Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Makete
AFISA Mhifadhi mkuu wa Kanda ya Kusini Jonathan Kaihura ametoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo katika hifadhi zetu hapa nchini na hasa Hifadhi ya Taifa za Kitulo iliyopo mkoani Njombe wilayani Makete na Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Rungwe na Mbeya vijijini.
Amesema kuwa mara zote pamekuwa na dhana ya kwamba wanaopaswa kutembelea na kufanya utalii ni wageni kutoka nje ya jambo ambalo si sawa hivyo ni vema Watanzania wakajenga utamaduni wa kufanya utalii kwenye hifadhi mbalimbali hapa nchin
Kaihura ametoa wito huo leo Januari 22 ,2024 wilayani Makete wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wamejikita katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Akizungumzia Hifadhi ya Taifa ya Kitulo amesema hifadhi hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2005 na kwamba ni moja ya hifadhi muhimu ambayo inapatikana nyanda za juu kusini ambapo imezungukwa na mikoa miwili ambayo ni Njombe na Mbeya.
Amesema kuwa Hifadhi ya Kitulo ina vivutio vya kustajaabisha saba, huku akitolea mfano uwepo wa Waterfall ambayo maji yanatirirka msimu mzima, lakini pia kuna bustani nzuri sana ya maua ambayo ni uoto wa asili lakini kubwa kuliko mandhari yake ni ya kipekee
“Hapa Kitulo hakika Mungu ni wa ajabu sana na amepapendelea sana nadhani mmeona pale kwenye chanzo ambapo maji yanatiririka msimu mzima na pamepewa jina la Mwakitelima ambaye ndiye alikuwa Mhifadhi mkuu wa kwanza katika hifadhi hii ya kitulo “amesema Kaihura.
Ameongeza kuwa licha ya chanzo hicho lakini pia Kuna maporomoko ya msitu wa mto Nhumbe yote hayo yanapatikana katika hifadhi ya Taifa ya kitulo hivyo watanzania waje kutembelea vivutio hivyo watafurahi na wataburudika.
Amefafanua kuwa hata gharama za kuingia kwenye hifadhi hiyo ni rafiki sana na hata sehemu za maradhi gharama zake ni rafiki sana ambapo kulala katika nyumba zilizopo kwenye hifadhi usiku mmoja ni sh.29000 tu lakini pia huduma za chakula vinywaji vyote vinapatikana ndani ya hifadhi.
Pia amesema ndani ya hifadhi hiyo pia kuna wanyama kama swala na wanyama wengine lakini mwa upande wa maua kuna aina 45 za maua lakini pia kuna mimea aina mbalimbali inapatikana hivyo ni fursa azmu kwa Watanzania kuendeleza kuunga mkono juhudi za Rais DKT. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vilivyopo nchini Tanzania.
Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ipo mita 2900 kutoka usawa wa bahari na inazunguka katika mikoa miwili ambayo ni mkoa wa Njombe katika Wilaya ya Makete lakini pia katika Mkoa wa Mbeya na hasa Mbeya vijiji pamoja Wilaya ya Rungwe mhifadhi mkuu wa kwanza wa hifadhi hiyo alikuwa anaitwa Simon Mwakilema .