Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Hofu imetanda kuhusu hatua ya uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, kutoa ekari 1,000 kati ya 5,900 za shamba la kampuni ya United Farming (UFC) lililopo Mlandizi mkoani Pwani  zilizofutwa na Rais John Magufuli.

Ardhi hiyo imemegwa ili iuzwe kwa mwekezaji, kampuni ya Kiluwa Steel Group inayomikiwa la Mohammed Kiluwa.

Hatua  hiyo inapingwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwa madai kuwa ni kinyume cha agizo la Rais Magufuli kutaka itolewe bure kwao.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Juni 17, mwaka jana, Kiluwa alimuomba Rais Magufuli kumuongezea ekari 1,000 za umiliki ili azitumie kwa uanzishwaji wa viwanda vitatu.

Viwanda hivyo ni vya vifaa za umeme, mabomba kwa ajili ya mradi wa usafirishaji mafuta kutoka Hoima nchini Uganda na gesi.

Ombi hilo lilikataliwa na Rais Magufuli kwa maelezo kwamba Kiluwa anapaswa kuzitumia kwa ufanisi ekari 50 alizonazo, kabla ya kuwasilisha ombi jipya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya JAMHURI, Rais Magufuli alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kumjulisha pindi Kiluwa atakapokidhi vigezo.

Chanzo chetu kinaeleza kuwa Septemba 28, mwaka jana, Ndikilo aliwashauri madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuidhinisha ombi la Kiluwa, ili wasipoteze kiasi cha fedha atakazolipia kwa ununuzi wa ardhi hiyo.

Ndikilo amekana kutumia ushawishi kwa madiwani hao na kusema akiwa mtumishi wa Serikali Kuu hana mamlaka ya kuingilia utendaji kazi wa Serikali za Mtaa.

Taarifa zaidi zinadai kuwa katika kile kinachoonekana kurahisisha upatikanaji wa ardhi hiyo, watumishi watano wa Serikali walifadhiliwa kwa ziara ya siku 14 kwenda China, Oktoba mwaka jana, ‘kutangaza’ fursa za uwekezaji kwenye eneo hilo.

Novemba 13, mwaka jana, baraza la madiwani linadaiwa kumuandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi likipendekeza ekari 1,000 kupewa kupewa kwa kampuni ya Kiluwa.

Pia inaelezwa kuwa wiki mbili baadaye, Kiluwa aliandika barua kwa wizara hiyo kuomba eneo hilo kwa ahadi ya kulipia Shilingi milioni moja kwa ekari.

Chanzo chetu kikaeleza kuwa Kiluwa alitanguliza malipo ya Shilingi  milioni 500 na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki atakapokabidhiwa hati.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa thamani halisi ya eneo hilo kwa mujibu wa makadirio ya wizara ni Shilingi 6,000,000.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi, amesema ombi la kutolewa ardhi hiyo kwa Kiluwa liliwasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Amesema shamba hilo ni miongoni mwa mengine yaliyopo ndani na nje ya mkoa wa Pwani yaliyofutiwa hati na Rais Magufuli na kurejeshwa kwa wakuu wa mikoa ili wayapangie matumizi.

“Kwa hiyo hapo ni suala la Mkuu wa Mkoa kujiongeza, ikiwa anawapata mwekezaji kwa eneo la ekari 1,000 kati ya 5,900 si makosa kwa maana bado linabaki la kuwagawia wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Lukuvi, maombi ya Kiluwa yalitolewa si kwa ajili yake kujenga viwanda, bali kuliandaa ili lifae kwa matumizi ya uwekezaji wa viwanda.

Amesema zaidi ya maombi yanayohusu kumegwa kwa ardhi hiyo na kuuziwa Kiluwa ambaye JAMHURI haikufanikiwa kumpata, wizara yake haijapokea maombi mengine kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuhusu wahitaji wengine wa eneo lililobaki.

Naye  Mhandisi Evarist Ndikilo, amesema maombi ya ekari hizo kupewa Kiluwa, yaliratibiwa na halmashauri ya wilaya ya Pwani na kwamba hapakuwa na malalamiko yaliyofikishwa ofisini kwake.

Amesema shutuma zinazotolewa dhidi yake kwamba alilishawishi baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya Pwani kuuza eneo hilo kwa Kiluwa hazina ukweli kwa vile hana mamlaka ya kuingilia utendaji na uamuzi wa Serikali za Mitaa.

“Sheria inatuambia sisi wa Serikali Kuu tunapotekeleza majukumu yetu tusiwazuie Serikali za Mitaa, isipokuwa tunapopata malalamiko tunaruhusiwa kuingilia kati ili kupata suluhu, kwa hilo sijapata malalamiko yoyote,” amesema.

Amesema kutokana na kutopokea malalamiko kuhusu mchakato wa kuliuza eneo hilo, ni ishara kwamba ‘mambo yalikuwa sawa’ na mchakato ulifuata sheria.

Mhandisi Ndikilo amesema suala la migogoro inayohusiana na ardhi mkoani Pwani hususani wilaya ya Kibaha haliepukiki kutokana na mafanikio ya kuvutia uwekezaji wa viwanda.

“Hivi sasa ukiwa na ekari 10 huku wewe ni bilionea, kwa maana ardhi imepanda ardhi na inatafutwa sana kwa uwekezaji wa viwanda,” amesema.

Mhandisi Ndikilo amesema undani wa mchakato unaohusiana na ardhi hiyo kukabidhiwa kwa Kiluwa, unapaswa kutolewa kwa kina na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Tatu Selemani.

JAMHURI iliwasiliana na Tatu kwa njia ya simu, akasema mjadala wa baraza la madiwani kuhusu hoja ya Kiluwa ‘ulifanyika zamani’ na kwamba hana taarifa ikiwa kuna mabadilikokwa vile yupo kikazi mjini Dodoma tangu Machi 7, mwaka huu.