Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kitendo cha Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kutomchukulia hatua za kisheria Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, kutokana na ofisi yake kutumia vibaya fedha za umma kinyume cha sheria, kimeupaka matope utawala wake na huenda anamuogopa kiongozi huyo.
Matamshi hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa ADC, Said Miraji Abdulla, katika mahojiano na JAMHURI ofisini kwake Bububu, mwishoni mwa wiki baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar ya mwaka 2011/12 kueleza kuwa ofisi ya Maalim Seif imetumia Sh milioni 299.5 bila maelezo.
Miraji alisema kukaa kimya kwa Dk. Shein na mamlaka yake kutochukua hatua za kumwajibisha kiongozi huyo, hakujengi picha ya maana kwa wananchi na huenda akawalazimisha wananchi kuitafsiri Serikali yake kuwa haifanyi kazi zake kwa njia za uwazi, umakini, uwajibikaji na uadilifu.
Alikitaja kitendo cha kumfumbia macho kiongozi huyo bila ya kumfukuza kazi au kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, hakimpi hadhi na heshima Rais ili kuonekana msimamizi bora wa fedha za umma na kwamba makosa na lawama hizo hazitenganishwi na uongozi wa Rais na chama kilichopo madarakani.
“Ikiwa lengo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar maana yake ni kufichiana maovu, kulindana na kubebana, Dk. Shein ni wazi anamuogopa Maalim Seif na pia hana ubavu wa kumwajibisha anapokiuka sheria,” alisema Miraji.
Alieleza kuwa matumizi ya fedha za Serikali ni lazima yaidhinishwe kwa kufuata taratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, hivyo uamuzi wowote wa kutumia fedha za umma kibabe ni kukiuka na kuvunja misingi ya kisheria na utawala bora.
Alisema ADC inajiandaa kuziandikia nchi washirika wa maendeleo kuwajulisha kuhusu uzembe na ufisadi unaofanyika Zanzibar, ili nao wajue kuwa misaada na fedha wanazochangia kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya jamii, zinatafunwa na wakubwa kienyeji na hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa.
Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa juu wa CUF kabla ya kujitoa na kuanzisha ADC, alisema anashangaa kuiona Zanzibar ikishindwa kusimamia utendaji wenye uwazi, uadilifu, umakini na nidhamu ya kazi, na badala yake kuonekana mfano wa shamba lisilo mwenyewe.
Alisema upotevu holela wa fedha za ruzuku ndani ya CUF ni kama ada na kawaida na kuongeza kuwa hata wao walipokuwa CUF walipoanza kuhoji matumizi wakaonekana vizingiti vya kuwazuia wakubwa wasichote fedha za kujenga nyumba za kifahari, hali isiyotarajiwa kutokea serikalini.
Juhudi za kuwapata wasaidizi wa Rais Shein kuzungumzia habari hizi hazikuzaa matunda, baada ya kila wakati kuambiwa kuwa wamebanwa na shughuli za kitaifa.