Mwasisi wa taaluma ya ‘Public relation Arthur Page’ alipata kuandika haya; “Unaweza kutumia miaka 20 kujenga haiba yako mbele ya jamii lakini sekunde tano tu zinatosha kukiharibu kile ulichokijenga kwa miaka 20’’.
Haiba iliyojengwa na wapigania uhuru wa bara la Afrika imepotea. Imepotea kwa sababu Afrika sasa inapata viongozi wenye uroho wa madaraka. Afrika limekuwa bara la visa na mikasa.
Leo hii katika bara la Afrika huwezi kuamka asubuhi ukasoma habari ya uvumbuzi wala maendeleo badala yake unaamka unakutana na ufisadi, wizi, hofu na maradhi, vita njaa na ubaguzi. Inasikitisha sana.
Bara la Afrika limesimama. Bara la Afrika limezama. Bara la Afrika limedumaa. Bara la Afrika limezimia. Bara la Afrika halitembei kiuchumi, kidemokrasia, kiteknolojia. Bara la Afrika linaelekea kupotea katika uso wa dunia.
Mkoloni hajaondoka Afrika! Bado yupo. Iliondoka tu ngozi nyeupe, lakini ukoloni ulibaki. Ipo ngozi nyeusi inaendeleza ukoloni uliokuwa umeasisiwa na ngozi nyeupe. Tarehe 18/4/1993 Mwandishi Paul Johnson wa gazeti la ‘Sunday New York Times’ la Marekani aliandika hivi; “Ukoloni umerudi na siyo mbalimbali karibu sana, nchi zingine haziwezi kabisa kujiongoza zenyewe nchi masikini za kusini mwa Sahara zitalazimika kujikabidhi kwa wakoloni walio watawala kwa kipindi cha kati ya miaka 50 hadi 100’’.
Kutokana na maoni na mtazamo wa mwandishi huyu mambo aliyoyazungumza na kuyatabiri yameanza kutimia kwa kiasi kikubwa huku wakoloni weusi ambao ni watawala wametoa fursa na mwanya wa kushirikiana na wakoloni wa zamani katika kuwahujumu waafrika.
Bara la Afrika halina viongozi, lina watawala, lina wakoloni. Watawala hawa wamejigeuza kuwa miungu watu. Wanataka wanyenyekewe. Wanataka waabudiwe. Wanataka kusifiwa. Hawataki kuondoka madarakani kwa amani. Wanataka watawale milele. Wamelewa madaraka. Kadri ya Emerich Edward Dalberg ni kwamba “Madaraka hulevya na madaraka makubwa hulevya zaidi.”
Nachelea kusema, ipo siku bara la Afrika litakuwa bara la kujihami. Waafrika watajihami kutafuta uhuru wa kutumia rasirimali zao. Watawala wa kiafrika watambue kwamba Waafrika hawakuutafuta uhuru kwa ajili ya kuwanyenyekea wao, bali waliutafuta uhuru ili waondokane na kongwa la ukoloni lililokuwa limewafunga.
Leo hii Afrika nzima inateseka, ina mahangaiko, manyanyaso, vifo vya watoto, vifo vya akina mama, vita, ujinga na maradhi wa sababu ya hawa watawala wasio na maono kwa watu wao. Leo hii Afrika nzima kuna mpasuko. Mpasuko wa kidini. Mpasuko wa vipato. Mkoloni mweusi ni nani?. Mkoloni mweusi ni mwafrika anayeamua kumtesa mwafrika mwenzake kwa masilahi yake. Machafuko yanayotokea barani Afrika yanayokana na matumizi mabaya ya viongozi waliopo.
Askofu Dag Heward Mills Katika kitabu chake cha Viongozi na uaminifu anasema yafuatayo; “Tatizo la Afrika ni uongozi. Afrika inatatizwa na viongozi wabaya, kuwa na viongozi wabaya ni sawa na kumkaribisha shetani kuwa rafiki yako. Nchi nyingi za Afrika zinapata viongozi ambao wanaiba rasirimali za mataifa yao. Viongozi wa nchi za Afrika wana utajiri binafsi kuliko wa nchi wanazoziongoza.”
Huo ndio ukweli. Viongozi wa Afrika ni watalii! Wawapo madaraka ziara haziishi. Hawakai maofisini, hawapangi maendeleo ya mataifa yao, wanapangiwa na wahisani kutoka nje. Sijui kama Afrika tutatoka. Ni vigumu kuamini.
Prof. Ali Mazrui katika andiko lake la ‘The Liberal Revival Privisation and Market; Africa Cultural Contradiction’, anatoa mtazamo wake namna mwafrika asivyoweza kuumiliki uchumi wake anasema, “Mwafrika hawezi kuongoza na kuendeleza uchumi wake, bali hutawaliwa na ufahari na majigambo badala ya kiu ya kupata faida.
Tatizo la Mwafrika sio jinsi ya kubinafsisha uchumi na kuchochea uchu wa kupata, bali tatizo ni jinsi ya kudhibiti na kupiga vita jeuri ya ufahari, majivuno na majigambo ya kiuzawa katika kutawala uchumi.’’
Mtazamo wa Prof. Ali haupo mbali sana na kejeli ambayo ilipata kutolewa na Rais wa kwanza wa Senegali Leopold Sedar Senghor kupitia kitabu chake cha ‘La Negritude yaani Uafrika’, Anasema, “Mtu mweusi siku zote hatumii akili yake ili aweze kuendesha maisha yake yeye mwenyewe. Mwafrika anatumia sana mdomo, tumbo, macho, pua, ulimi na sehemu zingine za mwili ili kuweza kutatua matatizo yake.”
Kauli za wasomi hawa ni za kuudhalilisha ‘Uafrika’, lakini kwa yale yanayotendwa na baadhi ya viongozi wa kiafrika kauli hizi zinaweza kuwa na ukweli ndani yake. Kama alivyopata kusema Mhubiri wa kimataifa kutoka Ghana Dr. Mensa Otabili, “Ni Afrika peke yake ambapo watu hupigwa na kuuwawa wakati wa maandamano ya Amani.”
Sikosei kusema, Afrika ni bara la viroja. Ukitaka kila kitu nenda Afrika. Udikiteta Afrika, ujinga Afrika, uporaji wa haki za binadamu Afrika, Katiba mbovu Afrika, umasikini Afrika, ukabila Afrika, uongozi wa kindugu Afrika, uroho wa madaraka Afrika, vita vya wenyewe kwa wenyewe Afrika. Dhambi saba alizotaja Mahtma Gandh, mwanamapinduzi wa India zinapatikana barani Afrika, dhambi hizo ni, ‘Kupata utajiri bila kazi, anasa bila dhamiri, maarifa bila tabia, biashara bila maadili, sayansi bila utu, dini bila sadaka na siasa bila kanuni’.
Akihubiri katika mkesha wa krismasi wa mwaka 2014, Askofu wa jimbo katoliki la Iringa Askofu Tarcius Ngalekumtwa alisema, “Leo tunao viongozi wanaojilikimbizia mali, kuliko hata wanavyoweza kuzitumia, mtu unakuwa na mamilioni ya fedha ambayo unaweza ukafa hata hujayatumia. Huu si uongozi, hata simba hajilikimbizii nyama ya ziada kuliko anayoihitaji.” Hii ni aibu, Viongozi wetu wanapenda ufahari sana kuliko uwajibikaji na ubunifu wa mataifa yao. Tarehe 12/3/2012 rafiki yangu mmoja alinitumia ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi, ujumbe ule ulikuwa unasomeka hivi, “Hivi watanzania tunaishi makaburini au? Kwa nini viongozi wetu wanaweka fedha Uswisi, wanatibiwa India, Afrika kusini, Uingereza na Marekani. Wanajenga London, wanawekeza Marekani, wanafanya manunuzi Dubai, likizo wanaenda Paris- Ufaransa.
Kuungama wanaenda Israeli au Saudi Arabia. Kitu cha ajabu ni kwamba wakifa wanazikwa Tanzania. Hivi Tanzania ni makaburini? alihoji huyu rafikiki yangu. Ujumbe huu ulinifanya nitafakaria mambo mengi sana, lakini nilibaini kwamba viongozi wetu wanapenda safari kuliko uwajibikaji. Sifahamu kama wanaposafiri wanaenda kuwekwa kwenye mabanda ya maonyesho?.
Hao ndio viongozi wetu wakitibiwa kwenye hospitali zetu hizi za uswahilini wanaona kwamba wamejishushia heshima, hawataki kupanga foleni ya kwenda kuchukua dawa. Watoto wao wakisoma kwenye hizi shule zetu za yeboyebo wanaona ni dhambi isiyosameheka. Wanaenda kutibiwa nje ya taifa letu kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii. Wanawekeza miradi mikubwa nje ya taifa letu kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii
Ninaungana na Prof. Patrick Lumumba kukosoa kwamba, “Viongozi wetu wa Afrika wanamiliki Ipad ambazo hawajui hata kuzitumia na wakati huo mabinti wetu wanakosa hata pesa ya kununulia pedi. Wanajenga majumba ya kifahari kila kona ya dunia wasiyoweza kuishimo. Wananunua vyakula vya kila aina na wakati hawana hamu ya kuvila. Wananunua vitanda vya dhahabu wasivyoweza kuvilalia.”
Afrika imefanywa kama kitega uchumi cha kuendeleza nchi za ughaibuni. Afrika imefanywa kama benki ya kukopesha mataifa ya ughaibuni. Rasirimali za Afrika hazina mwenyewe. Ajabu ni kwamba Viongozi wa Afrika wanawatosa wazawa wanawakumbatia wale wenye nywele nyeupe. Aibu kubwa hii, enyi viongozi wa Afrika historia itawahukumu.
Nachelea kusema ‘Hakuna lenye mwanzo lisilokuwa na mwisho wake’. Mark Twain amepata kusema; “Andika lakini uwe tayari kulaumiwa”. Mimi niko tayari kulaumiwa lakini hisia zangu, manung’uniko yangu yaufikie ulimwengu na viongozi wanaotuongoza. Niko tayari kuushuhudia ukweli kupitia kalamu yangu. Ukweli unabaki palepale kwamba, Waafrika wanateseka!. “Siku inakuja ambapo watu wanyonge na wanaonyanyaswa watachagua kifo kuliko fedheha, Na ole wao watakaoina siku hiyo. Na ole wao wale watakayoifanya siku hiyo isiepukike. Natumaini na kusali kwa Mwenyezi Mungu kuwa siku hiyo kamwe haitofika.’’ Maneno haya yalitamkwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Januari, 1966. Yanapatikana katika kitabu cha Haroub Othman kinachoitwa; ‘Reflection on Leadership in Africa Forty years after Independence Essay in Honour of Mwalimu Nyerere on the occasion of his 75th birthday’.
Nachelea kusema kama viongozi hawatabadilika ipo siku uvumilivu utawashinda Waafrika. Watapaza sauti zao, dunia itaona hisia zao na Mungu atasikiliza kilio chao. Na hapo wataupokea uhuru wa kutumia rasilimali zao kwa usawa. Gazeti la Mail la Julai, 15 Mwaka 1998 lilimnukuu Mark Dodd akisema; “Watanzania ni Wanyonyaji wakubwa kupindukia wa Watanzania wenzao, kuliko mnyonyaji mwingine yeyote duniani.”
Mwandishi Nkwabi Ng’wanakilala kupitia kitabu chake cha Unyayo wa Julius Nyerere, Uk wa 5, Ameonya viongozi wa Afrika kwa kusema; “Afrika ni nani asiyekufahamu?…Kama jina hili litafifia usitafute mchawi ni wewe Afrika. Umekuwa mkarimu kiasi cha kuwasahau watoto wako. Umeshindwa kuwajibika ipasavyo. Unahudumia waporaji. Huyo mgeni atakusaidia nini?.’’ Watanzania na Waafrika tunakwenda wapi? Viongozi wa Afrika wako kinyume na viongozi wa mabara mengine, wakati viongozi wa mabara mengine wakijitahidi kuwainua wananchi wao kielimu na kiuchumu Afrika wanang’ang’ana kuwaibia wananchi wanaowangoza rasilimali zao.
0757852377