Tangu baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili mwaka 1945, dunia imeshuhudia mivutano mikubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii. 

Mivutano hii inalenga kuathiri mlingano wa mamlaka ambayo yanazipa nchi, au makundi ya nchi nguvu ya kutawala dunia kupitia mambo mbalimbali kama uamuzi wa masuala makubwa, utawala wa rasilimali, nguvu za kiuchumi, nguvu za kijeshi na mambo mengine kadhaa.

Wakati zipo nchi chache ambazo zinafanya haya kwa lengo la kuhakikisha kuna kuwa na utawala wa pamoja wa masuala makubwa yanayoihusu au kuiathiri dunia, zipo nchi nyingine ambazo hufanya hivi kama mwamba ngoma. Nchi hizo hufanya mambo mengi kwa dhamira ya kujinyakulia, kujikusanyia au kujiongezea nguvu yake katika kuitawala dunia. Wanachotafuta wao ni kuona kuwa wao ndio wanakuwa na sauti katika masuala makubwa yote yanayohusu dunia, kwa masilahi yao binafsi.

Kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili kulifuatiwa na vita baridi ambapo Marekani kwa upande mmoja na Shirikisho la Nchi za Kisovieti (USSR) kwa upande mwingine zilijitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanaivuta nguvu ya kuitawala dunia upande wao. Kwa kuwa walijua wanahitaji marafiki ili kujiongezea nguvu hizo, nchi hizo zikashindana kutafuta wanaowaunga mkono wao.

USSR iliposambatarika na masilahi yake kushikwa kwa kiasi kikubwa na Urusi, mvutano huu uliendelea. Ingawa Marekani ilidhani kuwa kuvunjika kwa USSR kutaipa nguvu, hilo halikutokea kwa sababu Urusi iliendelea kushikilia nguvu yake hasa kwa kuzingatia kuwa wakati huo tayari ilikuwa imejikusanyia marafiki wa kutosha nyuma yake.

Lakini kwa upande wa pili yakaanza kuibuka mataifa mengine yakiwa na nguvu zinazoikaribia Marekani na kuinyima nchi hiyo nafasi ya kuwa mtawala wa dunia kwa uhakika.

Wakati haya yanatokea, Afrika, kwa kiasi kikubwa, ilijikuta ikiwa mtazamaji, ikivutwa huku na huko na wale wenye nguvu. Afrika ikagawanyika, wakiibuka marafiki wa pande hizo mbili. Baadhi ya watu kama vile Mwalimu Julius Nyerere wakaamua kuchukua msimamo wa kati, Tanzania ikawa nchi isiyofungamana na upande wowote, ingawa iliamua kufuata siasa za mrengo wa ujamaa unaohusishwa na Urusi na China.

Hali ya Afrika kutokuwa na msimamo wa nini cha kufanya katika kuitawala dunia bado inaendelea hadi hivi sasa, tena hali ikizidi kuwa mbaya. Pamoja na mataifa na njia mbalimbali zisizo halali kuzivuta nchi za Afrika upande wao, viongozi dhaifu, wenye uchu wa madaraka na wala rushwa wa Afrika, wamezidi kuzirahisishia nchi hizo kwa kukubali kujiuza kwao.

Tunashuhudia jinsi baadhi ya viongozi wa Afrika wanavyokubali kuuza nchi zao kwa vipande vya fedha, nyingi zikiingia katika mifuko binafsi ya viongozi. Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha mathalani sehemu kubwa ya fedha zinazotolewa kama misaada na wakati mwingine mikopo, zinatunisha akaunti za benki za baadhi ya viongozi wa Afrika zilizoko ughaibuni.

Kabla ya haya, mwandishi maarufu wa vitabu kutoka Zimbabwe, Bambisa Moyo, aliwahi kuonyesha kwenye kitabu chake kiitwacho Dead Aid, jinsi ambavyo misaada inavyotumika kuwanufaisha watu wachache, wakiwamo wanaotoa misaada hiyo, badala ya jamii maskini zinazotajwa kulengwa.

Afrika ina nafasi

Lakini, hali hiyo haimaanishi kuwa Afrika haiwezi kubadilisha hali ya mambo ya kujiweka katika nafasi ya kuitawala dunia, hata kama si kwa mambo yote. Ukubwa wake kijiografia, idadi ya watu, rasilimali nyingi ilizonazo ni baadhi ya vigezo ambavyo vinaipa Afrika nafasi ya kuingia kwenye utawala wa dunia. Lakini, hilo linawezekana kukiwa na uongozi bora, wenye maono na dhamira ya kulipeleka Bara la Afrika mbele na si kutunisha mifuko yao binafsi.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Institute for Security Studies (ISS) kwa kushirikiana na South Africa Institute of International Affairs (SAIIA), inaonyesha kuwa Afrika ina nafasi na ina uwezo mkubwa wa kujiinua kama mtawala wa dunia katika mambo mengi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Afrika ina vitu vingi sana vinavyohitajika kuifanya iwe kiongozi wa dunia. Kuna nchi ambazo hazina hata nusu ya kile ambacho Afrika inacho lakini kwa kutumia ipasavyo hicho kidogo walichonacho, wameweza kujiwekea nafasi kwenye meza ya watawala wa dunia na wao sasa wanasikilizwa kila linapotokea suala kubwa duniani linalohitaji uamuzi wa pamoja.

Pamoja na vigezo vilivyoanishwa hapo juu, lakini kuna mambo mengine ambayo yanaipa nguvu Afrika katika harakati za kujinyakulia madaraka ya kuitawala dunia. Mathalani, katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na mgawanyiko mkubwa baina ya nchi zenye nguvu, Afrika inaweza kuitumia hiyo kama fursa ya kujitutumua. Waswahili wanasema kuvuja kwa pakacha ndiyo nafuu ya mchukuzi.

Lakini katika mifumo rasmi Umoja wa Mataifa (UN) ndio unaoonekana kama kiranja mkuu duniani tangu mwaka 1945. Hivi sasa Umoja huo umo katika mbinyo mkubwa, huku nchi zikilenga kujiongezea madaraka kupitia Umoja huo. Hii nayo ni fursa kwa Afrika kutumia kile ilicho nacho nayo kujiongeza madaraka hayo.

Mathalani, Afrika inaweza kuanza harakati hizo kwa kuungana katika dai la kutaka kuwa na mwakilishi wa kudumu ambaye atakuwa na kura ya veto kama yalivyo mataifa mengine matano. Hapa la kuliangalia ni kuwa nchi itakwenda kama nchi lakini kimsingi itapaswa kuwakilisha masilahi ya bara zima.

Kama tulivyoonyesha awali, hili halitawezekana pasipo kuwa na uongozi bora, hasa katika kipindi hiki ambacho kinashuhudia viongozi wengi vibaraka.

Nafasi ya Afrika duniani

Ni dhahiri kuwa nafasi ya Afrika katika utawala wa dunia inapaswa kujadiliwa katika muktadha wa mabadiliko yanayotokea duniani. Kudharau yanayotokea kwingine duniani eti tu kwa sababu Afrika ina vigezo vingi vinavyoipa nafasi ya kuitawala dunia, hakutaleta matokeo chanya.

Afrika hivi sasa inaweza kuhesabika kama bara lenye nguvu lakini limewekwa pembeni katika masuala ya kidunia. Limebaki kuwa mtazamaji zaidi kuliko mchezaji, nafasi ambayo ndiyo inalistahili.

Wakati huo huo kuna haja pia ya kuangalia changamoto za ndani kama vile ukosefu wa ajira, umaskini, udhaifu wa uongozi, uwezo wa nchi kushiriki katika masuala ya kimataifa kwa ufanisi – kwa maana ya kutoa mawazo ambayo yatakubalika na kila mmoja – biashara baina ya mataifa ya Afrika na utandawazi.

Baadhi ya changamoto hizi zinasukumwa pia na utegemezi ambao Afrika inao kwa mataifa mengine. Na kwa kiasi kikubwa imeshaonyeshwa kuwa utegemezi huu ni wa mawazo zaidi kuliko mali. Afrika ina rasilimali nyingi kuliko nchi ambazo inazitegemea kwa misaada na ufadhili.

Kuna masuala makubwa matatu ambayo yanaweza kutumika kuelezea nguvu ya Afrika na udhaifu wake katika kuikamata dunia. Moja ni biashara ya ndani, pili ni idadi ya watu na tatu ni uhamaji wa watu.

Wachambuzi wanasema ili Afrika iweze kuwa na nguvu ya kuitawala dunia, inabidi iimarishe uchumi wake kwa kiasi kikubwa. Kuna mambo mengi yanayoweza kuimarisha uchumi na mojawapo ni biashara na hasa biashara baina ya nchi za Afrika zenyewe.

Katika hoja zake za kupinga utaratibu wa biashara baina ya nchi za Jumiuya ya Ulaya kwa upande mmoja na Afrika na Caribbean kwa upande wa pili, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alisisitiza sana umuhimu wa Afrika kukuza biashara ya ndani kabla haijajiingiza katika mikataba kama hiyo na mataifa mengine ya nje.

Mkapa anasema kuwa Afrika ina nafasi kubwa ya kujiendeleza kwa nchi zake kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe badala ya kuitumia mikataba ambayo ina dalili za unyonyaji.

Mkapa aliyasema haya miaka kadhaa iliyopita wakati huo akiwa madarakani. Lakini kwa bahati mbaya inaonekana nchi nyingi za Afrika hazijalichukulia suala hilo kwa uzito.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa biashara baina ya nchi za Afrika ni kati ya asilimia 12 na 14 ya kiwango cha biashara ambayo bara hilo inazifanya.

Ili kulitafutia ufumbuzi suala hili, Umoja wa Afrika ukaanzisha utaratibu mpya wa kufanya biashara ujulikanao kama African Continental Free Trade Agreement (AfCFTA), uliozinduliwa nchini Rwanda Machi 2018.

Inaelezwa kuwa iwapo mpango huu utatekelezwa kikamilifu, utawezesha kuanzishwa kwa masoko ya pamoja kwa ajili ya bidhaa, huduma na uwekezaji baina ya nchi za Afrika na hatimaye kuruhusu watu barani Afrika kwenda popote kufanya biashara na uwekezaji bila vikwazo vyovyote.

Pamoja na vikwazo, wataalamu wanabainisha kuwa mpango huu utaiwezesha Afrika kujikwamua kibiashara. Kile kilio cha wazalishaji barani Afrika kukosa soko la bidhaa zao kitakwisha kwa sababu idadi ya watu inalifanya Bara la Afrka kuwa soko kubwa sana.

Ikumbukwe kuwa China imefanikiwa kukuza biashara yake kwa kutumia wingi wa watu wake.

Idadi ya watu ni kigezo cha pili cha kuiwezesha Afrika kukua kiuchumi. Demografia inaonyesha kuwa watu wengi katika Bara la Afrika ni vijana. Hawa ndio nguvu kazi ya uzalishaji na hilo litawaongezea uwezo wa kununua kwa sababu watakuwa na vipato. Kwa mujibu wa UN, idadi ya watu Afrika ni bilioni 1.3.

Lakini, takriban asilimia 37 ya watu hawa, sawa na watu milioni 410 ni maskini ambao kipato chao ni chini ya dola 1.9 kwa siku. Lakini ukumbuke kuwa iwapo Afrika itakubali kuongeza biashara za ndani baina yake, uzalishaji viwandani utaongezeka na hilo linaamanisha kukua kwa ajira na hatimaye uwezo wa wananchi kiuchumi.

Idadi ya vijana (miaka 15-29) Afrika ambayo ni asilimia 60 ya watu wote inatarajiwa kufikia watu milioni 830 ifikapo 2050.

Iwapo Afrika itamudu kuwatumia vijana hawa vizuri, ina nafasi kubwa sana ya kuendelea kiuchumi na kijamii katika miongo michache ijayo. Lakini kunahitajika mipango kabambe ya kuhakikisha nguvu kazi hii inatumika kuzalisha na si kukaa tu na kuwa tegemezi.

Kuhusu suala la watu kukimbilia Ulaya, ni dhahiri kuwa linaliathiri Bara la Afrika. Lakini, wengi wa wahamaji hawa hukimbilia Ulaya kwa lengo la kwenda kutafuta ajira na vipato. Iwapo Afrika itafanya mapinduzi ya biashara, uhamaji huu utakoma wenyewe kwa sababu Waafrika watapata nyumbani kile ambacho wanakwenda kukitafuta nje ya nchi zao.

Uwezo wa Afrika

Moja, ni vigezo vya kupima uwezo wa nchi za Afrika katika uzalishaji na matumizi ya nishati kulinganisha na uzalishaji na matumizi ya nishati duniani.

Kipimo kikubwa cha jambo hili kinaitwa kitaalamu kama Global Powers Index (GPI), ambayo hukokotolewa kwa kuangalia vigezo vitano. Nchi ambazo GPI yake inafikia asilimia tatu na zaidi zinahesabiwa kuwa zenye uzalishaji na matumizi makubwa ya nishati.

Takwimu zilizopo zinaonyesha Marekani ina asilimia 22, China 14.5, Japan 5.2, Ujerumani 4.9, Ufaransa 4.7 na Uingereza 4.1%. Nchi zinazoendelea kama Urusi, India na Brazil zina asilimia 4, 3.4 na 2.17 mtawalia.

Kwa upande mwingine, GPI ya Afrika inaonyesha upungufu mkubwa sana ukilinganisha na wastani wa matumizi ya nishati katika maeneo mengine duniani. Nchi nyingi za Afrika zina matumizi madogo sana ya nishati, jambo linaloakisi uzalishaji mdogo na changamoto zote kuhusiana na hilo.

Afrika Kusini, nchi yenye uchumi mkubwa katika Bara la Arika, ina GPI ya asilimia 0.38. Nigeria na Algeria zinafuatia kwa karibu zikiwa na GPI za asilimia 0.32 na 0.35 mtawalia. Pengo kubwa katika GPI kati ya nchi za Afrika na nyingine duniani linaonyesha umuhimu wa Afrika kuungana ili kuongeza uwezo wake wa matumizi ya rasilimali zake. Hili litaongeza uzalishaji na kutatua changamoto nyingine zote kuhusiana na hilo.

Sauti Umoja wa Mataifa

Wakati UN inaanzishwa mwaka 1945 baada ya Vita Kuu ya Pili, nchi chache sana za Afrika zilikuwa huru. Leo hii, kati ya wanachama 193 wa UN, 54 ni kutoka Afrika, likiwa ni kundi kubwa ndani ya umoja huo kuliko kundi jingine lolote, likiwakilisha aslimia 28 ya wanachama wote.

Kwa maana hiyo, kwa umoja wao nchi za Afrika zinapaswa kuwa na sauti ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo tofauti na Baraza la Usalama, hakuna nchi yenye kura ya veto. Lakini hali haiko hivyo.

Aidha, nchi tatu za Afrika ni kati ya wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hii ni nafasi ya uwakilishi ambayo nchi huishikilia kwa kipindi cha miaka miwili. Inatarajiwa kuwa wawakilishi wa wenzao. Hadi mwishoni mwa mwaka jana Côte d’Ivoire, Guinea ya Ikweta na Afrika Kusini ndizo zilikuwa zinashikilia nafasi hii. Mwaka huu inatarajiwa kuwa Tunisia na Ghana zitaungana na Afrika Kusini baada ya zile nchi mbili nyingine kumaliza muda wao.

Haya ndiyo baadhi ya masuala ambayo yanaipa fursa Afrika kuwa na nguvu katika mambo mengi duniani. Kwa bahati mbaya sana, hadi sasa inaonekana kana kwamba bado nchi nyingi za Afrika hazijatambua nafasi ilizonazo katika suala hili kwa hiyo kulifanya Bara zima la Afrika kubakia nyuma.