Nawasalimu wasomaji wote, ninawapongeza na kuwashukuru wote ambao wamekuwa wakiwasiliana nami. Mbarikiwe. Itakumbukwa kuwa huko nyuma nimepata kuandika makala iliyokuwa na kichwa, ‘Naiona Afrika ikiinuka tena’.
Katika makala yale nilieleza kwa sehemu namna Afrika ilivyoanza kuzinduka, na leo katika makala haya (na zitakazofuata kila nitakapopata wasaa wa kuchambua uchumi wa Afrika), nitaeleza namna Afrika ilivyoanza kutembea katika mstari wa mafanikio ya kiuchumi, kijeshi na kijamii pasipo kuwategemea akina “bwana mkubwa” kutoka ng’ambo.
Nauona umuhimu wa kuyachambua haya ili kwamba Waafrika wote tujitambue, tujikubali, kisha tujenge ari ya matumaini na fikra za ushindi sasa na kwa vizazi vijavyo. Tumejikunyata vya kutosha, sasa ni wakati wetu kutamba duniani!
Kwa miaka mingi sasa kila neno Afrika linapotajwa huwa linaunganishwa na migogoro ya kivita, mabaa ya njaa na magonjwa, umbumbumbu na ulafi wa watawala, umaskini na ufukara uliopindukia, mikosi, laana, kuonewa pamoja na harufu ya jehanamu!
Waafrika wengi tulijiona katika picha hiyo (na bado wengi wanajiona hivyo), lakini vile vile dunia imekuwa ikiiona Afrika kwa jinsi hiyo hiyo. Mengi yameandikwa sana kuhusu Afrika, mengi yamesemwa, mikakati mingi kutoka nje ya Afrika imekuwa ikifanyika kwa madai ya kuliokoa bara hili ambalo wakati fulani Wazungu waliliita kuwa ni bara la giza.
Wanazuoni mahiri kutoka duniani waliibuka na nadharia na falsafa kedekede zinazoonesha kuwa Afrika imefika katika hali mbaya kwa ajili ya ukoloni. Namkumbuka Walter Roodney namna alivyoandika kitabu kiitwacho, ‘How Europe Underdeveloped Africa’. Katika kitabu hicho ameeleza namna Ulaya ilivyocheza karata zake kuimaliza Afrika. Wengine wakaja na mwanya wa kisayansi wakieleza kibaiolojia.
Hawa wakadai kuwa Waafrika wana genetiki zilizoumbwa kushindwa (unsuccessful genetic codes). Hawa wanamaanisha kuwa umaskini na matatizo ya Waafrika ni matokeo ya kukosewa kuumbwa! Yaani Waafrika waliumbwa kushindwa (programmed to fail). Haiishii hapo; kwani wapo wachambuzi wa Biblia ambao husema kuwa Waafrika ni kizazi kilicholaaniwa na Mungu ndiyo maana, kila kitu hakifanikiwi ndani ya Afrika!
Hizo ni sababu chache kati ya nyingi zilizoelezwa na kuendelea kuaminika kwa miaka mingi. Kimsingi kila nadharia, falsafa na sababu inayoelezwa kuhusu kukwama kwa Afrika, inaonekana kuwa na usadifu fulani wenye mashiko; kiasi kwamba kila nadharia imejipatia wafuasi wengi.
Bahati mbaya ni kuwa nadharia na falsafa zote zinaua uwezo wa Mwafrika kujikwamua, na zinaendelea kuwafanya Waafrika waamini kuwa wao si sehemu ya wanadamu kamili katika hii dunia.
Hata hivyo, tunaoifuatilia historia ya Afrika kwa macho ya uchanya, tunaona sababu za Afrika kupita ilikopitia lakini pia tunaona Afrika inakoelekea. Ni kweli kuwa Afrika imepita katika mkondo wa vita, umaskini, majanga, kutengwa, kuonewa na kudharauliwa; lakini wasaa wa Afrika kujikwamua umewadia, nao unaendelea kutokea.
Afrika inaumbika upya! Ninaposema Afrika inaumbika upya, ni vema tujikumbushe historia ya nguvu za mataifa katika dunia. Kimsingi mataifa tajiri na yenye nguvu yamekuwa yakipanda na kushuka huku nafasi zao zikichukuliwa na mataifa yanayoibuka. Ukiyachunguza mataifa ambayo huibuka na kuyapiku yale mataifa makubwa; mara zote huwa yametoka ama yamepitia kwenye matatizo makubwa, ikiwamo umaskini mkubwa, vita ya wenyewe kwa wenyewe, kuonewa na mengine niliyoyataja hapo juu.
Tunapoitazama China tunaona kuwa kwa miaka zaidi ya 20 ilikuwa ikielea katika Ujamaa ulioonekana kama umepoteza mwelekeo, lakini baada ya hapo imeibuka kwa kasi kwamba sasa inatishia nafasi ya Marekani kiuchumi na kijeshi.
India nayo kwa miaka mingi ilihaha kwa umaskini mkubwa lakini ndani ya miaka minne hadi 10 neema ikaitembelea na sasa uchumi wake unastawi kwa kasi mno. Hata Brazil huko zamani ilikuwa ikiogelea katika lindi la umaskini lakini kwa sasa ni moja ya nchi zinazopanda kwa kasi katika ustawi wa viwanda duniani.
Zamani yale mataifa saba tajiri (Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan) yalijiona kama miungu mtu duniani, yakajiandikia haki ya kuitawala dunia katika kila jambo – kuanzia uchumi, nguvu za kijeshi na kijamii.
Siku zilivyokuwa zinaenda yakabaini kuwa wanachoamini ni “kujilisha upepo” kwani kuna mataifa ambayo yanapanda kiasi kwamba ustawi wa uchumi wake ni mzuri kuliko wao wanaojiita G7. Hapana shaka kwamba nchi hizi zilikuwa zikijionea haya kujiita tajiri wa matajiri ilhali kuna matajiri wakubwa kupita wao.
Baada ya mvutano na mjadala mkubwa; kwa shingo upande yakasalimu kujibadilisha jina kutoka G-7 hadi G-8 ambapo walilazimika kuliongeza taifa la Urusi. Haikuishia hapo kwani mataifa haya yakabaini kuwa matatizo ya kiuchumi duniani hayawezi kumalizwa na wao pekee, hivyo wakaona ni wasaa wa kutengeneza umoja utakaoyatambua mataifa mengine ambayo yanazidi kuongezeka kila kona. Hii ikawa ndiyo sababu ya dunia kupata kinachoitwa G-20.
Ukiacha ngazi ya uchumi wa mataifa, tunaporudi katika uchumi wa mtu mmoja mmoja (micro-economics) tunaona pia mambo yakibadilika. Kwa miaka nenda rudi Taifa la Marekani ndilo limekuwa likitoa binadamu tajiri kuliko wote duniani. Lakini miaka ya karibuni binadamu tajiri kuliko wote ametokea Taifa la Mexico; taifa ambalo miaka kadhaa nyuma lilikuwa kwenye orodha ya nchi za Dunia ya Tatu.
Nini maana ya mambo haya? Ni hivi: Mambo yanabadilika na yanabadilika kwa kasi sana. Taifa lenye nguvu leo haimaanishi kuwa litakuwa na nguvu milele. Matajiri kwa sasa wanapatikana kutoka nchi zote – za Dunia ya Kwanza na ya tatu.
Pia ukweli ni kuwa mataifa mengi yanaanguka moja kwa moja na nafasi zao zinazidi kuchukuliwa na yale mataifa ambayo yalidhaniwa kuwa ni madogo na manyonge kabisa. Mataifa makubwa sasa yanatoa jasho!
Haya mabadiliko yanayotokea duniani hayajaliacha nyuma bara la Afrika. Mwanga wa matumaini unazidi kuonekana Afrika. Afrika imeanza kujitambua, kuamka, kusimama na kimsingi itasimama moja kwa moja na kuitawala dunia kiuchumi, kijeshi na kijamii.
Hili jambo si “habari ya maono ya rohoni” isipokuwa ni mtiririko (trends) na mahesabu yajayo (forecast) kutokana na yale yaliyotokea Afrika, yanayoendelea kutokea na Afrika inavyojipachika (reposition) katika “mdundo wa mabadiliko”.
Kabla ya mwaka 1950, karibu Afrika nzima ilikuwa ikitawaliwa na wakoloni isipokuwa nchi chache tu. Baada ya mwaka 1950 Bara la Afrika lilipatwa na mfumuko wa ukombozi, ambapo makumi ya nchi zilianza kujipatia Uhuru wake miaka ya 1960 hadi 1980.
Ifahamike kuwa kilichofanya nchi nyingi za Ulaya ziachie makoloni ni kuyumba kwa uchumi wao kiasi kwamba wakawa hawana tena jeuri ya kuendesa makoloni hasa baada ya Vita ya Pili ya Dunia. Mataifa haya ni kwamba yalilazimika kuyaachia makoloni kwa shingo upande.
Msomaji napenda ushike hapa: Afrika haikupata Uhuru kwa bahati mbaya ama kwa hiari ya walioitawala; isipokuwa ilipata Uhuru kwa sababu ya kuyumba kwa uchumi wa walioitawala. Kisosholojia na kiimani tunasema Uhuru wa Afrika ulikuwa kama ujio wa nguvu za Mungu kwa Afrika baada ya kutawaliwa kwa miongo mingi. (First God’s Visitation to Africa).
Bahati mbaya ninaweza kusema kwamba Afrika iliuchezea ujio wa mara ya kwanza wa Mungu! Hii ni kwa sababu baada ya nchi nyingi kujipatia Uhuru, wale viongozi wa kwanza na wapigania uhuru wengi wao walijisahau. Badala ya kuwatumikia wananchi wakajikuta wanalewa madaraka, wakawa walafi na mafisadi na idadi ya kutosha wakageuka kuwa madikteta ghafla.
Huzuni ilitanda upya Afrika pale ambapo viongozi kutoka mataifa mengi yaliyopata Uhuru; waliporudi kuwapigia magoti wakoloni. Badala ya kubuni mikakati ya kujitegemea wakawa kiguu na njia kwenda kuomba misaada kwa wale wale waliowatawala.
Mataifa mengi yakageuka kuwa tegemezi na mengi yao hadi leo hayana jeuri ya kujitegemea kwa asilimia 100 kiuchumi, kijeshi na kijamii. Hata hivyo hali haijabaki vivyo hivyo hadi sasa; kwani mambo yanabadilika mno Afrika.
Tuonane wiki ijayo katika sehemu ya pili ya makala haya. Waafrika ni wakati wetu wa kung’aa kiuchumi.