Mei, 1954 majeshi ya kikoloni ya Ufaransa yalipata pigo kali kutoka kwa wapiganaji wa Vietnam katika mapambano kwenye mji wa Dien Bien Phu.
Yapo matukio ambayo hubadilisha mkondo wa historia ya ulimwengu na moja ya matukio haya ni mapambano haya ya Bien Dien Phu. Ni muhimu kukumbuka tukio hili kwa sababu ni somo la jinsi gani dhamira kubwa ya wanyonge inaweza kuleta matokeo ambayo kwa kawaida yangeonekana ni ndoto.
Mapambano ya kivita dhidi ya Ufaransa na Vietnam wakati huo yanaweza kulinganishwa na mapambano kati ya bingwa wa ligi na timu inayoshika mkia. Ni mcheza kamari tu anayeweza kuamini matokeo ya ushindi dhidi ya bingwa.
Ufaransa ya wakati huo lilikuwa taifa kubwa lenye uwezo mkubwa wa kijeshi, kiuchumi na viwanda. Isitoshe, Ufaransa ilitawala eneo lililofikia ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya milioni 11 ikijumuisha makoloni katika bara la Afrika, Asia, na Visiwa vya Pacific.
Vietnam ilikuwa ka-nchi kadogo chini ya mfumo wa kikabaila, wamiliki wachache wa ardhi walioitumia kuwatumikisha wengi kwa faida yao; nchi yenye watu wachache, wenye silaha duni, isiyo na viwanda na ambayo kwa hali yoyote isingekaribia kulinganishwa na Ufaransa.
Kilichotokea kwenye mapambano hayo ni sawa na timu ya Biashara United kuifunga timu ya Simba. Majeshi ya Ufaransa, mtawala wa eneo lililoitwa French Indochina, yaliweka mtego uliokusudia kuvuta vikosi vya Viet Minh na kuvishambulia kwa silaha nzito. Katika mapambano makali yaliyodumu karibu miezi miwili vikosi vya Ufaransa vilisalimu amri na kusababisha kiongozi wa vikosi hivyo kujiua.
Haukuwa ushindi rahisi. Wakati wanajeshi 1,600 wa Ufaransa waliuawa na 4,800 kujeruhiwa ni wapiganaji 7,900 wa vikosi vya Viet Minh waliouawa na 15,000 kujeruhiwa.
Vita si jambo zuri hata kidogo, lakini ni tukio linaloweza kuleta matokeo chanya. Matokeo ya kisiasa ya kushindwa kwa Ufaransa yalikuwa makubaliano ya Mkutano wa Geneva wa Julai 1954 na kusambaratika kwa utawala wa Ufaransa huko French Indochina na kuundwa kwa mataifa ya Vietnam ya Kaskazini, Vietnam ya Kusini, Ufalme wa Laos, na Ufalme wa Cambodia.
Sehemu kubwa ya watu duniani waliokuwapo nyakati hizo walikuwa chini ya tawala za kikoloni za Ufaransa na Uingereza, pamoja na mataifa mengine ya Ulaya na Marekani. Kama ilijengeka imani kuwa haiwezekani kwa watu wanyonge kushinda nguvu za kijeshi za tawala za kikoloni, basi ushindi wa Dien Bien Phu uliamsha ari kuwa ushindi huo unawezekana.
Ukoloni ulikuwa mfumo wa kibaguzi ambao msingi wake mkubwa ulikuwa kuvunja imani yoyote ya watawaliwa kuwa wana uwezo wa kujitawala wenyewe. Ushindi ule ulibomoa imani hiyo siyo kwa watu wa Vietnam pekee, bali kwa wengine barani Asia, Afrika na kwingineko.
Vita dhidi ya ukoloni haikwisha baada ya nchi nyingi za Asia, Afrika, na kwingineko kupata uhuru. Hoja zile zile za kibaguzi ambazo zilitetea uwepo wa ukoloni bado zinashawishi, hadi hii leo, uamuzi mwingi wa ushirikiano uliopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini duniani. Changamoto iliyopo sasa ni kuwa hoja zenyewe haziko dhahiri sana na hazitajwi wazi wazi kama zamani.
Ni jambo la kawaida kwamba mawazo yanayojenga mifumo yetu ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa ni mawazo ambayo yanashawishiwa na mawazo kutoka nje ya Bara la Afrika. Tangu wageni wa kwanza kutembelea Bara la Afrika imewekwa jitihada kubwa ya kudhalilisha mifumo iliyoongoza jamii zetu na tumeburuzwa kwenye fikra kuwa ni mifumo ile ya wageni tu ndiyo bora.
Ipo misamiati inayoingia kwenye mijadala ya mipango na miradi ambayo inatufundisha, bila kusema wazi wazi, kuwa mipango inayofaa hutoka nje. Mila potofu hazipo Ulaya wala Marekani, huwa zipo Afrika tu. Kwamba zipo mila zisizofaa siyo suala la kutunga, lakini kuweka uzito kwenye mila kama kikwazo cha maendeleo ni njia nzuri ya kutufanya kuhoji kila jambo ambalo linatokana na mila – zuri au baya. Kibaya zaidi ni kuwa tunarithishana imani kuwa hatuna zuri zaidi ya yale tunayoyapokea kutoka nje.
Na kwa kufanya hivyo tunajenga rika la watu wasioyojiamini kwa lolote zaidi ya kuelekezwa na kuiga yale yanayotokana na jamii nyingine.
Tunachokikosa sasa kwa muda mrefu ni ushindi wa aina ya ile ya Dien Bien Phu katika nyanja mbalimbali zinazoongoza maendeleo yetu, lakini hasa kwenye mawazo yanayosimamia maendeleo hayo.
Tunawapokea wafadhili na wawekezaji kwa unyenyekevu halafu wanatumia rasilimali zetu kutuletea ‘maendeleo’; kazi ambayo tunaweza kuifanya wenyewe kwa kutumia vizuri rasilimali hizo hizo.
Tunapaswa kuweka jitihada kukumbusha vijana wanaoelekea kukamata majukumu ya uongozi kwenye siasa, biashara, sayansi, na masuala yote mengine yanayosimamia jamii kwamba ufanisi na mafanikio hauna uhusiano wowote na kwenye bara gani umezaliwa, au rangi ya ngozi yako.
Ni uongo tu uliokithiri unaoongozwa na tamaa unaodidimiza ari ya ujasiri na ufanisi na kuibua woga na kutojiamini miongoni mwetu. Inahitaji kukumbushana kila mara na kuamini kuwa binadamu wote ni sawa kama tunavyojifunza kwenye matokeo ya mapambano ya Dien Bien Phu.