Udanganyifu wa ada za wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Moshi kilichopo wilayani Hai unaodaiwa kufanywa na mhasibu wa chuo hicho akishirikiana na mtunza fedha wa ELCT SACCOS umeigharimu Benki ya CRDB na SACCOS hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, ameamua kuzibana taasisi hizo baada ya kubainika kuwa zimezembea kuzuia udanganyifu huo usitendeke. Sh milioni 76 hazionekani kwenye akaunti ya chuo hicho licha ya wanafunzi kulipa ada na kupewa stakabadhi za malipo na chuo hicho.
Udanganyifu huo unadaiwa kuchangiwa na Mhasibu wa Chuo hicho, Sarafina Mbwambo, kuweka ada hewa kwenye akaunti ya chuo huku Mtunza Fedha wa ELCT SACCOS (ambao ni wakala wa CRDB), Baraka Melkzedeck, kutuhumiwa kushiriki udanganyifu huo kwa kutoa risiti hewa kuonyesha kuwa ada hizo zimelipwa.
“Baada ya kuwakamata na kuwahoji mhasibu wa chuo na mtunza fedha wa ELCT SACCOS walikiri kuhusika na udanganyifu huo na baada ya mashauriano tukabaini kinachohitajika hapa ni hizo pesa za wanafunzi,” amesema Sabaya.
Sabaya anasema mhasibu wa chuo cha ualimu na mtunza fedha wa SACCOS kila mmoja atalipa Sh milioni 20; na Benki ya CRDB, Tawi la Hai wametakiwa walipe Sh milioni 12.313; Bodi ya ELCT SACCOS nao wametakiwa walipe kiasi kama hicho, halikadhalika uongozi wa chuo nao umetakiwa ulipe Sh milioni 12.313.
Kuibuliwa kwa udanganyifu huo kunatokana na maandamano ya wanachuo hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai wakipinga kufukuzwa chuoni kwa madai ya kutokulipa ada.
Polisi waliwapiga wanachuo hao waliokadiriwa kuwa 400. Sabaya alifika chuoni na kufanya kikao na wanachuo na uongozi wa chuo.
Sabaya akaagiza wanachuo waendelee na mitihani yao na kuutaka uongozi wa chuo kutowanyima vyeti vyao vya kuhitimu mafunzo ya ualimu pindi matokeo yao yatakapokuwa yametangazwa.
Mkuu wa Chuo hicho, Frederick Akyoo, amezungumza na JAMHURI chuoni hapo na kusema kuwa Novemba, mwaka jana chuo hicho kilifanya ukaguzi na kubaini fomu 487 za malipo ya ada zina utata; na fomu 20 zikionyesha kiwango cha pesa kinachofanana.
“Tulijaribu kuwasiliana na ELCT SACCOS kuwaeleza hili jambo, lakini hawakuonyesha ushirikiano wakisisitiza tuwasiliane na aliyehusika na udanganyifu huo, lakini hili halina ubishi kuwa SACCOS wamehusika kwa sababu risiti zimetolewa kwenye mashine yao waliyopewa na CRDB kama wakala,” amesema.
Kwenye udanganyifu huo, wanafunzi hao wanaonekana kuwa na risiti za malipo halali kutoka CRDB kupitia wakala wao ELCT SACCOS, lakini fedha hazionekani kwenye akaunti ya chuo na risiti hazionyeshi majina yao, lakini zimeambatanishwa na fomu ya kuweka pesa ambayo inayo majina yao.
Katibu wa ELCT SACCOS, Monica Mlay, anasema hawawezi kubeba mzigo ambao si wao na kutaka aliyehusika na udanganyifu huo ndiye awajibike.
“Hatuwezi kuchukua pesa za wanachama kulipia kitu ambacho si kwa matakwa ya wanachama, huo mzigo atabeba mhusika mwenyewe kwa sababu alichokifanya hakikuwa na baraka za wanachama,” amesema.
Julai 31, mwaka huu uongozi wa SACCOS hiyo kupitia kwa Katibu wake, Mlay, uliandika barua kwa uongozi wa chuo: “Bodi ya ELCT SACCOS inapenda mgogoro huu uweze kufikia utatuzi wa amani na kwa maridhiano ya pande zote, yaani chuo, CRDB, wazazi na Kanisa/Dayosisi ya Kaskazini.”
Katibu huyo akawataka wazazi kuwa na subira wakati sakata hilo likipatiwa ufumbuzi. Akawataka wazazi watafute fedha kwingineko wawalipie watoto wao ili waendelee na masomo. Wanafunzi walipinga agizo hilo.
Mtunza Fedha wa SACCOS hiyo, Baraka Melkzedeck, anakiri kuwapo kwa tatizo hilo, lakini anasema hawezi kulipa kwa kuwa hahusiki kwenye udanganyifu huo.
“Hakuna kitu kama hicho ndugu yangu, mimi siwezi kulipa pesa ambayo sijahusika nayo, wao wambane vizuri Sarafina na bahati nzuri hata yeye mwenyewe amekiri kuhusika na huo udanganyifu, sasa mimi nilipe nini?” amehoji.