Bibi Carolina Tibakwegomba aliyezaliwa mwaka 1902 katika Kijiji na Kata Kitendagoro, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 113.

Mkuu wa ukoo wa Abakoba, ambao ni ukoo wa bibi huyo, Mzee Khasim Abdalah Karuandila (80) anasema bibi huyo alifariki hivi karibuni baada ya kuugua.

Katika umri wake wa miak 113 alizaa watoto sita, akafanikiwa kupata wajukuu 29, vitukuu 92 na vilembwe 3. Watoto aliowaacha yupo mwenye umri wa miaka 89.

 Mama huyo aliolewa na Mzee Rugimbana akazaa watoto watatu wawili kati ya hao walifariki wakiwa bado wadogo na akabaki Alfred Rugimbana aliyezaliwa mwaka 1932.

Baadaye Rugimbana alioa mke mwingine jambo lililomkera Bibi Tibakwegomba akaamua kuondoka mwaka 1936 na kuolewa kwa Mzee Baitani Ndyamukama kijiji cha Kitwe Kitongoji Kabale, Wilaya ya Bukoba vijijini.

 Bibi huyo alizaa watoto wengine watatu wa kiume alikoolewa mara ya pili ambao ni Clement Baitani aliyezaliwa mwaka 1937, Leopord Baitani mwaka 1940 na Leonard Baitani mwaka1942 na mwaka 1948 alitoka na kuolewa tena kwa Mzee Jeremiah Banyenza wa kijiji cha Kyanyonyi, Kata Bujugo Wilaya Bukoba viijini. Huko nako alizaa watoto wawili John Jelemiah mwaka 1949 na Immaculatha Jelemiah 1952.

 Mtoto wake Immaculatha (63) anasema: “Baba yetu alipouza shamba letu la Kyanyonyi akanunua shamba jingine huko kijiji cha Izimbya Kitongoji cha Iboyero alioa wake wawili huko na ndilo kosa lililomtoa mama na aliamua kuishi na kaka yetu mkuu Mzee Alfred Lugimbana huko Kiziba alikokuwa amejenga.”

 Immaculatha anasema tangu mwaka 1984 mama yake Tibakwegomba aliamua kukaa kwa mwanae hadi mwaka 2001, wakati mjukuu wake alipomunulia shambata Kibeta.

 “Nilinunuliwa shamba na mwanangu Kamugisha huko Kibeta Mtaa wa Omukituli na nikaamua kuishi huko na mama yangu tangu mwaka 2001 hadi Octoba,2015 mama aliponitoka mikononi mwangu,” Immakulatha.

 Mtoto wake mwingine Baitani ambaye ni Mtakwimu Mstaafu wa Mkoa wa Kagera, anasema mama yake alipata kuwambia kuwa pamoja na kuelewa mara nyingi hakuwahi kufanya kosa wala kupigwa na mumewe yeyote isipokuwa alikuwa akiamua kuondoka kila walipomuudhi.

 Julai, mwaka 2014 alibatizwa na Padri Christopher Mpambo kutoka Ofisi ya habari aambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari Jimbo Katoliki la Bukoba aliyembatiza kwa jina la Caroline.

 Mkuu wa Ukoo Kassim Abdallah aliyeteuliwa na Father James Rugemalira, anasema mama huyo alikuwa nguzo ya umoja katika ukoo wao.

Mzee Abdalah anasema historia ya ukoo wa Abakoba walianzia Mtaa wa Kafuti, Bunena kwenye ufukwe wa Ziwa Victoria na ukapewa heshima ya pekee ya kuitwa Kata Bakoba, japo hakuweza kutaja ni mwaka gani kwa maelezo kuwa alikuwa hajazaliwa.

 Anasema baadhi ya familia zilihama, ikiwamo familia ya Bibi Tibakwegomba iliyohamia Kitendaguro, wengine walielekea Itahwa, Ibwera, Kishogo na vijiji vilivyoko Wilaya ya Bukoba Vijijini, huku wengine wakihamia Kagoma, wilayani Muleba.

 Historia ya ukoo wa Abakoba inaelezwa kwa undani na Mwalimu mstaafu Alphonce Rwezahula (62), maarufu kama Bwikizo anayesema Abakoba walitokea Isheshe nchini Uganda, ambapo Kijiji cha Isheshe kwa maajabu kilikuwa kinaelea juu ya Ziwa Victoria kwa miaka mingi hadi Wahaya wakakiita “EKISHAMBARA”, lakini baadae kilisukumwa na upepo wa ziwani hadi eneo la Kafuti ambalo hatimaye yaligeuka makazi ya Abakoba, wlaioishi katika kijiji hicho cha maajabu.

 Aansema siri ya mama huyo kuishi muda mrefu ni kula vyakula vya asili ikiwamo mihogo, viazi vikuu, viazi vitamu, karanga na mahindi pamoja na maarage bila kusahau matunda mwitu ya aina za amashaasha, emoi, nkerere. Kwa upande wa mboga Tibakwegomba alipendelea kula maini yaliyochomwa.

 

0684-305555/0755-301474.