prof. Peter Gesase, ambapo naye ameahidi kuwapatia eneo MSD kwa ajili ya kuendeshea duka la MSD litakalohudumia wateja wote wa Kanda ya Kati.

 Mbali na Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameeleza kuwa wao wana duka kwa ajili ya vifaa tiba na dawa kwa ajili ya wateja wao, hivyo wako tayari MSD ipewe jukumu la kuhakikisha duka la hospitali hiyo lina dawa wakati wote.

 

Arusha

 “Kwa Kanda ya MSD Moshi ambayo inahudumia mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha nimefanya ziara ambayo bado naendelea nayo na kuzungumza na watendaji kadhaa ambapo pamoja na mambo mengine ni kuangalia uwezekano wa kupata maeneo kwa ajili ya kufungua duka la MSD,” anasema.

Hata hivyo, habari njema ni kwamba kwa Arusha tayari uongozi umetoa kwa MSD eneo ndani ya Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kufanyia shughuli hiyo, hivyo huu utakuwa mkoa mmojawapo utakaofaidika na huduma bora za MSD.

 

Singida

 Anasema Mganga Mkuu wa Mkoa Singida naye ameeleza kuwa wao wana duka tayari, hivyo MSD itawauzia bidhaa kwa ajili ya kuhakikisha duka hilo lina vifaa wakati wote.

 

Mwanza

Mkurugenzi wa MSD pia tayari amekutana na viongozi wa Mkoa wa Mwanza ambapo ameeleza mpango wa MSD wa kuanzisha maduka kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wananchi, nako amepatiwa eneo ndani ya Hospitali ya Sekou Toure.

 Kwa sasa MSD iko kwenye maandalizi ya ukarabati wa vyumba kwa ajili ya maduka ya dawa mkoani Mwanza na Arusha, ambayo Bwanakunu anasema yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba.

 Anasema maduka hayo yataiongezea bohari wigo wa kutoa huduma kwa wananchi kinyume na utaratibu uliozoeleka wa huduma ya dawa na vifaa tiba kutolewa kupitia mali zinazohifadhiwa bohari (stock items) kwa mujibu wa orodha ya Taifa ya dawa na vifaa tiba (National Essential Medicine List), mali za miradi misonge (vertical programs items) na dawa na vifaa tiba takribani aina 3,000 zinazoagizwa nchini kwa mahitaji maalum.

 

 Nembo dawa za Serikali

Bwanakunu anasema kwa sasa dawa za MSD kama dawa za Serikali zinawekewa nembo ya GOT na wanatumia mfumo wa Bar-coding kwa ajili ya kupokea, kutunza na kusambaza dawa na vifaa tiba. “Hii yote tunalenga kudhibiti wizi wa dawa za umma,” anasema.

 “Mpango huu tumeuanzisha tangu mwaka wa fedha uliopita tumeanza kuziwekea alama ya GOT bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na vidonge. Zamani mkumbuke ilikuwa tunaweka kwenye vifungashio vya ndani na maboksi, lakini sasa hata kidonge. Vidonge hivyo ambavyo tayari vimeweka nembo ya GOT hadi sasa vipo aina 45 na tunaendelea kuwapa maelekezo wazabuni ili vyote viwekwe alama hizo.

“Kwa sasa unaweza ukaona nembo hiyo kwenye dawa za serikali za Diclofenac, Amoxicillin, Ciprofloxacin, Cotrimoxazole, Paracetamol na Magnesium,” anasema.

 Tangu mwaka wa fedha uliopita, MSD imeanza kutumia mfumo wa Bar-coding katika upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba. Mfumo huu unaiwezesha MSD kupata taarifa sahihi za bidhaa zake na kurahisisha utendaji na ufuatiliaji, anasema.

Mkurugenzi Mkuu anawataka wateja wa MSD kufanya maoteo (predictions) sahihi, kuandaa na kuleta ‘oda’ zao kwa wakati.

 Bwanakunu amewataka wateja wa MSD kutumia vyanzo vyao vingine vya mapato kununua dawa za ziada pale mahitaji yasipoendana na bajeti ya Serikali kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

“Inawapasa [wateja] kufuatilia salio la akaunti zao (Statement of accounts) ili kujua kiasi ulichobaki nacho ukilinganisha na mahitaji wanayoomba na katika kufanya hivyo, wawahusishe MSD kwenye vikao vyao vya kujadili utendaji na utekelezaji wa majukumu ili MSD iweze kujua mahali pa kurekebisha.

 “Tunawataka pia kufanya ulinzi shirikishi wa dawa za Serikali. Tunasema toa taarifa pale unapoona dawa za Serikali zinahujumiwa,” anasema Bwanakunu.

 Kimsingi, amesema watendaji serikalini wakiamua nchi hii inaweza kumaliza matatizo yanayolikabili Taifa ndani ya muda mfupi, kwani ameridhika kuwa Watanzania wana uwezo wa kufanya kazi hata baada ya muda wa kazi kufanikisha maagizo halali ya Serikali kama MSD ilivyofanya katika agizo la Rais Magufuli kuhusiana na suala la vitanda Muhimbili na maduka ya dawa.