BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Afrika.
Pia, AfDB imesifu juhudi za Serikali ya Tanzania kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini.
Rais wa AfDB, Akinwumi Adesina alitoa pongezi hizo Dar es Salaam kwenye majadiliano katika siku ya kwanza ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika Kuhusu Nishati.
Mkutano huo unalenga kuimarisha juhudi kuhakikisha umeme unawafikia watu milioni 300 Afrika katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
“Wanawake milioni 1.5 hawana nishati safi ya kupikia barani Afrika, lakini kila mwaka wanakufa zaidi ya watoto na wanawake 300,000 wanakufa kwa maradhi ya mfumo wa hewa kutokana na matumizi ya nishati chafu, hili halikubaliki,” alisema Dk Adesina.
Alisema AfDB imemuunga mkono Rais Samia kwa kutoa Dola za Marekani bilioni mbili kuhakikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia inafanikiwabarani.
Dk Adesina alisema utekelezaji wa ajenda hiyo utabadilisha maisha ya Waafrika na kuifanya ipate suluhisho la nishati safi ya kupikia na akasema Tanzania imeanza kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia.
Rais Samia alizindua mkakati huo Mei mwaka jana na aliiagiza Wizara ya Nishati ikae na wadau kubaini maeneo ya kuboreshwa kusaidia upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Alisema asilimia 90 ya Watanzania bado wanatumia nishati isiyo rafiki. Alisisitiza umuhimu wa kusimamia utekelezaji wa mikakati hiyo ili kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ifikapo 2033.
“Kila mmoja anawajibika na kila nchi inapaswa iwe na ajenda ya nishati safi ili tuwaokoe wanawake na watoto, hakuna sababu ya wao kufa kwa madhara ya nishati chafu, tuwe na mfumo wa tathmini na ufuatiliaji kutekeleza hilo,” alisema Dk Adesina.
Amesifu juhudi za kusambaza umeme nchini Tanzania kwa kuwa vijiji vyote vimefikiwa na nishati hiyo.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Tanzania inazalisha umeme wa kutosha na kwamba kwa sasa zinazalishwa megawati 3,410 na mahitaji ni megawati 1,888.
“Tunakwenda kufikia megawati 5,000 mwisho wa mwaka huu, tukakwenda megawati 10,000 pengine mpaka 2030 ambako tunakwenda kwenye hiyo misheni 300 kwenye kuwapelekea Waafrika milioni 300 umeme,” alisema Msigwa.
“Tunachotaka kuona ni sekta binafsi zinashirikishwa na kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya gridi ambayo itapata fedha kusaidia wazalishaji wadogo wa nishati hiyo kutoka vyanzo vingine kama nishati jadidifu,” alisema Dk Adesina.
Alisema taasisi za kifedha zimeshiriki mkutano huo na zinahitaji sekta binafsi ili zifanikiwe kwa kuwekeza kwenye maeneo ambayo hajayafikiwa kuwa na miradi ya gridi.
Alisema ili kufanikisha na kushirikisha sekta binafsi kikamilifu, kunahitajika mapitio ya sera, mifumo na mazingira thabiti ya manunuzi iwe wazi na yenye ushindani. Alisema pia gharama za mitaji zisiwe kubwa bali nafuu na mikopo itolewe ya muda mrefu.
Dk Adesina alisema ili kukabili changamoto ya uhamiaji, ni muhimu kutoa fursa za ajira kwa vijana Afrika na hivyo umeme wa uhakika unahitajika.
Mkutano huo unaratibiwa na Benki ya Dunia, AfDB, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Tanzania.