H
adithi hii ya kale inaonesha mambo mawili muhimu kwanza kusikiliza pande zote mbili za kesi papo hapo wote wakiwa hapo, na pili kutoa uamuzi kwa kutumia hekima na busara. Hapakuwa na kitu kama mention wala kitu vielelezo (exhibits) wala mashahidi, wakiwamo wapambe na matapeli wachumia matumbo kama inavyotokea. Mahakamani siku hizi nchini pote wamejitokeza mawakili lukuki kungojea kutetea kesi za ‘double allocation.’
Katika Baraza la Ardhi na Nyumba hapo Kinondoni, nilianza kusikilizwa maombi yangu ya kuwaondoa wavamizi CCM Tawi la Kilongawima na Aidan Ibrahim Mongi kuanzia tarehe 16/3/2009 mbele ya Mwenyekiti, Mhesh Davis. Kukaanza na ule ule ukiritimba wa ‘mention.’ Tarehe 3/4/2009 sasa ikawa ‘mention’ kwa Baraza la Wadhamini wa CCM na siyo Tawi la Kilongawima tena. Tarehe 20/7/2009 ikawa imeanza kusikilizwa. Nilitoa malalamiko yangu juu ya uvamizi uliofanywa na CCM.
Nikaelezea, wavamizi hawana ‘offer’ yoyote tungesema kuna “double allocation.” Isitoshe CCM hawalipi kodi ya kiwanja na wamejenga ofisi ya tawi kwa ubabe bila hata kuwa na ‘Building Permit’ maana hakuna mamlaka iliyowapa ploti ile. Baada ya mimi kutoa vielelezo vyangu mahakamani, ikapangwa kuwa tarehe 30/7/2009 CCM waje wajitetee.
Badala ya kuja kujitetea CCM (mwanasheria) walikuja na ombi la kutaka shauri hili limalizwe nje ya mahakama kwa mazungumzo kati ya mimi na CCM. Nilikubali kulinda heshima ya chama (mbona huko nyuma suala namna hii lilipoletwa Mahakama Kuu katika kesi No. 266/98 nilikubali na mambo yakamalizika kwa amani?) Hivyo nilitegemea tutayamaliza.
Kuona CCM hawana kielelezo hata kimoja kuonesha kiwanja kile walipewa na mamlaka halali ya nchi hii wakachukua hatua kimya kimya kuagiza ofisi ya CCM Mkoa iagize Wilaya Kinondoni, kuondoa ofisi yao ya tawi pale Kilongawima, ili mrejesho upelekwe Baraza la Ardhi na Nyumba kuwa shauri tumesharidhiana na kiwanja kimerejeshwa mikononi mwangu na hivyo kuomba Baraza lifunge kesi au ombi lile Na. 40/9 kuwa limemalizika.
Tarehe 29/10/2010 CCM makao makuu ofisi ndogo waliiandikia CCM Mkoa kuitaka utekelezaji wa uamuzi wake ule. Tarehe 7/1/2011 CCM Wilaya ya Kinondoni ilitoa amri kwa Katibu Kata CCM Kunduchi Kumb. Na. CW/KN/U.25/4/9 ya tarehe 07/01/2011 yenye kichwa cha habari “Ujenzi wa jengo CCM tawi la Kilongawima.” Humo kulitolewa agizo/amri kusema. ….“kwa barua hii simamia kuvunja jengo lililopo katika eneo hilo na kuondoa mali zilizopo. Zoezi hili lifanyike mara moja bila kuchelewa. Aidha nakuletea vielelezo vya baraza kutoka ngazi ya juu.”
Ofisi ya Tawi Kilongawima hawakutekeleza amri ile ya chama na waliendelea kutumia kiwanja changu kama vile wao uamuzi wa ngazi ya juu haukuwahusu. Kuona vile niliuliza ofisi ya sheria, kuna nini? Twende mahakamani kupeleka mrejesho wa makubaliano nje ya Mahakama. Kilichojitokeza kwa mtazamo wangu, hakuna aliyekuwa tayari kutoa uamuzi wa kupeleka mahakamani. Basi nilikwenda kwa wakili wangu kupata barua rasmi kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa mali ya chama nipate uamuzi. Kiutaratibu tawi halina mali hivyo ni Baraza la Wadhamini ndilo lenye kauli juu ya mali za chama.
Tarehe 27/7/2012 nilikwenda kumuona Mwenyekiti Baraza la Wadhamini wa CCM pale ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Mzee Peter Kisumo, (sasa ni marehemu). Nikamkabidhi barua yangu ya malalamiko, CCM inavyonicheleweshea kukiendeleza kiwanja changu No. 387 Jangwani Beach. Nikampa na barua kutoka Wakili wangu Kumb. No. FK/CP/Civil Case No. 266/ Action Attorney, Dk. Mapunda AM ya tarehe 27/6/2012. Mzee Peter Kisumo, Mwenyekiti hakuelewa CCM ikoje. Matokeo ya kukutana kwetu, Mwenyekiti yule alitoa uamuzi wa CCM juu ya kiwanja kile.
Katibu Mkuu CCM, Wilson C. Mukama, aliandika barua Kumb. No. CCM/OND/636/VOL III/50 ya tarehe 27/7/2012 kuagiza mkoa uchukue hatua kuondoa vibanda vya CCM ambavyo vimejegwa kwenye kiwanja hicho kinyume cha sheria mkoa urejeshe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo la makao makuu ofisi ndogo Lumumba. Barua ile iliendelea kusema, kinyume chake Baraza la Wadhamini wa CCM halitahusika na hatua yoyote itakayochukuliwa na Brig. Gen. Mbenna au mawakili wake kutokana na kukaidi kutekeleza maelekezo na maagizo ya makao makuu.
Inavyoonekana, katika CCM hakuna kile tunachokiita “chain of command,” yaani utiifu wa amri au utawala wa kisheria haupo kabisa. Wangali na fikra zile zile za CCM kushika hatamu. Tawi la Kilongawima likatunishiana misuli na makao makuu. Hawakubomoa vibanda wakandelea ‘business as usual’ kwa maana nyingine CCM ilishindwa (ofisi ya sheria) kutoa tamko la makubaliano nje ya Mahakama.
Tarehe 11/3/2014 nikarudi mahakamani Baraza la Ardhi na Nyumba kuishitaki CCM kwa kukalia eneo langu kimabavu. Baraza kwa uzoefu wao na busara za kuitunzia heshima chama tawala wakaniomba nirudi CCM wanipe kile kinachoitwa ‘Deed of Settlement’ nipeleke mahakamani wakatoe uamuzi wa kisheria kumaliza kesi ile No. 40/9 ya tangu 2009.
Kuna wazee wa CCM wakanishauri nitumie hekima wala chama tawala nisikishtaki bali nimuone Katibu Mkuu, Col. Kinana, nikimweleza atalimaliza tu. Nikaenda ofisi ndogo ya CCM tarehe 26 Feb 2014 siku ya Ijumaa saa 4 asubuhi tukaongea na Katibu Mkuu akasema atalishughulikia haraka iwezekanavyo.
Tarehe 25/4/2014 tukiwa katika ukumbi wa PTA huko Temeke katika ‘occasion’ ya Rais Kikwete kuwapokea vijana waliotembea kwa miguu kutoka Dodoma, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kusini na Kanda ya Nyanda za Juu, Katibu Mkuu alinikabidhi kwa Mzee Madabida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, kwa maelezo wameshaongea na hana shaka huyo mwenyekiti atamaliza tatizo langu. Nikawa mtu wa matumaini kweli kwamba sasa suala lile la kiwanja litafikia tamati nitaweza kupeleka mrejesho Mahakama ya Ardhi Kinondoni na hivyo kufunga kesi ile.
Wapi jamani, mambo hayakuwa hivyo. Nikaanza kupigwa dana dana upya. Kila nikienda ofisini, Mwenyekiti wa CCM Mkoa ananipa kisingizo kipya. Basi tarehe 8/1/2015 nilipomuuliza kwa meseji juu ya mihadi yetu ya kuonana nilipokea SMS kutoka Zanzibar iliyosema “Brig. Mbena Shikamoo. Niko Zanzibar nimekuja kwenye sherehe za Mapinduzi. Tafadhali ninaomba uje Jumanne. Utaniwia radhi kwa usumbufu. Time 07:34:57.” Hapo sikuwa na la kufanya nilishukuru kwa taarifa hiyo kuwa Jumanne tarehe 13 Januari ifikapo tutaonana.
Ile Jumanne tarehe 13 Januari 2015 tuliyokubaliana huyu Mwenyekiti wa CCM Mkoa hakuwapo ofisini, hivyo hatukuonana. Lakini tarehe 20/1/2015 Mwenyekiti Mkoa alinipigia simu saa 1:35 asubuhi kuniarifu niende Makao Makuu ya CCM Ofisi ndogo kupata taarifa kamili. Nilipofika CCM Ofisi ndogo sikupata maelezo wala barua yotote. Ofisi ya sheria waliniambia hawajui lolote na wala hawakuongea na Mwenyekiti wa Mkoa. Ofisi ya Katibu Mkuu PS akaniambia hana maagizo yoyote, hivyo nirudi mkoani wanieleze wazi nikamuone nani hapo ofisi ndogo ya CCM. Sikufurahishwa na danadana namna ile, nikaamua nirudi Mahakama ya Ardhi na Nyumba.
Mahakama ya Ardhi na Nyumba wakashauri sasa niwaeleze CCM, nimechoka kupigwa danadana, ninaendelea na ombi langu mahakamani kusikilizwa upande mmoja yaani bila wao CCM kuhudhuria. Nikapeleka samansi CCM lakini kama kawaida yao hawakufika mahakamani tarehe waliyopangiwa.
Mkoa kwa kuogopa lawama wakamwandikia Mwenyekiti wa Mahakama ya Nyumba barua Kumb. No. CMD/L/20/46/78 ya tarehe 20/3/2015 ikiomba Baraza liwavumilie kwa kuwa taratibu zao za chama zinachukua muda, hivyo CCM wapewe miezi 2 watakuja na uamuzi.
>>ITAENDELEA