Nilipoipeleka mahakamani barua ile, nikaambiwa wasipopata ‘Deed of Settlement’ baada ya miezi 2 kupita Baraza la Nyumba litaendelea kusikiliza maelezo yangu na kupokea vielelezo vyangu kisha litoe uamuzi bila ya CCM kuwapo. 

Miezi miwili kuanzia mwezi Machi ikamalizika bila CCM kutoa ile ‘Deed of Settlement.’ Kukawa kimyaa kama vile hakuna jambo jipya. Mimi nikarudi Mahakama ya Ardhi na Nyumba na kusema sijaona barua yoyote. Baraza wakasema wataendelea kusikiliza ombi langu. 

Tarehe 27/11/2015 Baraza lilinisikiliza kuanzia saa 5 mpaka 6:30 nilipomaliza kutoa madai yangu pamoja na vielelezo vyake, ndipo ikapangiwa tarehe 22/12/2015 siku ya kutolewa hukumu. Kwa sababu zisizozuilika tarehe ile 22/12/2015 haikuwezekana kutolewa hukumu. Hatimaye tarehe 05/02/2016 saa 7 mchana Mahakama ile ilisoma hukumu ya kesi No. 40/9.

Tarehe 17/02/2016 nilikwenda kupokea hiyo hukumu yenyewe ‘Court Judgement’ iliyosema hivi: In the District Land and Housing Tribunal for Kinondoni District at Mwananyamala LAND APPLICATION NO. 40 of 2009 EX – PATRE JUDGEMENT before M. Lyambina, Y. J. CHAIRMAN – At the outset, the Court dares to point that Brig General FX Mbenna has proved on balance of probability that he is the sole owner of Plot No. 387……The Tribunal doth hereby order that: 1 The 2nd Applicant is declared lawful owner of the suit Plot No. 387 Jangwani Beach, Kinondoni Municipal…..

Nilipata haki yangu ya kumiliki kiwanja No 387 na Mahakama iliteua dalali kubomoa vibanda vile vya CCM vilivyojengwa kinyume cha sharia katika kiwanja changu. Huo ndiyo ukawa mwisho wa ubabe wa CCM kuvamia ardhi kinyume cha utaratibu.

Dalali kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba aliwapa ‘Notice’ ya kubomoa ofisi zao hao CCM, lakini kwa kutokufanya vile siku ilipofika ubomoaji wa ofisi ulifanyika na dalali. Cha kushangaza, ndani ya hiyo iliyokiitwa ofisi ya Tawi Kilongawima mlikuwa na kitanda 1 na godoro lake, pikipiki moja na baiskeli; hapakuwa na meza wala kiti wala kabati lenye kuonesha ilikuwa ni ofisi. Je, huo siyo ufisadi? Kisingizio cha ofisi ya CCM huku wajanja wanakula. Nje ya ofisi kulikuwa na genge la mama ntilie kuandaa vitafunwa kwa wafanyakazi wa ujenzi wa pale Art Gallary. Hakutokea kiongozi yoyote wa CCM kuja kuchukua vile vilivyokuwa mle ndani. Dalali akavichukua vikawa ‘No body’s property’. 

Hii ndiyo Bongo. Ilikuwa ni dili ya viongozi wa CCM kupata mshiko bila jasho hapo. Kiwanja changu kikawa kitegauchumi cha wajanja kwa kutumia mgongo wa CCM. 

Niliona nieleze wananchi maneno yote waone namna nchi inayojengwa na wenye moyo lakini pia inayotafunwa na mafisadi kwa ngozi ya kondoo CCM. Hapo imani kwa CCM inajengwa au inabomolewa? 

Niliposikia Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, anataka kujua mali zote za Chama na ziorodheshwe, nikasema sasa wale wachumia tumbo waliokiimba ‘CCM ina wenyewe’ wakati uliopita, sasa wataumbuka. CCM ni chama dume, chama tawala kinapaswa kuwa kina haki na kinaongoza kwa uadilifu wake. 

Kuna usemi wakirumi wa kale kuwa ‘Non in Quantitate SED in QUALITATE’ yaani siyo katika wingi bali katika ubora. Makada wa CCM wawe wachache lakini wawe na imani thabiti juu ya chama. Wawe waumini wa kweli. Wasidhulumu wanachama wenzao. Utitiri wa wanachama wanaoganga njaa hakutakijenga chama. 

CCM isijivunie wingi wa wanachama bali ijivunie ubora wa hao wanachama wake kimaadili. Kiongozi katika kulinda haki za wananchi kusiwe na wababaishaji na mafisadi. Dira ya chama iwaongoze wananchi wa Taifa hii. Kamwe kisiwalinde viongozi wababaishaiji na wasioweza hata kutii kwa viongozi wa juu na wasiopuuza miongozo kutoka makao makuu ya chama. Chama kikifikia hali ya katibu wa tawi anashindwa kutekeleza miongozo ya kutoka makao makuu ya chama chake.

Hapo kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili. Hatua za haraka zichukuliwe kukinusuru chama. Makatibu namna hiyo waadabishwe mara moja ili kukijengea chama ile hadhi yake ya kule tulikotoka miaka ya 1958. Katibu wa tawi ni mhimili muhimu wa chama. Agizo la Katibu Mkuu wa Chama ni amri wala siyo suala la kujadiliana bali ni utekelezaji tu, basi. 

Ni matumaini yangu kuwa ziara za Mkuu wa Mkoa katika wilaya za Jiji la Dar es Salaam zitakijengea chama heshima ile ya zamani ya kutatua kero za wanyonge waliodhulumiwa kwa muda mrefu. Dhuluma kutoka viongozi wa matawi ya chama, Serikali za Mitaa na kuendelea. 

Nilipata kumsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika safari zake katika wilaya za jiji akiwaambia wananchi; “Nadhani itakuwa vigumu kwa maafisa ardhi kuingia peponi”. Mara moja nikakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere kwa waandishi wa habari pale Kilimanjaro Hotel Machi 14, 1995 alipoongelea suala la rushwa, aliwahi kutamka hivi namnukuu; “Tajiri kwenda peponi ni vigumu zaidi kuliko ngamia kuingia katika tundu la sindano (Nyufa Uk. 20 ibara ya pili mstari wa 3).

Hawa wote wawili, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na Baba wa Taifa wanachokisema ni marejeo ya matamshi ya Bwana Yesu Kristo kwa matajiri wa Kiyahudi enzi hizo. Tunasoma hivi, “Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu” (Marko sura ya 10 mstari ule wa 23).

Hapo ndipo Mkuu wa Mkoa alipowatahadharisha Maafisa Ardhi kwa ile tabia yao ya kujirundikia mali kupitia viwanja vya wananchi wanyonge, maskini, hohehahe waliodhulumiwa ardhi yao, basi kwa wadhalimu wote kwao ingekuwa vigumu kuingia peponi maafisa ardhi wa Dar es Salaam.

Nimekuwa napokea SMS nyingi au pengine kupigiwa simu na wasomaji wa makala zangu katika JAMHURI wakiniambia “mbona unasakama sana Ukawa hao CCM unawaogopea nini?” Wewe ni kada wa CCM, na unajikomba ili Magufuli akuone upate ukuu wa mkoa. Moja ya meseji za ushauri inasomeka hivi: 

“Sms kutoka 0676 581089 ya tarehe 7 Oktoba, 13:26 hrs. Mhesh. Umelitumikia Taifa kwa weledi nakushauri usijiingize katika uandishi wa masuala ya kisiasa. Watanzania wanataka mabadiliko. CCM haina uwezo wa kuivusha nchi hii hapa ilipo, kuanzia mjumbe wa nyumba kumi anakula rushwa hadi ngazi ya kitaifa, dhambi kutetea maovu, tambua kuna maisha nje ya Serikali ya CCM. Tulia, kula pensheni yako taratibu, ukipenda sana CCM waweza kupata matatizo ya msongo wa mawazo pindi itakaposhindwa.”

Kelele za mpita njia hazimzuii mwenye nyumba kulala usingizi. Mimi nilijikita katika somo la uraia. Nimeandika makala juu ya udini, ushoga, elimu, utawala bora, demokrasia humo kuna mambo ya Ukawa na CCM? Leo hii nimeandika juu ya ardhi ‘Double allocation’ ni Ukawa au ni CCM? Nategemea wasomaji kuwa wapevu (matured) na wenye upeo mkubwa na siyo kujielekeza kwenye vyama vya siasa. Huo ni ufinyu wa fikra tu. Mtu haishi kwa siasa tu bali kwa kujifanyia kazi za kipato cha halali. 

Tuongelee ‘issues’ za nchi siyo suala la nani kapata madaraka gani. Umri wangu sasa ni miaka 87 huo ukuu wa mkoa nitaufanyia nini? Sheria katika nchi yetu watu wanang’atuka katika umri wa miaka 60. Mimi nilistaafu katika umri wa miaka 58 mwaka ule 1988 basi vijana msiwe na hofu haiwezekani mkongwe kuajiriwa. Ninaomba tuone ‘gist’ ya somo na siyo kwa jicho la chama tawala au Upinzani.

Hayo kwangu siyo muhimu. Wazo kuu ni ile elimu ya uraia tunaita ‘civics’ ndiyo inayotolewa hapa. Tusiwe daima tunaongelea au tuna mtazamo wa kisiasa tunaita “political outlook” yaani ‘politics’. Siyo kila makala inalenga siasa za chama tawala au upinzani. Huo Waingereza wanaita ‘myopic outlook’ mtazamo finyu. Watu wote waliopevuka kiakili na kielimu huwa na mtazamo wa kimaendeleo zaidi na siyo wa kisiasa. 

Mtawala anatazamiwa kuwahudumia watawaliwa wote wa nchi anayotawala pasi mwegemeo wa mlengo wake wa kisiasa. Ndivyo ninavyoamini. Hata matamshi ya Rais mteule wa Marekani baada ya uchaguzi yamebadilika kuwa ya kitaifa na siyo ya kichama kama ilivyokuwa wakati wa kampeni. 

Tanzania yetu sote. Ukitoboa mtumbwi basi sote tutazama. Mungu ibariki Tanzania. 

 

>>TAMATI