Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Nchi za Jumuiya ya IGAD, kinasema kuwa eneo la Afrika Mashariki litapata hali ya ukame kuliko kawaida kati mwezi wa Januari na Machi 2025.
Katika utabiri wake uliotolewa Jumatatu, kinasema Ethiopia, Uganda, Rwanda, Kenya, Burundi, na Tanzania zitaathiriwa na hali ya ukame.
Kanda hiyo pia itarekodi joto zaidi kuliko kawaida wakati wa msimu wa Januari hadi Machi 2025. “Joto la kawaida huenda likarekodiwa katika maeneo machache ya kaskazini mwa Uganda na magharibi mwa Sudan,” imesema ripoti.
Kwa mujibu wa kituo hicho, katika kanda nzima, kusini magharibi mwa Tanzania na kusini magharibi mwa Uganda pekee ndizo zitakumbwa na hali ya mvua kuliko kawaida katika kipindi hicho, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia nchi katika ukanda huo.
Mataifa ya Pembe ya Afrika ni miongoni mwa yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi kwani ukame, mafuriko, na wadudu waharibifu huwa jambo la kawaida huku kukiwa na joto la juu la nyuzi joto 32, kulingana na kituo hicho.
Zaidi ya watu milioni 64 walihitaji msaada wa kibinadamu katika Pembe ya Afrika mwishoni mwa Novemba kutokana na migogoro na majanga ya hali ya hewa, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na IGAD walibainisha katika ripoti ya hivi karibuni.