Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizotia saini mkataba unaolenga kuongeza wigo wa kufanya
biashara miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kwa zaidi ya asilimia 14
iliyopo sasa miongoni mwao.
Mkataba huo ulitiwa saini mjini Kigali, Rwanda. Mkataba huo ulilenga kuzindua rasmi mkataba
wa biashara huria kwa bara la Afrika, mkataba ambao wachambuzi wa masuala ya uchumi
wanasema endapo ukitekelezwa vyema unaweza kuwa mkombozi wa kibiashara.
Mkataba huo umesainiwa baada ya kukamilika kwa mkutano wa kamati za wataalamu
zilizoshirikisha mawaziri wa biashara na mambo ya nje wa nchi husika.
Mbali na mkataba huo, wawakilishi wa nchi washirika wa maendeleo walisaini itifaki ya
utekelezaji wa makubaliano ambayo yanatoa uhuru wa makazi, kutembea, haki ya kuishi na
kufanya kazi popote miongoni mwa nchi hizo.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema mkataba huo ni muhimu katika kuimarisha
biashara barani Afrika, hasa kati ya nchi na nchi ambapo kwa sasa mataifa ya Afrika yanafanya
biashara chini ya asilimia 16 miongoni mwao.
Wanasema mkataba huu utasababisha kuazishwa pia kwa soko la pamoja, ambapo nchi na
nchi zitaweza kufanya biashara kwa uhuru huku wananchi wakiwa na uwezo wa kutoka nchi
moja kwenda nyingine bila ya vikwazo.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, tayari kuna harufu ya mgawanyiko miongoni mwa nchi
wanachama kutokana na kuna baadhi ya nchi hazikuridhia kutia saini makubaliano hayo, hali
inayoweza kuleta mgawanyiko.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Umoja wa Afrika, amesema mkataba huo hautarajiwi kuharibu uhusiano wa kibiashara
uliopo kati ya bara la Afrika na mataifa mengine.
Amesema kuimarisha biashara za ndani ya mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika hauna
maana ya kusitisha biashara na mataifa mengine, badala yake itaongeza ushindani
utakaozichochea kampuni zetu kujizatiti zaidi.
Amesema mkataba huu unatarajiwa kuongeza biashara ya ndani kwa bara la Afrika kwa
asilimia 52.3 kufikia mwaka 2020 na hii ni kwa mujibu wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa
Mataifa (UNECA).
Hata hivyo, baadhi ya viongozi hawakuhudhuria utiaji saini mkataba huo akiwamo Rais wa
Nigeria, Muhammadu Buhari, ambaye alisema nchi yake itatia saini baada ya kukutana na
wadau wengine wa biashara nchini mwake.
Mwingine ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliyemtuma Waziri wake wa mambo ya nje,
Sam Kutesa, kumuwakilisha, hatua ambayo hata hivyo imetafsiriwa tofauti na baadhi ya
wadadisi wa mambo.
Wanasema huenda ni kutokana na uhusiano uliolegalega baina ya mataifa hayo mawili.
Hiyo ni baada ya hivi karibuni kuingia kwenye mzozo wa kidiplomasia, huku kila mmoja
akimtuhumu mwenzake kwa kujaribu kuingilia uhuru wa nchi nyingine.
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, pia ni miongoni mwa viongozi ambao
hawakuhudhuria, na badala yake aliwakilishwa na Waziri wake wa Waziri wa Mambo ya Nchi
za Nje, Balozi Augustine Mahiga.
Wafanyabiashara kutoka Tanzania waliohudhuria sherehe hizo ni Mwenyekiti wa Makampuni ya
IPP, Reginald Mengi, na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakurugenzi Tanzania, Ally Mufuruki,
ambaye alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika mjadala huo wa uchumi na biashara.
Ni matarajio ya wengi kuwa mkataba huo utasababisha kuazishwa pia kwa soko la pamoja,
ambapo nchi na nchi zitaweza kufanya biashara kwa uhuru huku wananchi wakiwa na uwezo
wa kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Wakati hali ikiwa hivyo Afrika, takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinasema biashara ya bidhaa
nchi za nje imeongezeka mara tatu duniani katika miongo miwili iliyopita na kufikia zaidi ya dola
za Marekani bilioni 18, huku asilimia 25 ya kiwango hicho kikitoka nchi za kusini au
zinazoendelea.
Taarifa hizo zinaonesha biashara ya nje kati ya nchi na nchi ikiongozwa zaidi na nchi za Asia,
ikifuatiwa na zile za Amerika ya Kusini, ingawa biashara baina ya nchi za Afrika inaonekana
kushamiri katika kipindi hicho cha kuanzia mwaka 1995.
UNCTAD inasema nchi za Afrika zimenufaika kwa kiasi kikubwa na mabadilishano ya biashara
na nchi za Asia, mfano mwaka jana pekee, thamani ya biashara ya China kwa bara la Afrika
ilikuwa dola za Marekani milioni 970.
Nchi ya Misri imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizonufaika na kupanuka kwa biashara kati ya
Asia na Afrika, bidhaa zinazohusika tofauti na mafuta na gesi ni vifaa vya umeme na elektroniki.