Karibu kila mwanachama wa Simba ambaye anaonekana kwenye runinga akizungumzia mustakabali wa timu hiyo, anakosa hoja nzito yenye mashiko.
Kila anayemkaribia mwandishi wa habari wa kituo cha runinga anaizungumzia Simba kwa uchungu kwa sababu tu timu haijafikia lengo lililokusudiwa.
Hajasikika hata mmoja mwenye kuzungumzia uhusiano wa uongozi wa timu bila ya kujali matokeo ya uwanjani. Kinachomuuma shabiki wa Simba ni kuiona Yanga ikifanya mambo yake vema, huku klabu anayoipenda ikiwa haijafikia lengo wanalolitaka.
Wivu mzuri wa maendeleo ndio unaotawala maoni ya Mwanasimba, ingawa anashindwa kuelewa ukweli kwamba hata kama klabu itakuwa chini ya mikono ya watu tofauti na hawa wa leo, bado inaweza kuwepo misimu ya majonzi pia. Simba ni timu kongwe, jengo la klabu pale Msimbazi lilijengwa mwaka 1971.
Miongo minne iliyopita, wakati Jiji la Dar es Salaam likiwa na maghorofa machache yenye ghorofa zaidi ya kumi na kuendelea, wakati ambao hata idadi ya magari mjini ilikuwa ni ndogo sana pengine chini ya 100, Simba ilikuwa na umri wa zaidi ya miaka 30.
Wanachama wengi wanaotoa maoni yao juu ya mustakabali wa Klabu ya Simba, walikuwa aidha ni watoto wadogo wakati jengo la Msimbazi linajengwa au hawakuwepo kabisa duniani.
Dunia ya mwaka 2016 inayo mengi mapya kabisa, yenye kupaswa kuwa ndani ya fikra za mwanachama au shabiki wa Simba wakati akijadili hatima ya timu aipendayo. Kushindwa kubeba kombe lolote kwa zaidi ya misimu minne wala hakupaswi kuwa kigezo cha kumuondolea kabisa busara Mwanasimba kiasi cha kuishia kuwa na mawazo ya timu kuongozwa na mtu atakayeleta mafanikio peke yake.
Wapo wanaotaka utaratibu wa sasa wa wanachama kuwa na mamlaka na sauti ya mwisho kwenye uamuzi wote uendelee kama ilivyozoeleka. Ulisikia walichotaka kwa Mohammed Dewji?
Pande zote mbili zinakutanishwa na mapenzi kwa Klabu ya Simba kwanza, kabla ya jambo jingine lolote. Ikiwa Wanasimba wanakubaliana na wazo la Mo Dewji kupewa klabu kama ambavyo amesikika akisema, basi yapo ya msingi yanayopaswa kushughulikiwa kwanza. Simba iondokane na utaratibu huu wa sasa na isajiliwe kama kampuni.
Taratibu zote za usajili wa kampuni zifanyike na zieleweke kwa kila mdau wa Simba. Baada ya hapo Simba isajiliwe katika uuzaji wa hisa zake pale Dar es Salaam Stock Exchange (DSE). Lakini kabla ya kufika kote huko ni lazima kwanza mabadiliko ya msingi yafanyike kwenye katiba.
Kwamba timu inaondokana na utaratibu wa kuwa mali ya kila mwanachama na kubadilika kuwa kampuni ambayo wanachama ndio wanabadilika na kuwa wanahisa.
Mabadiliko hayo ya msingi yatamuwezesha kila Mwanasimba kutambua kuwa anao wajibu wa kuilinda mali anayoipenda, hivyo anao pia wajibu wa kutambua nafasi yake katika mazingira mapya ya kampuni ya Simba.
Hamisi Kilomoni
“Sina tatizo na Mo, ila anatakiwa aje mezanii tukae tuzungumze, tunapaswa tukae mezani kwa masilahi ya kalbu.
“Tunachotaka katika Simba ni kwamba kila kitu kiwe wazi na kusiwe na mambo ya kuzungushana, wote tunataka tutoke hapa tulipo, lakini klabu kwanza,” Kilomoni amewahi kunukuliwa akisema.
Anachokitaka Kilomoni ni kuwa na wanahisha watatu ambao watagawana asilimia 49 kama serikali inavyotaka.
Mo Dewji
Wakati Kilomoni akiwaza yake, bilionea huyo wa Simba, Mo Dewji, ameamua kuongeza fungu ndani ya klabu ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
“Kuwekeza kwangu ndani ya Simba kumeifanya timu iwe na nguvu kubwa ndani na nje ya nchi na haya ni mafanikio makubwa,” anasema Dewji.
Msimu uliopita Simba inadaiwa kutumia kiasi cha Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya wachezaji, huku Dewji akidaiwa kuongeza fedha msimu huu.
Sikia hii
Simba isije kuingia mkenge jumla jumla kwa kuuza hisa wakati yenyewe bado inao muundo usioendana na mahitaji ya ulimwengu wa biashara za kikampuni. Litakuwa ni kosa ambalo litajutiwa na kila atakayeshiriki katika kufanikisha tendo hilo la kutowapatia haki Wanasimba kwenye zoezi zima la kuibadilisha Simba kutoka kuwa klabu ya wanachama kuwa kampuni.
Shabiki au mwanachama wa Simba wala asiwe tayari kukurupuka akidhani kwamba mabadiliko mepesi ya uongozi yanaweza kuja na furaha ya uwanjani itakayodumu kwa misimu mingi ijayo.
Fedha ya mtu mmoja inaweza kutumika kama chambo cha kuzitega fikra na mitazamo ya wanachama wengi lakini si hakikisho la furaha ya kudumu. Wanachama wanao uwezo wa kuwa na sauti kwa kuwa wanahisa ndani ya Simba mpya yenye sura ya kampuni.
Na wala hawataishia kuwa na umiliki wa asilimia hizo peke yake, wanao uwezo wa kuongeza wingi wa asilimia zao kwa sababu wakati wa mabadiliko kutoka katika uendeshaji wa sasa kwenda kwenye uendeshaji wa kikampuni, wao walibakia kuwa na sauti.
Simba yenye umri wa miaka 80 ni mojawapo ya taasisi muhimu sana za kijamii na hata kisiasa. Isije kuyumbishwa na kuja kupoteza heshima yake.
Labda majungu yanaweza kuwa yanatumika katika kujenga hoja dhidi ya uongozi wa sasa wa Simba. Na si jambo la ajabu kwa kutazama uzoefu na hulka za klabu zetu.
Kwani upo uwezekano hata huu uongozi unaowekwa kwenye mazingira ya kujitetea, uliingia madarakani kwa kutegemea siasa hizi hizi za baadhi ya watu kutumika kwa nia mbaya.
Lakini yote kwa yote ipo haja kwa kila Mwanasimba kuwa makini na kila hatua inayoendelea wakati mjadala wa hatima ya klabu ukiwa unaendelea.