Agizo la Rais John Magufuli kwa taasisi za serikali na mashirika ya umma kuhamisha ofisi zao kutoka kwenye majengo binafsi kwenda majengo ya serikali limewaacha baadhi ya wamiliki wa majengo katika maumivu baada ya taasisi hizo kuhama.

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo zimehamisha ofisi zao kutoka katika majengo ya watu na taasisi binafsi na kuhamia majengo yanayomilikiwa na taasisi za umma.

Akiwa katika ziara mkoani Rukwa, Rais Magufuli alitoa siku tano kwa TANROADS kuwa wamehama katika jengo la Airtel eneo la Morocco jijini Dar es Salaam na kuhamia kwenye majengo ya serikali. 

Hakuishia hapo, kwani alionyesha kushangazwa kwake na taasisi za umma ambazo bado zinaendelea kukodi ofisi kwenye majengo ya watu binafsi wakati majengo mengi ya serikali yamebaki wazi, hasa jijini Dar es Salaam, baada ya serikali kuhamia Dodoma.

TANROADS ilitekeleza agizo hilo kabla ya kwisha muda uliotolewa na Rais Magufuli na kuhamishia ofisi zao kwenye jengo linalomilikiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, TRA nayo ikatekeleza kwa vitendo agizo hilo kwa kuhamisha ofisi zake kadhaa kutoka katika majengo ya watu binafsi na kuhamia kwenye majengo ya serikali.

Ili kufanikisha suala hilo, baadhi ya ofisi za TRA ambazo zilikuwa katika jengo la Mapato House na Summit Tower zilihamisha ofisi ili kuhakikisha kuwa ofisi zote ambazo zilikuwa katika majengo ya watu binafsi zinapata nafasi kwenye majengo ya serikali kuanzia mwezi huu.

Ofisi zilizobadilishiwa majengo ni pamoja na ofisi ya Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa ambayo ilikuwa ikiendesha shughuli zake katika jengo la serikali la Mapato House.

Kwa sasa shughuli za ofisi hiyo zimehamia ghorofa ya kwanza ya jengo jipya la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), lililopo Sokoine Drive jijini Dar es Salaam.

Idara ya Walipa Kodi Wakubwa nayo ilikuwa inaendesha shughuli zake katika jengo hilo hilo la Mapato House, lakini kwa sasa wamehamishia shughuli zao katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango lililoko Mtaa wa Madaraka katika Manispaa ya Ilala.

Ofisi za TRA Mkoa wa Kodi wa Ilala, zilizokuwa jengo la Summit Tower lililopo Mnazi Mmoja, TRA – Shauri Moyo walikuwa katika jengo la Marium Tower na TRA Upanga ambao walikuwa Samora House wote wamehamishia ofisi zao kwenye jengo la Mapato House.

Kaimu Meneja Mkoa wa Kodi Ilala, Stephano Kauzeni, amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa walilazimika kuhama kwenye jengo la Summit Tower ili kupisha ofisi ya Mamlaka ya Kodi Mkoa wa Kodi Kariakoo zinazotakiwa kuhamia katika jengo hilo.

Awali, ofisi za TRA Mkoa wa Kodi Kariakoo zilikuwa katika jengo binafsi la 14 Rays Building lililoko Gerezani, Kariakoo.

Nayo ofisi ya Mkurugenzi wa TANROADS imelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa kuhama kwa ofisi za TANROADS ni utaratibu uliotolewa na serikali, hivyo wao wametekeleza agizo hilo kwa vitendo.

“Hatuna tunachoweza kuzungumza kuhusu kuhamishwa kwa ofisi za TANROADS katika jengo la Airtel, hilo ni agizo la serikali, ilitutaka tufanye hivyo, tumehama kwenye jengo hilo tangu Novemba Mosi,” imesema ofisa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Naye msimamizi wa jengo la Airtel aliyejitambulisha kwa jina moja la Ronald amelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa sasa wanalazimika kupunguza wafanyakazi katika kitengo cha usimamizi wa jengo baada ya TANROADS kuhamisha ofisi zao katika jengo hilo.

“Madhara lazima yaonekane, TANROADS walikuwa walipaji kodi wazuri, sasa walivyoondoka hatuwezi kuendelea na utaratibu wetu ule ule lazima tutafute utaratibu mwingine wa kuendesha shughuli zetu bila kuathirika zaidi,” amesema Ronald na kuongeza kuwa wako kwenye mchakato wa kutafuta wapangaji wapya japo anaeleza kuwa hali ya upatikanaji wa wapangaji wapya inasuasua.

Taarifa ambazo JAMHURI limezinasa zinaeleza kuwa ukiacha ofisi za Airtel, jengo hilo sasa halina mpangaji mwingine, kwani kabla ya TANROADS kuhama taasisi nyingine ya umma iliyokuwa imepanga kwenye jengo hilo nayo ilihamisha ofisi zake.

Serikali iliunda kikosi kazi cha kuratibu uhamaji wa ofisi za serikali kwenye majengo ya taasisi binafsi na tayari imeshakamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Hata hivyo, jitihada za JAMHURI kupata undani wa ripoti hiyo ziligonga mwamba baada ya wahusika kukwepa kulizungumzia suala hilo.

Ofisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja, amesema ni mapema kulizungumzia zoezi la kuratibu uhamaji wa taasisi na mashirika ya umma kwani ripoti bado inafanyiwa kazi kabla ya kuwekwa wazi.

“Suala hili bado ni nyeti, katibu mkuu bado anaishughulikia ripoti iliyowasilishwa kwake, kwa nini nyinyi mnataka kupata taarifa hizi kwa uharaka kiasi hicho?” alihoji baada ya JAMHURI kutaka kupata undani wa kilichobainishwa na kikosi kazi hicho.